Wafilipi 2:19-30
Wafilipi 2:19-30 SRUV
Lakini natumaini katika Bwana Yesu kumtuma Timotheo afike kwenu karibu, nifarijiwe na mimi, nikiijua hali yenu. Maana sina mtu mwingine mwenye nia moja nami, atakayeiangalia hali yenu kweli kweli. Maana wote wanatafuta vyao wenyewe, sivyo vya Kristo Yesu. Ila mwajua sifa yake, ya kuwa ametumika pamoja nami kwa ajili ya Injili, kama mwana na baba yake. Basi, natumaini kumtuma huyo mara, hapo nitakapojua yatakayonipata. Nami naamini katika Bwana ya kuwa nitakuja na mimi mwenyewe hivi karibuni. Lakini niliona imenilazimu kumtuma kwenu Epafrodito, ndugu yangu, mfanyakazi pamoja nami, askari pamoja nami; tena ni mtume wenu na mhudumu wa mahitaji yangu. Kwa kuwa alikuwa na shauku kwenu ninyi nyote, akahuzunika sana, kwa sababu mlisikia ya kwamba alikuwa mgonjwa. Kwa maana alikuwa mgonjwa sana, karibu kufa; lakini Mungu alimhurumia; wala si yeye peke yake, ila na mimi pia; nisiwe na huzuni juu ya huzuni. Kwa hiyo nimefanya bidii nyingi zaidi kumtuma, ili mtakapomwona tena mpate kufurahi, nami nipunguziwe huzuni yangu. Mpokeeni, basi, katika Bwana, kwa furaha yote, mkawahesabu watu kama huyu kuwa watu wa kuheshimiwa. Maana kwa ajili ya kazi ya Kristo alikaribia kufa akahatarisha roho yake ili kusudi aitimize huduma ambayo msingeweza kunitimizia.