Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 20:1-16

Mathayo 20:1-16 SRUV

Kwa maana ufalme wa mbinguni unafanana na mtu aliyetoka alfajiri kwenda kuwaajiri wafanya kazi awapeleke katika shamba lake la mizabibu. Naye alipokwisha kupatana na wafanya kazi kuwapa kutwa dinari, aliwapeleka katika shamba lake la mizabibu. Akatoka mnamo saa tatu, akaona wengine wamesimama sokoni wasiokuwa na kazi; na hao nao akawaambia, Nendeni nanyi pia katika shamba langu la mizabibu, na iliyo haki nitawapa. Wakaenda. Akatoka tena mnamo saa sita na saa tisa, akafanya vile vile. Hata kama saa kumi na moja akatoka, akakuta wengine wamesimama, akawaambia, Mbona mmesimama hapa mchana kutwa bila kazi? Wakamwambia, Kwa sababu hakuna mtu aliyetuajiri. Akawaambia, nanyi pia nendeni katika shamba la mizabibu. Kulipokuchwa, yule bwana wa shamba akamwambia msimamizi wake, Waite wafanya kazi, uwalipe ujira wao, ukianzia wa mwisho hadi wa kwanza. Na walipokuja wale wa saa kumi na moja, walipokea kila mtu dinari. Na wale wa kwanza walipokuja, walidhani kwamba watapokea zaidi; na hao pia wakapokea kila mtu dinari. Basi wakiisha kuipokea, wakamnung'unikia mwenye nyumba, wakisema, Hao wa mwisho wamefanya kazi saa moja tu, nawe umewasawazisha na sisi tuliostahimili taabu na joto la mchana kutwa. Naye akamjibu mmoja wao, akamwambia, Rafiki, sikudhulumu; hukupatana nami kwa dinari? Chukua iliyo yako, uende zako; napenda kumpa huyu wa mwisho sawa na wewe. Si halali yangu kutumia vilivyo vyangu kama nipendavyo? Au jicho lako limekuwa ovu kwa sababu ya mimi kuwa mwema? Vivyo hivyo wa mwisho watakuwa wa kwanza, na wa kwanza watakuwa wa mwisho.

Soma Mathayo 20