Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 23

23
Kifo cha Sara#23:1-20 Umuhimu wa Abrahamu kupata mahali pa kumzika mkewe katika nchi ya Kanaani ni kwamba tukio hilo linaashiria hata sasa uhusiano wake na nchi hiyo kutokana na ahadi ya Mungu, kana kwamba huo ni mwanzo tu wa kuinyakua hiyo nchi.
1Sara aliishi miaka 127. Hiyo ndiyo iliyokuwa miaka ya maisha yake Sara. 2Alifia huko Kiriath-arba, yaani Hebroni, katika nchi ya Kanaani. Abrahamu akaomboleza na kumfanyia matanga Sara mkewe. 3Abrahamu akaiacha maiti ya mkewe, akatoka kwenda kuzungumza na Wahiti, akawaambia, 4“Mimi ninaishi kama mgeni miongoni mwenu.#23:4 Naishi kama mgeni miongoni mwenu: Taz Mwa 19:9; Lawi 25:35. Kuwa na mahali pa kuzika watu wake ni muhimu kwa vile ilifikiriwa kwamba hiyo inawapa fursa watu wa jamaa wanaokufa kujiunga na wazee wao (rejea Mwa 49:29-32; 1Fal 13:22; Mate 7:16). Nipatieni sehemu ya ardhi ya kaburi, ili nipate kumzika marehemu mke wangu.” 5Wahiti wakamjibu, 6“Ee bwana wetu, tusikilize; wewe ni kiongozi maarufu#23:6 Kiongozi maarufu: Kiebrania kina maneno yanayotafsirika neno kwa neno kama “Kiongozi wa Mungu”. miongoni mwetu. Mzike marehemu mkeo katika kaburi lolote utakalojichagulia; hakuna yeyote miongoni mwetu atakayekunyima kaburi lake, wala kukuzuia kumzika marehemu mkeo.” 7Hapo Abrahamu akasimama na kuinama kwa heshima mbele ya wananchi Wahiti, 8akawaambia, “Ikiwa mnaniruhusu nimzike marehemu mke wangu, tafadhali mwombeni Efroni mwana wa Sohari, kwa niaba yangu, 9aniuzie lile pango lake la Makpela lililo mpakani mwa shamba lake. Msihini aniuzie nilifanye makaburi yangu; anipatie kwa bei ya haki papa hapa mbele yenu.”
10Efroni mwenyewe alikuwa miongoni mwa Wahiti hao waliokuwa wamekutanika penye lango la mji.#23:10 Penye lango la mji: Hapo palikuwa mahali ambapo matatizo na mambo rasmi yaliweza kupatiwa ufumbuzi wake. Taz Rut 4:1 maelezo; Zab 127:5. Basi, Efroni Mhiti, akamjibu Abrahamu, mbele ya Wahiti wote hapo langoni, 11“La, bwana; tafadhali unisikilize. Ninakupa shamba lote na pango lililomo humo; tena ninakupa mbele ya wananchi wenzangu. Mzike humo marehemu mkeo.”
12Abrahamu akainama tena kwa heshima mbele ya wananchi, 13akamwambia Efroni, wananchi wote wakisikia, “Nakuomba, tafadhali unisikilize. Nitakulipa bei kamili ya shamba lako, na ninakuomba upokee malipo haya, ili nipate kumzika humo marehemu mke wangu.” 14Efroni akamjibu Abrahamu, “Bwana, nisikilize; 15shamba lenye thamani ya shekeli 400 tu za fedha#23:15 Shekeli mia nne … za fedha: Sarafu za fedha hazikutumika huko Palestina kabla ya karne ya saba K.K. Kwa kawaida, kabla ya hapo, watu walipima uzito wa madini au chuma kwa kupimia bei na kununua vitu. ni nini kati yako na mimi? Mzike marehemu mke wako.” 16Abrahamu akakubaliana na Efroni, akampimia kiasi cha fedha alichotaja mbele ya Wahiti wote, fedha shekeli 400, kadiri ya vipimo vya wafanyabiashara wa wakati huo.
17Basi, shamba la Efroni lililoko huko Makpela, mashariki ya Mamre, pango na miti yote iliyokuwamo pamoja na eneo zima, likawa lake 18Abrahamu mbele ya Wahiti wote waliokutanika penye lango la mji. 19Baada ya hayo, Abrahamu akamzika Sara mkewe katika pango hilo lililokuwamo katika shamba la Makpela, mashariki ya Mamre (yaani Hebroni) katika nchi ya Kanaani.#23:19 Katika pango hilo la Makpela, licha ya Sara, walizikwa pia Abrahamu (Mwa 25:9-10), Isaka (Mwa 35:29), Rebeka, Lea na Yakobo (Mwa 49:31; 50:13). Kadiri ya mapokeo fulani kaburi hilo linakisiwa kuwa mahali ambapo sasa ni Msikiti maarufu huko Hebroni. 20Shamba na pango lililokuwamo humo lilithibitishwa na Wahiti liwe mali yake Abrahamu apate kuzika humo wafu wake.

Iliyochaguliwa sasa

Mwanzo 23: BHNTLK

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia