Mathayo 6:19-34
Mathayo 6:19-34 SRUV
Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wezi huvunja na kuiba; bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wezi hawavunji wala hawaibi; kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako pia. Taa ya mwili ni jicho; basi jicho lako likiwa kamili, mwili wako wote utakuwa na nuru. Lakini jicho lako likiwa bovu, mwili wako wote utakuwa na giza. Basi ile nuru iliyomo ndani yako ikiwa giza; si giza hilo! Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali. Kwa sababu hiyo nawaambieni, Msisumbukie maisha yenu, mle nini au mnywe nini; wala miili yenu, mvae nini. Maisha je! Si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi? Waangalieni ndege wa angani, ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je! Si bora kuliko hao? Ni yupi kwenu ambaye akijisumbua aweza kujiongeza kimo chake hata mkono mmoja? Na mavazi, ya nini kuyasumbukia? Fikirini maua ya mashamba, jinsi yameavyo; hayafanyi kazi, wala hayasokoti nami nawaambia, ya kwamba hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo. Basi, ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya kondeni, yaliyopo leo, na kesho hutupwa katika tanuri, je! Hatazidi sana kuwavika ninyi, enyi wa imani haba? Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini? Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote. Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa. Basi msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Maovu ya siku yanaitosha siku hiyo.