Mathayo 6:19-34
Mathayo 6:19-34 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi huvunja na kuiba; bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi; kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako. Taa ya mwili ni jicho; basi jicho lako likiwa safi, mwili wako wote utakuwa na nuru. Lakini jicho lako likiwa bovu, mwili wako wote utakuwa na giza. Basi ile nuru iliyomo ndani yako ikiwa giza; si giza hilo! Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali. Kwa sababu hiyo nawaambieni, Msisumbukie maisha yenu, mle nini au mnywe nini; wala miili yenu, mvae nini. Maisha je! Si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi? Waangalieni ndege wa angani, ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je! Si bora kupita hao? Ni yupi kwenu ambaye akijisumbua aweza kujiongeza kimo chake hata mkono mmoja? Na mavazi, ya nini kuyasumbukia? Fikirini maua ya mashamba, jinsi yameavyo; hayafanyi kazi, wala hayasokoti nami nawaambia, ya kwamba hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo. Basi, ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya kondeni, yaliyopo leo, na kesho hutupwa kalibuni, je! Hatazidi sana kuwavika ninyi, enyi wa imani haba? Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini? Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote. Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa. Basi msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake.
Mathayo 6:19-34 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Msijiwekee hazina duniani, mahali ambapo nondo na kutu huharibu, nao wevi huvunja na kuiba. Lakini jiwekeeni hazina mbinguni, mahali ambapo nondo na kutu haviharibu, wala wevi hawavunji na kuiba. Kwa sababu mahali hazina yako ilipo, hapo ndipo pia moyo wako utakapokuwa. “Jicho ni taa ya mwili. Kama jicho lako ni nyofu, mwili wako wote utajaa nuru. Lakini kama jicho lako ni ovu, mwili wako wote utajawa na giza. Kwa hiyo basi, kama nuru iliyomo ndani yako ni giza, hilo ni giza kuu namna gani! “Hakuna mtu awezaye kuwatumikia mabwana wawili. Kwa kuwa atamchukia huyu na kumpenda yule mwingine, au atashikamana sana na huyu na kumdharau yule mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu pamoja na Mali. “Kwa hiyo nawaambia, msisumbukie maisha yenu kwamba mtakula nini au mtakunywa nini; au msumbukie miili yenu kwamba mtavaa nini. Je, maisha si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi? Waangalieni ndege wa angani; wao hawapandi wala hawavuni au kuweka ghalani, lakini Baba yenu wa mbinguni huwalisha. Je, ninyi si wa thamani zaidi kuliko hao ndege? Ni nani miongoni mwenu ambaye kwa kujitaabisha kwake anaweza kujiongezea hata saa moja zaidi katika maisha yake? “Nanyi kwa nini mnajitaabisha kwa ajili ya mavazi? Fikirini maua ya shambani yameavyo. Hayafanyi kazi wala hayafumi. Lakini nawaambia, hata Solomoni katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo ya hayo maua. Basi ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya shambani, ambayo leo yapo na kesho yanatupwa motoni, je, hatawavika ninyi vizuri zaidi, enyi wa imani haba? Kwa hiyo msiwe na wasiwasi, mkisema, ‘Tutakula nini?’ au ‘Tutakunywa nini?’ au ‘Tutavaa nini?’ Watu wasiomjua Mungu ndio wanaoshindania hayo, lakini Baba yenu wa mbinguni anafahamu kuwa mnahitaji haya yote. Lakini utafuteni kwanza Ufalme wa Mungu na haki yake, na haya yote atawapa pia. Kwa hiyo msiwe na wasiwasi kuhusu kesho, kwa sababu kesho itajitaabikia yenyewe. Yatosha kwa siku masumbufu yake.
Mathayo 6:19-34 Biblia Habari Njema (BHN)
“Msijiwekee hazina hapa duniani ambako nondo na kutu huharibu, na wezi huingia na kuiba. Jiwekeeni hazina mbinguni ambako nondo na kutu hawawezi kuiharibu, wala wezi hawaingii wakaiba. Maana pale ilipo hazina yako, ndipo pia utakapokuwa moyo wako. “Jicho ni taa ya mwili. Kama basi jicho lako ni zima, mwili wako wote utakuwa katika mwanga. Lakini ikiwa jicho lako ni bovu, mwili wako wote utakuwa katika giza. Basi, ikiwa mwanga uliomo ndani yako ni giza, basi, hilo ni giza la kutisha mno! “Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili. Maana atamchukia mmoja na kumpenda huyo wa pili; au ataambatana na mmoja na kumdharau huyo mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali pamoja. “Ndiyo maana nawaambieni, msiwe na wasiwasi juu ya chakula na kinywaji mnavyohitaji ili kuishi, wala juu ya mavazi mnayohitaji kwa ajili ya miili yenu. Je, maisha ni chakula tu au zaidi? Na mwili, je, si zaidi ya mavazi? Waangalieni ndege wa mwituni: Hawapandi, hawavuni, wala hawana ghala yoyote. Hata hivyo, Baba yenu wa mbinguni huwalisha. Je, nyinyi si wa thamani kuliko hao? Ni nani miongoni mwenu kwa kuwa na wasiwasi sana anaweza kuuongeza muda wa maisha yake? “Na kuhusu mavazi, ya nini kuwa na wasiwasi? Tazameni maua ya porini jinsi yanavyostawi. Hayafanyi kazi wala hayasokoti. Lakini nawaambieni, hata Solomoni mwenyewe na fahari zake zote hakupata kuvikwa vizuri kama ua mojawapo. Ikiwa basi, Mungu hulivika hivyo jani la shambani ambalo leo liko na kesho latupwa motoni, je, si atawafanyia nyinyi zaidi? Enyi watu wenye imani haba! “Basi, msiwe na wasiwasi: ‘Tutakula nini, tutakunywa nini, tutavaa nini!’ Maana hayo yote yanahangaikiwa na watu wasiomjua Mungu. Baba yenu wa mbinguni anajua kwamba mnahitaji vitu hivyo vyote. Bali, shughulikeni kwanza juu ya ufalme wa Mungu na matakwa yake, na hayo yote mtapewa kwa ziada. Basi, msiwe na wasiwasi juu ya kesho; kesho inayo yake. Matatizo ya siku moja yanawatosheni kwa siku hiyo.
Mathayo 6:19-34 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wezi huvunja na kuiba; bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wezi hawavunji wala hawaibi; kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako pia. Taa ya mwili ni jicho; basi jicho lako likiwa kamili, mwili wako wote utakuwa na nuru. Lakini jicho lako likiwa bovu, mwili wako wote utakuwa na giza. Basi ile nuru iliyomo ndani yako ikiwa giza; si giza hilo! Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali. Kwa sababu hiyo nawaambieni, Msisumbukie maisha yenu, mle nini au mnywe nini; wala miili yenu, mvae nini. Maisha je! Si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi? Waangalieni ndege wa angani, ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je! Si bora kuliko hao? Ni yupi kwenu ambaye akijisumbua aweza kujiongeza kimo chake hata mkono mmoja? Na mavazi, ya nini kuyasumbukia? Fikirini maua ya mashamba, jinsi yameavyo; hayafanyi kazi, wala hayasokoti nami nawaambia, ya kwamba hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo. Basi, ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya kondeni, yaliyopo leo, na kesho hutupwa katika tanuri, je! Hatazidi sana kuwavika ninyi, enyi wa imani haba? Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini? Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote. Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa. Basi msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Maovu ya siku yanaitosha siku hiyo.