Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 21:1-19

Luka 21:1-19 SRUV

Akainua macho yake akawaona matajiri wakitia sadaka zao katika sanduku la hazina. Akamwona mjane mmoja maskini akitia mle senti mbili. Akasema, Hakika nawaambia, huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote; maana, hao wote walitoa sadaka katika mali iliyowazidi, bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo. Na watu kadhaa walipokuwa wakiongea habari za hekalu, jinsi lilivyopambwa kwa mawe mazuri na sadaka za watu, alisema, Haya mnayoyatazama, siku zitakuja ambapo halitasalia jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomolewa. Wakamwuliza wakisema, Mwalimu, mambo hayo yatakuwa lini? Nayo ni nini ishara ya kuwa mambo hayo yako karibu kutukia? Akasema, Angalieni, msije mkadanganyika, kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ndiye; tena, Majira yamekaribia. Basi msiwafuate hao. Nanyi mtakaposikia habari za vita na fitina, msitishwe; maana, hayo hayana budi kutukia kwanza, lakini ule mwisho hauji upesi. Kisha aliwaambia, Taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; kutakuwa na mitetemeko mikubwa ya ardhi; na njaa na tauni mahali pengi; na mambo ya kutisha na ishara kuu kutoka mbinguni. Lakini, kabla hayo yote hayajatokea, watawakamata na kuwaudhi; watawapeleka mbele ya masinagogi, na kuwaua magerezani, mkipelekwa mbele ya wafalme na watawala kwa ajili ya jina langu. Na hayo yatakuwa ushuhuda kwenu. Basi, kusudieni mioyoni mwenu, kutofikiri-fikiri kwanza mtakavyojibu; kwa sababu mimi nitawapa kinywa na hekima ambayo watesi wenu wote hawataweza kushindana nayo wala kuipinga. Nanyi mtasalitiwa na wazazi wenu, na ndugu zenu, na jamaa zenu, na rafiki zenu, nao watawaua baadhi yenu. Nanyi mtachukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu. Lakini hautapotea hata unywele mmoja wa vichwa vyenu. Nanyi kwa subira yenu mtaziponya nafsi zenu.

Soma Luka 21