Mathayo 25:31-40
Mathayo 25:31-40 SRUV
Hapo atakapokuja Mwana wa Adamu katika utukufu wake, na malaika watakatifu wote pamoja naye, ndipo atakapoketi katika kiti cha utukufu wake; na mataifa yote yatakusanyika mbele zake; naye atawabagua kama vile mchungaji abaguavyo kondoo na mbuzi; atawaweka kondoo katika mkono wake wa kulia, na mbuzi mkono wake wa kushoto. Kisha Mfalme atawaambia wale walioko katika mkono wake wa kulia, Njooni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu; kwa maana nilikuwa na njaa, mkanipa chakula; nilikuwa na kiu, mkaninywesha; nilikuwa mgeni, mkanikaribisha; nilikuwa uchi, mkanivika nilikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama; nilikuwa kifungoni, mkanijia. Ndipo wenye haki watakapomjibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona ukiwa na njaa, tukakulisha, au ukiwa na kiu tukakunywesha? Tena ni lini tulipokuona ukiwa mgeni, tukakukaribisha, au ukiwa uchi, tukakuvika? Ni lini tena tulipokuona ukiwa mgonjwa, au ukiwa kifungoni, tukakujia? Na Mfalme atajibu, akiwaambia, Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.