Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 28

28
1Hivyo Isaka akamwita Yakobo, akambariki, akamwagiza akisema, “Usioe mwanamke yeyote Mkanaani. 2Nenda Padan-aramu,#28:2 Padan-aramu: Taz mwa 25:20 maelezo. nyumbani kwa babu yako Bethueli, ukaoe mmojawapo wa binti za mjomba wako Labani. 3Mungu mwenye nguvu#28:3 Mungu Mwenye Nguvu: Kiebrania ni “El Shaday”; taz Mwa 17:1 maelezo. na akubariki upate wazawa wengi na kuongezeka, ili uwe jamii kubwa ya watu. 4Akubariki wewe pamoja na wazawa wako kama alivyombariki Abrahamu, upate kuimiliki nchi ambamo unakaa kama mgeni; nchi ambayo Mungu alimpa Abrahamu!” 5Basi, Isaka akamtuma Yakobo, naye akaenda Padan-aramu kwa Labani, mwana wa Bethueli, Mwaramu, kaka yake Rebeka, mama yao Yakobo na Esau.
Esau anaoa mke wa tatu
6Esau alitambua kwamba Isaka alikuwa amembariki Yakobo na kumtuma aende kuoa huko Padan-aramu, na ya kuwa alipombariki, alimkataza asioe mwanamke Mkanaani. 7Alitambua pia kuwa Yakobo alimtii mama yake na baba yake, akaenda Padan-aramu. 8Basi, Esau akafahamu kwamba baba yake hapendezwi na wanawake wa Kanaani. 9Hivyo, mbali na wale wake zake wengine, Esau akaenda kwa Ishmaeli, mwana wa Abrahamu, akamwoa Mahalathi binti Ishmaeli, dada yake Nebayothi.
Ndoto ya Yakobo kule Betheli
10Yakobo aliondoka Beer-sheba, akaelekea Harani. 11Alipofika mahali fulani, akalala hapo kwa sababu jua lilikuwa limetua. Alichukua jiwe moja la mahali hapo, akaliweka chini ya kichwa chake, akalala. 12Aliota ndoto, na katika ndoto hiyo, aliona ngazi iliyosimamishwa duniani na ncha yake inafika mbinguni. Malaika wa Mungu walikuwa wakipanda na kushuka katika ngazi hiyo. 13Mwenyezi-Mungu alisimama juu ya ngazi hiyo, akamwambia, “Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Abrahamu baba yako, na Mungu wa Isaka. Nchi unayoilalia nitakupa wewe na wazawa wako. 14Wazawa wako watakuwa wengi kama mavumbi ya dunia, na milki yao itaenea kila mahali: magharibi, mashariki, kaskazini na kusini. Kwako jamii zote duniani zitabarikiwa.#28:13-14 Kwako jamii zote duniani zitabarikiwa: Taz Mwa 12:2-3 maelezo. Ahadi aliyopewa Abrahamu (Mwa 12:1-3; 13:14-15; 15:18-21; 22:16-18) na ile aliyopewa Isaka (Mwa 26:3-5); sasa inarudiwa upya kwa Yakobo (rejea Mwa 46:3). 15Mimi nipo pamoja nawe;#28:15 Mimi niko pamoja nawe: Taz Mwa 26:3 maelezo. nitakulinda popote uendapo na kukurudisha katika nchi hii. Sitakuacha mpaka nitakapotimiza ahadi niliyokupa.”
16Ndipo Yakobo akaamka usingizini, akasema, “Hakika, Mwenyezi-Mungu yupo mahali hapa, nami sikujua!” 17Yakobo akaogopa na kusema, “Mahali hapa panatisha kama nini! Bila shaka hapa ni nyumba ya Mungu#28:17 Nyumba ya Mungu: Maneno haya ni tafsiri ya neno la Kiebrania “Bethel”. Betheli ulikuwa mji wa kale wa Wakanaani ambao baadaye ulimilikiwa na Waisraeli (rejea Amu 1:22-26). Huko Betheli kulikuwa na mahali pa zamani sana pa ibada (rejea Mwa 12:8; 13:3; 1Fal 12:29; Amo 7:13). na lango la mbinguni.”
18Yakobo akaamka asubuhi na mapema, akachukua lile jiwe alilokuwa ameliweka chini ya kichwa chake, akalisimika kama nguzo na kuliweka wakfu kwa kulimiminia mafuta.#28:18 Katika Mashariki ya Kati ya Kale, minara au mawe ya ukumbusho mara nyingi ilitumiwa kukumbuka tukio fulani la maana kama vile ushindi dhidi ya adui, mkataba au hata kujionesha kwa Mungu (rejea Mwa 31:45-54; taz pia Kut 24:4 maelezo). Muda mrefu baadaye sheria iliamuru kwamba mawe ya ukumbusho ambayo yalikuwa yamehusishwa na ibada za watu wa Kanaani lazima yatokomezwe (rejea Kumb 7:5; 12:3; 16:22). 19Akapaita mahali hapo Betheli;#28:19 Betheli: Taz Mwa 28:17 maelezo. lakini jina la awali la mji huo lilikuwa Luzu. 20Kisha Yakobo akaweka nadhiri akisema, “Iwapo, ee Mungu, utakuwa pamoja nami na kunilinda katika safari yangu, ukinipa chakula na mavazi 21ili nirudi nyumbani kwa baba yangu salama, basi, wewe Mwenyezi-Mungu utakuwa ndiwe Mungu wangu. 22Nalo jiwe hili nililosimika hapa kama nguzo, litakuwa nyumba yako Mungu, nami nitakupa sehemu moja ya kumi ya vitu#28:22 Sehemu ya kumi ya vitu: Desturi ya kutoa sehemu ya kumi (au asilimia kumi) ya mali ya mtu na kumtolea Mungu ilifanyika huko nchini Kanaani hata kabla ya kuwasili Waisraeli nchini humo (rejea Mwa 14:20). Baadaye sheria ya Mose iliingiza desturi hiyo katika Israeli kama njia ya kufanikisha mahitaji ya ibada kwa Mungu (Kumb 12:6,17-18; 26:12). vyote utakavyonipa.”

Iliyochaguliwa sasa

Mwanzo 28: BHNTLK

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia