Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohana 5:1-15

Yohana 5:1-15 SRUV

Baada ya hayo palikuwa na sikukuu ya Wayahudi; naye Yesu akapanda kwenda Yerusalemu. Na huko Yerusalemu karibu na mlango wa kondoo pana bwawa la maji liitwalo kwa Kiebrania Bethzatha, nalo lilikuwa na matao matano. Ndani ya hayo jamii kubwa ya wagonjwa walikuwa wamelala, vipofu, viwete, nao waliopooza, [wakingoja maji yachemke. Kwa maana kuna wakati ambapo malaika hushuka, akaingia katika lile bwawa, akayatibua maji. Basi yeye aliyeingia wa kwanza baada ya maji kutibuliwa, akapona ugonjwa wote uliokuwa umempata.] Na hapa palikuwa na mtu, ambaye amekuwa mgonjwa muda wa miaka thelathini na minane. Yesu alipomwona huyu amelala, naye akijua ya kuwa amekuwa katika hali hiyo siku nyingi, alimwambia, Wataka kuwa mzima? Yule mgonjwa akamjibu, Bwana, mimi sina mtu wa kunitia katika bwawa, maji yanapotibuliwa; ila wakati ninapokuja mimi, mtu mwingine hushuka mbele yangu. Yesu akamwambia, Simama, jitwike godoro lako, uende. Mara yule mtu akawa mzima, akajitwika godoro lake, akaenda. Nayo ilikuwa ni sabato siku hiyo. Kwa sababu hiyo Wayahudi wakamwambia yule aliyeponywa, Leo ni sabato, wala si halali kwako kujitwika godoro. Akawajibu, Yeye aliyenifanya kuwa mzima ndiye aliyeniambia, Jitwike godoro lako, uende. Basi wakamwuliza, Yule aliyekuambia, Jitwike, uende, ni nani? Lakini yule mtu aliyeponywa hakumjua ni nani; maana Yesu alikuwa amejitenga, kwa sababu palikuwa na watu wengi mahali pale. Baada ya hayo Yesu akamkuta ndani ya hekalu, akamwambia, Angalia, umekuwa mzima; usitende dhambi tena, lisije likakupata jambo lililo baya zaidi. Yule mtu akaenda zake, akawapasha habari Wayahudi ya kwamba ni Yesu aliyemfanya kuwa mzima.

Soma Yohana 5

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Yohana 5:1-15