Ufunuo 6:9-17
Ufunuo 6:9-17 SRUV
Na alipoufungua mhuri wa tano, nikaona chini ya madhabahu roho zao waliochinjwa kwa ajili ya neno la Mungu, na kwa ajili ya ushuhuda waliokuwa nao. Wakalia kwa sauti kuu, wakisema, Ee Mola, Mtakatifu, na Mkweli, utakawia hadi lini kuhukumu na kuilipa damu yetu kwa hao wakaao juu ya nchi? Nao wakapewa kila mmoja nguo ndefu, nyeupe, wakaambiwa wasubiri bado muda mchache, hadi itakapotimia idadi ya watumishi wenzao na ndugu zao, watakaouawa kama wao walivyouawa. Nami nikaona, alipoufungua mhuri wa sita, palikuwa na tetemeko kuu la nchi; jua likawa jeusi kama gunia la singa, mwezi wote ukawa kama damu, na nyota zikaanguka juu ya nchi kama vile mtini upukutishavyo mapooza yake, utikiswapo na upepo mwingi. Mbingu zikaondolewa kama ukurasa ulivyokunjwa, na kila mlima na kisiwa kikahamishwa kutoka mahali pake. Na wafalme wa dunia, na wakuu, na majemadari, na matajiri, na wenye nguvu, na kila mtumwa, na muungwana, wakajificha katika pango na chini ya miamba ya milima, wakiiambia milima na miamba, Tuangukieni, tusitirini, mbele za uso wake yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na kwenye hasira ya Mwana-kondoo. Kwa maana siku iliyo kuu, ya hasira yao, imekuja; naye ni nani awezaye kuistahimili?