Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mithali 4:1-27

Mithali 4:1-27 SRUV

Wanangu, yasikilizeni mausia ya baba yenu, Tegeni masikio mpate kujua ufahamu. Kwa kuwa nawapa mafundisho mazuri; Msiiache sheria yangu. Maana nilikuwa mwana kwa baba yangu, Mpole, mpenzi wa pekee wa mama yangu. Naye akanifundisha, akaniambia, Moyo wako uyahifadhi maneno yangu; Shika amri zangu ukaishi. Jipatie hekima, jipatie ufahamu; usiusahau; Wala usiyakatae maneno ya kinywa changu. Usimwache, naye atakusitiri; Umpende, naye atakulinda. Bora hekima, basi jipatie hekima; Naam, kwa mapato yako yote jipatie ufahamu. Umtukuze, naye atakukuza; Atakupatia heshima, ukimkumbatia. Atakupa neema kuwa kilemba kichwani; Na kukukirimia taji la uzuri. Mwanangu, sikiliza, na kuzipokea kauli zangu; Na miaka ya maisha yako itakuwa mingi. Nimekufundisha katika njia ya hekima; Nimekuongoza katika mapito ya unyofu. Uendapo, hatua zako hazitadhiikika, Wala ukipiga mbio hutajikwaa. Mkamate sana elimu, usimwache aende zake; Mshike, maana yeye ni uzima wako. Usiingie katika njia ya waovu, Wala usitembee katika njia ya wabaya. Jiepushe nayo, usipite karibu nayo, Igeukie mbali, ukaende zako. Maana hawalali isipokuwa wametenda madhara; Huondolewa usingizi, ikiwa hawakumwangusha mtu. Maana wao hula mkate wa uovu, Nao hunywa divai ya ujeuri. Bali njia ya wenye haki ni kama nuru ing'aayo, Ikizidi kung'aa hata mchana mkamilifu. Njia ya waovu ni kama giza; Hawajui ni kitu gani kiwakwazacho. Mwanangu, sikiliza maneno yangu; Tega sikio lako, uzisikie kauli zangu. Zisiondoke machoni pako; Uzihifadhi ndani ya moyo wako. Maana ni uhai kwa wale wazipatao, Na afya ya mwili wao wote. Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima. Jiepushe na kinywa cha ujeuri, Na midomo ya upotovu uiweke mbali nawe. Macho yako yatazame mbele, Na kope zako zitazame mbele yako sawasawa. Ulisawazishe pito la mguu wako, Na njia zako zote zithibitike; Usigeuke kwa kulia wala kwa kushoto; Ondoa mguu wako maovuni.

Soma Mithali 4