Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 3

3
Mungu anamwita Mose
1Siku moja, Mose alikuwa anachunga kundi la kondoo la baba mkwe wake, Yethro, kuhani wa Midiani. Mose alilipeleka kundi hilo upande wa magharibi wa jangwa, akaufikia mlima Horebu,#3:1 Mlima Horebu: Jina lingine la Mlima Sinai. Unaitwa pia Mlima wa Mungu; nao Waarabu wanauita Mlima wa Mose (jebel Musa); mlima huo uko kusini mwa peninsula ya Sinai. Taz Kut 19:1-2; Kumb 1:2; Gal 4:24-26. mlima wa Mungu. 2Basi, malaika wa Mwenyezi-Mungu#3:2 Malaika wa Mwenyezi-Mungu: Hapa yahusu Mungu mwenyewe (aya 4). Taz Mwa 16:7 maelezo; taz pia Amu 6:22-23; 13:21-22. Na kuhusu “moto”, itakumbukwa kwamba mara kwa mara katika A.K. moto ulikuwa ishara ya Mungu kuwatokea watu. akamtokea katika mwali wa moto katikati ya kichaka. Mose akaangalia, akashangaa kuona kichaka kinawaka moto na wala hakiungui. 3Basi, akajisemea, “Hiki ni kioja! Kichaka kuwaka moto na kisiungue? Hebu nitazame vizuri.”
4Mwenyezi-Mungu alipoona kwamba Mose amegeuka kukiangalia kichaka, akamwita pale kichakani, “Mose! Mose!” Mose akaitika, “Naam! Nasikiliza!” 5Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Usije karibu! Vua viatu vyako#3:5 Vua viatu vyako: Katika Mashariki ya Kati ya Kale watu walikuwa na desturi ya kuvua viatu kila mara walipoingia mahali patakatifu na walifanya hivyo kama alama ya heshima (Yos 5:15). kwa sababu mahali unaposimama ni mahali patakatifu.” 6Kisha Mungu akamwambia, “Mimi ndimi Mungu wa baba yako; Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo.” Mose akaufunika uso wake kwa kuwa aliogopa#3:6 Akafunika uso wake …aliogopa: Jambo la kukaribia alipo Mungu ni kama hatari inayoweza kusababisha kifo kwani ilifikiriwa kwamba hakuna mtu awezaye kumwona Mungu na kisha akaendelea kuishi (Kut 33:20; Isa 6:5; rejea Mwa 32:30; Kumb 5:24-27; Amu 6:22-23; 13:21-22). Lakini katika A.J. uwezekano wa kumwona Mungu unatajwa (taz 1Kor 13:12; 1Yoh 3:2). kumwangalia Mungu.
7Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Nimeyaona mateso ya watu wangu walioko nchini Misri na nimekisikia kilio chao kinachosababishwa na wanyapara wao. Najua mateso yao, 8na hivyo, nimeshuka ili niwaokoe mikononi mwa Wamisri. Nitawatoa humo nchini na kuwapeleka katika nchi nzuri na kubwa; nchi inayotiririka maziwa na asali,#3:8 Nchi inayotiririka maziwa na asali: Maneno yanayotumiwa mara nyingi katika vitabu vitano vya kwanza vya Biblia kueleza wingi wa utajiri na rutuba ya ile nchi waliyoahidiwa Waisraeli yaani Kanaani (Kumb 8:7-9; Hes 16:13). nchi ya Wakanaani, Wahiti, Waamori, Waperizi, Wahivi na Wayebusi. 9Naam, kilio cha Waisraeli kimenifikia; nimeona jinsi Wamisri wanavyowatesa. 10Sasa, nitakutuma kwa Farao ili uwatoe watu wangu, watu hao wa Israeli, kutoka nchini Misri.”
11Lakini Mose akamwambia Mungu, “Mimi ni nani hata nimwendee Farao na kuwatoa Waisraeli nchini Misri?”#3:11 Mimi ni nani …?: Kwa kusema hivyo Mose anaona hakuna uwiano kati ya uwezo wake yeye mwenyewe na hilo jukumu analopewa. Taz Amu 6:15; 1Sam 9:21. 12Mungu akamwambia, “Mimi nitakuwa pamoja nawe. Utawatoa watu wa Israeli na kuja kuniabudu mimi Mungu juu ya mlima huu. Hiyo itakuwa ishara kwamba ni mimi Mungu niliyekutuma wewe.”
13Hapo, Mose akamwambia Mungu, “Sasa, nikiwaendea Waisraeli na kuwaambia, ‘Mungu wa babu zenu amenituma kwenu,’ nao wakiniuliza, ‘Jina lake ni nani,’ nitawaambia nini?”#3:13 Jina lake ni nani?: Hili ni swali muafaka kabisa hapa kwani miungu ya watu wengine ilikuwa na majina yao ya kuitambulisha. 14Mungu akamjibu, “MIMI NDIMI NILIYE.#3:14 MIMI NDIMI NILIYE: Au: NIKO KAMA NILIVYO; au: NITAKUWA KAMA NITAKAVYOKUWA. Maneno hayo yanaeleza jina la Mungu wa Waisraeli. Jina ambalo katika tafsiri hii ni “Mwenyezi-Mungu” (taz 3:15) na inaonekana kwamba Mungu yuko na atakuwako milele na ndiye ambaye yu hai kikweli na sio kama miungu ya uongo. Ling Kut 6:3; Yoh 8:58; Ebr 13:8; Ufu 1:4. Waambie hivi watu wa Israeli: Yule anayeitwa, NDIMI NILIYE, amenituma kwenu. 15Waambie hivi Waisraeli: Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zenu, Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amenituma kwenu. Hili ndilo jina langu milele, na hivyo ndivyo nitakavyokumbukwa katika vizazi vyote.#3:15 Tafsiri hii mpya ya Kiswahili kila mara jina la Kiebrania “Yahweh” linapotumika inatumia jina la kawaida la Mungu kama anavyotajwa katika lugha yetu, yaani, Mwenyezi-Mungu ambaye ni mmoja tu na wala hakuna mwingine. 16Nenda ukawakusanye wazee wa Israeli#3:16 Ukawakusanye wazee wa Israeli: Maneno “wazee wa Israeli” yanatumiwa hapa kwa mara ya kwanza katika Biblia. Katika Kiebrania, neno kwa neno ni wale “wenye ndevu” kwa maana ya wazee ambao walikuwa wazoefu na viongozi wa koo au kabila. na kuwaambia: Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zenu: Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amenitokea na kusema, ‘Nimewachunguzeni na kuyaona mambo mnayotendewa nchini Misri! 17Naahidi kuwa nitawatoa katika mateso yenu huko Misri na kuwapeleka katika nchi ya Wakanaani, Wahiti, Waamori, Waperizi, Wahivi na Wayebusi; nitawapeleka katika nchi inayotiririka maziwa na asali.’
18“Wao watakusikiliza, nawe pamoja na wazee wa Waisraeli mtamwendea mfalme wa Misri na kumwambia, ‘Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Waebrania, ametutokea. Sasa, uturuhusu tuende safari ya mwendo wa siku tatu jangwani, tukamtambikie Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu.’ 19Najua kuwa mfalme wa Misri hatawaacha mwende asipolazimishwa kwa mkono wenye nguvu. 20Kwa hiyo nitaunyosha mkono wangu na kuipiga nchi ya Misri kwa maajabu ambayo nitayafanya huko. Baadaye mfalme atawaacha mwondoke. 21Tena nitahakikisha Wamisri wanawapendelea Waisraeli, na mtakapoondoka Misri, hamtatoka mikono mitupu. 22Kila mwanamke Mwebrania atamwomba jirani yake Mmisri, au mgeni wake aliye nyumbani kwake, ampe vito vya fedha na dhahabu pamoja na nguo.#3:22 Vito vya fedha …na nguo …: Waisraeli walipata mali ya Wamisri kama inavyoelezwa katika Kut 12:35-36. Hivyo mtawavisha watoto wenu wa kiume na wa kike. Ndivyo mtakavyowapokonya Wamisri mali yao.”

Iliyochaguliwa sasa

Kutoka 3: BHNTLK

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia