Zaburi 17:1-15
Zaburi 17:1-15 SRUV
Ee BWANA, usikie haki, ukisikilize kilio changu, Utege sikio lako kwa maombi yangu, Yasiyotoka katika midomo ya hila. Hukumu yangu na itoke kwako, Macho yako na yatazame mambo ya adili. Umenijaribu moyo wangu, umenijia usiku, Umenichunguza usione neno; Nimenuia kinywa changu kisikose, Kuhusu matendo ya wanadamu; Kwa neno la midomo yako Nimejiepusha na njia za wenye jeuri. Nyayo zangu zimeshikamana na njia zako, Hatua zangu hazikuondoshwa. Ee Mungu, nimekuita kwa maana utaitika, Utege sikio lako ulisikie neno langu. Dhihirisha fadhili zako za ajabu Wewe uwaokoaye wanaokukimbilia; Kwa mkono wako wa kulia Uwaokoe kutoka kwa adui zao. Unilinde kama mboni ya jicho, Unifiche chini ya kivuli cha mbawa zako; Wasinione wasio haki wanaonionea, Adui za roho yangu wanaonizunguka. Wamejawa na ukaidi, Kwa vinywa vyao wanajigamba. Wamenifuatia; na sasa wananizunguka, Na kuyakaza macho yao watuangushe chini. Kama mfano wa simba atakaye kurarua, Kama mwanasimba aoteaye katika maotea yake. Inuka, Ee BWANA, umkabili, umwangushe, Kwa upanga wako uniokoe nafsi yangu na mtu mbaya. Ee BWANA, kwa mkono wako uniokoe na watu, Watu wa dunia hii ambao fungu lao liko katika maisha haya. Matumbo yao wayajaza kwa hazina yako, Hushiba wana, huwaachia watoto wao akiba zao, Bali mimi nikutazame uso wako katika haki, Niamkapo nishibishwe kwa sura yako.