Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Marko 4:1-20

Marko 4:1-20 SRUV

Akaanza kufundisha tena kando ya ziwa. Kundi kubwa sana la watu wakamkusanyikia, hata yeye akapanda katika mashua, akakaa ziwani, watu wote walikuwa katika nchi kavu kando ya ziwa. Akawafundisha mambo mengi kwa mifano, akawaambia katika mafundisho yake, Sikilizeni; Tazama, mpanzi alitoka kwenda kupanda; ikawa alipokuwa akipanda, mbegu nyingine ilianguka kando ya njia, wakaja ndege wakaila. Nyingine ikaanguka penye mwamba, pasipokuwa na udongo mwingi; mara ikaota kwa kuwa na udongo haba; hata jua lilipozuka iliungua, na kwa kuwa haina mizizi ikanyauka. Nyingine ikaanguka penye miiba; ile miiba ikamea ikaisonga, isizae matunda. Nyingine zikaanguka penye udongo ulio mzuri, zikazaa matunda, zikimea na kukua, na kuzaa, moja thelathini, moja sitini, na moja mia. Akasema, Aliye na masikio ya kusikilia, na asikie. Naye alipokuwa peke yake, wale watu waliomzunguka, na wale Kumi na Wawili, walimwuliza kuhusu ile mifano. Akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuijua siri ya ufalme wa Mungu, bali kwa wale walio nje, yote hufanywa kwa mifano, ili wakitazama watazame, wasione; Na wakisikia wasikie, wasielewe; Wasije wakaongoka, na kusamehewa. Akawaambia, Hamjui mfano huu? Basi mifano yote mtaitambuaje? Mpanzi huyo hulipanda neno. Hawa ndio walio kando ya njia lipandwapo neno; nao, wakiisha kusikia, mara huja Shetani, akaliondoa lile neno lililopandwa mioyoni mwao. Kadhalika na hawa ndio wapandwao penye miamba, ambao kwamba wakiisha kulisikia lile neno, mara hulipokea kwa furaha; ila hawana mizizi ndani yao, bali hudumu muda mchache; kisha ikitokea dhiki au udhia kwa ajili ya lile neno, mara hujikwaa. Na hawa ndio wale wapandwao penye miiba; ni watu walisikiao lile neno, na shughuli za dunia, na udanganyifu wa mali, na tamaa za mambo mengine zikiingia, hulisonga lile neno, likawa halizai. Na hawa ndio waliopandwa penye udongo ulio mzuri; ni watu walisikiao lile neno na kulipokea, na kuzaa matunda, mmoja thelathini, mmoja sitini, na mmoja mia.

Soma Marko 4