Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zekaria 4:1-14

Zekaria 4:1-14 SRUV

Na yule malaika aliyesema nami akanijia mara ya pili, akaniamsha, kama mtu aamshwavyo katika usingizi wake. Akaniuliza, Unaona nini? Nikasema, Nimeona, na tazama, kinara cha taa cha dhahabu tupu, nacho kina bakuli juu yake, na taa zake saba juu yake; tena iko mirija saba ya kuleta mafuta, kwa taa zote zilizo juu yake; na mizeituni miwili karibu yake, mmoja upande wa kulia wa lile bakuli, na mmoja upande wake wa kushoto. Nami nikajibu, nikamwambia yule malaika aliyesema nami, nikasema, Ee Bwana wangu, vitu hivi ni nini? Ndipo malaika aliyesema nami akajibu, akaniambia, Hujui vitu hivi ni nini? Nikasema, La, Bwana wangu. Akajibu akaniambia, akisema, Hili ndilo neno la BWANA kwa Zerubabeli, kusema, Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa roho yangu, asema BWANA wa majeshi. Nani wewe, Ee mlima mkubwa? Mbele ya Zerubabeli utakuwa nchi tambarare; naye atalileta lile jiwe la kuwekwa juu kabisa pamoja na vigelegele vya, Neema, neema, ilikalie. Tena neno la BWANA likanijia, kusema, Mikono yake Zerubabeli imeiweka misingi ya nyumba hii, na mikono yake ndiyo itakayoimaliza; nawe utajua ya kuwa BWANA wa majeshi amenituma kwenu. Maana yeyote aliyeidharau siku ya mambo madogo watafurahi, naye ataiona timazi ikiwa katika mkono wa Zerubabeli; naam, hizi taa saba ndizo macho ya BWANA; yanaona huku na huko duniani kote. Ndipo nikajibu, nikamwambia, Ni nini mizeituni hii miwili iliyo upande wa kulia wa kinara cha taa kile na upande wake wa kushoto? Na kwa mara ya pili, nikamwuliza, Ni nini haya matawi mawili ya mizeituni, ambayo kwa njia ya ile mifereji miwili ya dhahabu hutoa mafuta yao? Akanijibu, akasema, Hujui hivi ni nini? Nikasema, La, Bwana wangu. Ndipo akasema, Hivi ni hao wana wawili watiwa mafuta, wasimamao karibu na Bwana wa dunia yote.

Soma Zekaria 4