Hosea 5:1-15
Hosea 5:1-15 SRUV
Sikieni haya, enyi makuhani, sikilizeni, enyi nyumba ya Israeli, tegeni masikio yenu, enyi wa nyumba ya mfalme, kwa kuwa hukumu hii yawahusu ninyi; maana mmekuwa mtego huko Mizpa, na wavu uliotandwa juu ya Tabori. Nao walioasi wameongeza sana ufisadi wao; lakini mimi ndiye awakaripiaye wote pia. Mimi namjua Efraimu, wala Israeli hakufichwa nisimwone; maana sasa, Ee Efraimu, umefanya uzinzi; Israeli ametiwa unajisi. Matendo yao hayatawaacha kumgeukia Mungu wao; maana roho ya uzinzi imo ndani yao, wala hawamjui BWANA. Na kiburi cha Israeli chamshuhudia mbele ya uso wake; kwa sababu hiyo, Israeli na Efraimu watajikwaa katika uovu wao. Yuda naye atajikwaa pamoja nao. Watakwenda na makundi yao ya kondoo na ng'ombe wamtafute BWANA; lakini hawatamwona; amejitenga nao. Wamemtendea BWANA kwa hila; maana wamezaa wana wageni; sasa mwezi huu uandamao utawaangamiza pamoja na mashamba yao. Pigeni tarumbeta katika Gibea, na baragumu katika Rama; pazeni sauti ya hofu katika Beth-aveni; nyuma yako, Ee Benyamini! Efraimu atakuwa ukiwa siku ya adhabu; katika makabila ya Israeli nimetangaza jambo litakalotukia kweli. Wakuu wa Yuda ni kama watu waondoao alama ya mpaka; nitawamwagia ghadhabu yangu kama maji. Efraimu ameonewa, amesetwa katika hukumu, kwa sababu alikuwa radhi kufuata ubatili. Kwa sababu hiyo mimi nimekuwa kama nondo kwa Efraimu, nimekuwa kama ubovu kwa nyumba ya Yuda. Efraimu alipouona ugonjwa wake, na Yuda jeraha lake, ndipo Efraimu alipokwenda kwa Ashuru, akatuma watu kwa mfalme Yarebu; lakini yeye hawezi kuwapoza, wala hatawaponya jeraha lenu. Maana mimi nitakuwa kama simba kwa Efraimu, na kama mwanasimba kwa nyumba ya Yuda; mimi, naam, mimi nitararua, kisha nitakwenda zangu; nitachukua mbali, wala hapatakuwa na mtu wa kuokoa. Nitakwenda zangu niparudie mahali pangu, hata watakapoungama makosa yao na kunitafuta uso wangu; katika taabu yao watanitafuta kwa bidii.