Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Methali 4:1-27

Methali 4:1-27 Biblia Habari Njema (BHN)

Wanangu, sikilizeni mwongozo wa baba yenu, tegeni sikio mpate kuwa na akili. Maana ninawapa maagizo mema, msiyakatae mafundisho yangu. Mimi pia nilikuwa mtoto mwenye baba, nilikuwa mpole, kipenzi cha mama yangu. Baba yangu alinifundisha hiki: “Zingatia kwa moyo maneno yangu, shika amri zangu nawe utaishi. Jipatie hekima, jipatie ufahamu; usisahau wala kupuuza maneno yangu. Usimwache Hekima, naye atakutunza; umpende, naye atakulinda. Jambo la msingi ni kujipatia hekima; toa vyote ulivyonavyo ujipatie akili. Mthamini sana Hekima, naye atakutukuza; ukimshikilia atakupa heshima. Atakuvika kilemba kizuri kichwani pako, atakupa taji maridadi.” Mwanangu, sikia na kuyapokea maneno yangu, ili upate kuwa na miaka mingi ya kuishi. Nimekufundisha njia ya hekima, nimekuongoza katika njia nyofu. Ukitembea hatua zako hazitazuiwa, wala ukikimbia hutajikwaa. Zingatia mafundisho ya Hekima na usimwache aponyoke, mshike kwa makini maana yeye ni uhai wako. Usijiingize katika njia ya waovu, wala usifuate mwenendo wa watu wabaya. Iepe njia hiyo wala usiikaribie; jiepushe nayo, uende zako. Waovu kamwe hawalali wasipotenda uovu; hawapati usingizi wasipomkwaza mtu. Maana uovu ndicho chakula chao, ukatili ndiyo divai yao. Njia ya watu wema ni kama nuru ya alfajiri, ambayo hungaa zaidi na zaidi hata mchana kamili. Lakini njia ya waovu ni kama giza nene, hawajui kinachowafanya wajikwae. Mwanangu, sikiliza kwa makini maneno yangu, itegee sikio misemo yangu. Usiyaache yatoweke machoni pako, yahifadhi ndani ya moyo wako. Maana hayo ni uhai kwa mtu anayeyapata, ni dawa kwa mwili wake wote. Linda moyo wako kwa uangalifu wote, maana humo zatoka chemchemi za uhai. Tenga mbali nawe lugha potovu; wala midomo yako isitamke maneno madanganyifu. Uyaelekeze macho yako mbele kwa ujasiri, mtazamo wako uwe mbele moja kwa moja. Fikiria njia utakayochukua, na hatua zako zote zitakuwa kamili. Usigeukie kulia wala kushoto; epusha mguu wako mbali na uovu.

Shirikisha
Soma Methali 4

Methali 4:1-27 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Wanangu, yasikilizeni mausia ya baba yenu, Tegeni masikio mpate kujua ufahamu. Kwa kuwa nawapa mafundisho mazuri; Msiiache sheria yangu. Maana nilikuwa mwana kwa baba yangu, Mpole, mpenzi wa pekee wa mama yangu. Naye akanifundisha, akaniambia, Moyo wako uyahifadhi maneno yangu; Shika amri zangu ukaishi. Jipatie hekima, jipatie ufahamu; usiusahau; Wala usiyakatae maneno ya kinywa changu. Usimwache, naye atakusitiri; Umpende, naye atakulinda. Bora hekima, basi jipatie hekima; Naam, kwa mapato yako yote jipatie ufahamu. Umtukuze, naye atakukuza; Atakupatia heshima, ukimkumbatia. Atakupa neema kuwa kilemba kichwani; Na kukukirimia taji la uzuri. Mwanangu, sikiliza, na kuzipokea kauli zangu; Na miaka ya maisha yako itakuwa mingi. Nimekufundisha katika njia ya hekima; Nimekuongoza katika mapito ya unyofu. Uendapo, hatua zako hazitadhiikika, Wala ukipiga mbio hutajikwaa. Mkamate sana elimu, usimwache aende zake; Mshike, maana yeye ni uzima wako. Usiingie katika njia ya waovu, Wala usitembee katika njia ya wabaya. Jiepushe nayo, usipite karibu nayo, Igeukie mbali, ukaende zako. Maana hawalali isipokuwa wametenda madhara; Huondolewa usingizi, ikiwa hawakumwangusha mtu. Maana wao hula mkate wa uovu, Nao hunywa divai ya ujeuri. Bali njia ya wenye haki ni kama nuru ing'aayo, Ikizidi kung'aa hata mchana mkamilifu. Njia ya waovu ni kama giza; Hawajui ni kitu gani kiwakwazacho. Mwanangu, sikiliza maneno yangu; Tega sikio lako, uzisikie kauli zangu. Zisiondoke machoni pako; Uzihifadhi ndani ya moyo wako. Maana ni uhai kwa wale wazipatao, Na afya ya mwili wao wote. Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima. Jiepushe na kinywa cha ujeuri, Na midomo ya upotovu uiweke mbali nawe. Macho yako yatazame mbele, Na kope zako zitazame mbele yako sawasawa. Ulisawazishe pito la mguu wako, Na njia zako zote zithibitike; Usigeuke kwa kulia wala kwa kushoto; Ondoa mguu wako maovuni.

Shirikisha
Soma Methali 4

Methali 4:1-27 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Wanangu, yasikilizeni mausia ya baba yenu, Tegeni masikio mpate kujua ufahamu. Kwa kuwa nawapa mafundisho mazuri; Msiiache sheria yangu. Maana nalikuwa mwana kwa baba yangu, Mpole, mpenzi wa pekee wa mama yangu. Naye akanifundisha, akaniambia, Moyo wako uyahifadhi maneno yangu; Shika amri zangu ukaishi. Jipatie hekima, jipatie ufahamu; usiusahau; Wala usiyakatae maneno ya kinywa changu. Usimwache, naye atakuhifadhi; Umpende, naye atakulinda. Bora hekima, basi jipatie hekima; Naam, kwa mapato yako yote jipatie ufahamu. Umtukuze, naye atakukuza; Atakupatia heshima, ukimkumbatia. Atakupa neema kuwa kilemba kichwani; Na kukukirimia taji ya uzuri. Mwanangu, sikiliza, na kuzipokea kauli zangu; Na miaka ya maisha yako itakuwa mingi. Nimekufundisha katika njia ya hekima; Nimekuongoza katika mapito ya unyofu. Uendapo, hatua zako hazitadhiikika, Wala ukipiga mbio hutajikwaa. Mkamate sana elimu, usimwache aende zake; Mshike, maana yeye ni uzima wako. Usiingie katika njia ya waovu, Wala usitembee katika njia ya wabaya. Jiepushe nayo, usipite karibu nayo, Igeukie mbali, ukaende zako. Maana hawalali isipokuwa wametenda madhara; Huondolewa usingizi, ikiwa hawakumwangusha mtu. Maana wao hula mkate wa uovu, Nao hunywa divai ya jeuri. Bali njia ya wenye haki ni kama nuru ing’aayo, Ikizidi kung’aa hata mchana mkamilifu. Njia ya waovu ni kama giza; Hawajui ni kitu gani kiwakwazacho. Mwanangu, sikiliza maneno yangu; Tega sikio lako, uzisikie kauli zangu. Zisiondoke machoni pako; Uzihifadhi ndani ya moyo wako. Maana ni uhai kwa wale wazipatao, Na afya ya mwili wao wote. Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima. Kinywa cha ukaidi ukitenge nawe, Na midomo ya upotovu uiweke mbali nawe. Macho yako yatazame mbele, Na kope zako zitazame mbele yako sawasawa. Ulisawazishe pito la mguu wako, Na njia zako zote zithibitike; Usigeuke kwa kuume wala kwa kushoto; Ondoa mguu wako maovuni.

Shirikisha
Soma Methali 4

Methali 4:1-27 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Sikilizeni wanangu, mafundisho ya baba yenu; sikilizeni kwa makini na mpate ufahamu. Ninawapa mafundisho ya maana, kwa hiyo msiyaache mafundisho yangu. Nilipokuwa mvulana mdogo katika nyumba ya baba yangu, ningali mchanga na mtoto pekee kwa mama yangu, baba alinifundisha akisema, “Yashike maneno yangu yote kwa moyo wako wote; yashike maagizo yangu na wewe utaishi. Pata hekima, pata ufahamu; usiyasahau maneno yangu wala usiyaache. Usimwache hekima naye atakuweka salama; mpende, naye atakulinda. Hekima ni bora kuliko vitu vyote; kwa hiyo jipe hekima. Hata ikikugharimu vyote ulivyo navyo, pata ufahamu. Mstahi, naye atakukweza; mkumbatie, naye atakuheshimu. Atakuvika shada la neema kichwani mwako na kukupa taji ya utukufu.” Sikiliza mwanangu, kubali ninachokuambia, nayo miaka ya maisha yako itakuwa mingi. Ninakuongoza katika njia ya hekima na kukuongoza katika mapito yaliyonyooka. Utembeapo, hatua zako hazitazuiliwa; ukimbiapo, hutajikwaa. Mkamate sana elimu, usimwache aende zake; mshike, maana yeye ni uzima wako. Usiuweke mguu wako katika njia ya waovu wala usitembee katika njia ya watu wabaya. Epukana nayo, usisafiri katika njia hiyo; achana nayo, na uelekee njia yako. Kwa kuwa hawawezi kulala mpaka watende uovu; wanashindwa hata kusinzia mpaka wamwangushe mtu. Wanakula mkate wa uovu, na kunywa mvinyo wa jeuri. Njia ya wenye haki ni kama nuru ya kwanza ya mapambazuko, ambayo hungʼaa zaidi na zaidi mpaka mchana mkamilifu. Lakini njia ya waovu ni kama giza nene; hawajui kinachowafanya wajikwae. Mwanangu, yasikilize kwa makini yale ninayokuambia; sikiliza kwa makini maneno yangu. Usiruhusu yaondoke machoni pako, yahifadhi ndani ya moyo wako; kwa sababu ni uzima kwa wale wanaoyapata na afya kwa mwili wote wa mwanadamu. Zaidi ya yote, linda moyo wako, kuliko yote uyalindayo, maana ndiko zitokako chemchemi za uzima. Epusha kinywa chako na ukaidi; weka mazungumzo machafu mbali na midomo yako. Macho yako na yatazame mbele, kaza macho yako moja kwa moja mbele yako. Sawazisha mapito ya miguu yako na njia zako zote ziwe zimethibitika. Usigeuke kulia wala kushoto; epusha mguu wako na ubaya.

Shirikisha
Soma Methali 4