Wafilipi 2:19-30
Wafilipi 2:19-30 Biblia Habari Njema (BHN)
Katika kuungana na Bwana Yesu ninalo tumaini kwamba nitaweza kumtuma Timotheo kwenu hivi karibuni, ili nitiwe moyo kwa kupata habari zenu. Sina mtu mwingine kama yeye ambaye anawashughulikieni kwa moyo. Wengine wanashughulikia tu mambo yao wenyewe badala ya kuyashughulikia mambo ya Yesu Kristo. Nyinyi wenyewe mwafahamu jinsi Timotheo alivyo thabiti; yeye na mimi, kama vile mtoto na baba yake, tumefanya kazi pamoja kwa ajili ya Injili. Kwa hiyo natumaini kumtuma kwenu mara nitakapojua jinsi mambo yatakavyoniendea. Na, ninatumaini katika Bwana kwamba nami pia nitaweza kuja kwenu karibuni. Nimeona sina budi kumtuma kwenu ndugu yetu Epafrodito, ambaye ni mwenzangu kazini na vitani na ambaye ni mjumbe wenu aliyenisaidia katika mahitaji yangu. Anayo hamu kubwa ya kuwaoneni nyinyi nyote, na amesikitika sana kwani nyinyi mmepata habari kwamba alikuwa mgonjwa. Naam, alikuwa mgonjwa hata karibu ya kufa. Lakini Mungu alimwonea huruma, na si yeye peke yake, ila na mimi pia ili nisipate uchungu zaidi. Basi, nataka sana kumtuma kwenu, ili mtakapomwona mpate kufurahi tena, nayo huzuni yangu itoweke. Mpokeeni, basi, kwa furaha yote kama ndugu katika Bwana. Mnapaswa kuwastahi watu walio kama yeye, kwani yeye alikuwa hata karibu ya kufa kwa ajili ya kazi ya Kristo, na kuhatarisha maisha yake ili aweze kunipa mimi msaada ule ambao hamkuweza kuuleta nyinyi wenyewe.
Wafilipi 2:19-30 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini natumaini katika Bwana Yesu kumtuma Timotheo afike kwenu karibu, nifarijiwe na mimi, nikiijua hali yenu. Maana sina mtu mwingine mwenye nia moja nami, atakayeiangalia hali yenu kweli kweli. Maana wote wanatafuta vyao wenyewe, sivyo vya Kristo Yesu. Ila mwajua sifa yake, ya kuwa ametumika pamoja nami kwa ajili ya Injili, kama mwana na baba yake. Basi, natumaini kumtuma huyo mara, hapo nitakapojua yatakayonipata. Nami naamini katika Bwana ya kuwa nitakuja na mimi mwenyewe hivi karibuni. Lakini niliona imenilazimu kumtuma kwenu Epafrodito, ndugu yangu, mfanyakazi pamoja nami, askari pamoja nami; tena ni mtume wenu na mhudumu wa mahitaji yangu. Kwa kuwa alikuwa na shauku kwenu ninyi nyote, akahuzunika sana, kwa sababu mlisikia ya kwamba alikuwa mgonjwa. Kwa maana alikuwa mgonjwa sana, karibu kufa; lakini Mungu alimhurumia; wala si yeye peke yake, ila na mimi pia; nisiwe na huzuni juu ya huzuni. Kwa hiyo nimefanya bidii nyingi zaidi kumtuma, ili mtakapomwona tena mpate kufurahi, nami nipunguziwe huzuni yangu. Mpokeeni, basi, katika Bwana, kwa furaha yote, mkawahesabu watu kama huyu kuwa watu wa kuheshimiwa. Maana kwa ajili ya kazi ya Kristo alikaribia kufa akahatarisha roho yake ili kusudi aitimize huduma ambayo msingeweza kunitimizia.
Wafilipi 2:19-30 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Walakini natumaini katika Bwana Yesu kumtuma Timotheo afike kwenu karibu, nifarijiwe na mimi, nikiijua hali yenu. Maana sina mtu mwingine mwenye nia moja nami, atakayeiangalia hali yenu kweli kweli. Maana wote wanatafuta vyao wenyewe, sivyo vya Kristo Yesu. Ila mwajua sifa yake, ya kuwa ametumika pamoja nami kwa ajili ya Injili, kama mwana na baba yake. Basi, natumaini kumtuma huyo mara, hapo nitakapojua yatakayonipata. Nami naamini katika Bwana ya kuwa nitakuja na mimi mwenyewe hivi karibu. Lakini naliona imenilazimu kumtuma kwenu Epafrodito, ndugu yangu, mtenda kazi pamoja nami, askari pamoja nami; tena ni mtume wenu na mhudumu wa mahitaji yangu. Kwa kuwa alikuwa na shauku kwenu ninyi nyote, akahuzunika sana, kwa sababu mlisikia ya kwamba alikuwa hawezi. Kwa maana alikuwa hawezi kweli kweli, karibu na kufa; lakini Mungu alimhurumia; wala si yeye peke yake, ila na mimi pia; nisiwe na huzuni juu ya huzuni. Kwa hiyo nimefanya bidii nyingi zaidi kumtuma, ili mtakapomwona tena mpate kufurahi, nami nipunguziwe huzuni yangu. Mpokeeni, basi, katika Bwana, kwa furaha yote, mkawahesabu watu kama huyu kuwa watu wa kuheshimiwa. Maana kwa ajili ya kazi ya Kristo alikaribia kufa akaponza roho yake; ili kusudi ayatimize yaliyopungua katika huduma yenu kwangu.
Wafilipi 2:19-30 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Natumaini katika Bwana Yesu kumtuma Timotheo hivi karibuni aje kwenu, ili nipate kufarijika moyo nitakapopata habari zenu. Sina mtu mwingine kama yeye, ambaye ataangalia hali yenu kwa halisi. Kwa maana kila mmoja anajishughulisha zaidi na mambo yake mwenyewe wala si yale ya Yesu Kristo. Lakini ninyi wenyewe mnajua jinsi Timotheo alivyojithibitisha mwenyewe, kwa maana ametumika pamoja nami kwa kazi ya Injili, kama vile mwana kwa baba yake. Kwa hiyo, ninatumaini kumtuma kwenu upesi mara nitakapojua mambo yangu yatakavyokuwa. Nami mwenyewe ninatumaini katika Bwana kwamba nitakuja kwenu hivi karibuni. Lakini nadhani ni muhimu kumtuma tena kwenu Epafrodito, ndugu yangu na mtendakazi pamoja nami, aliye askari mwenzangu, ambaye pia ni mjumbe wenu mliyemtuma ili ashughulike na mahitaji yangu. Kwa maana amekuwa akiwaonea sana shauku ninyi nyote, akiwa na wasiwasi kwa kuwa mlisikia kwamba alikuwa mgonjwa. Kweli alikuwa mgonjwa, tena karibu ya kufa. Lakini Mungu alimhurumia, wala si yeye tu, bali hata na mimi alinihurumia, nisipatwe na huzuni juu ya huzuni. Kwa hiyo mimi ninafanya bidii kumtuma kwenu ili mtakapomwona kwa mara nyingine, mpate kufurahi, nami wasiwasi wangu upungue. Kwa hiyo mpokeeni katika Bwana kwa furaha kubwa, nanyi wapeni heshima watu kama hawa, kwa sababu alikaribia kufa kwa ajili ya kazi ya Kristo, akihatarisha maisha yake ili aweze kunihudumia vile ninyi hamkuweza.