Matendo 5
5
Anania na Safira
1Alikuwepo mtu aliyeitwa Anania na mke wake aliyeitwa Safira. Anania aliuza shamba lake, 2lakini aliwapa mitume sehemu tu ya pesa alizopata baada ya kuuza shamba lake. Kwa siri alibakiza kiasi cha pesa kwa ajili yake mwenyewe. Mke wake alilijua hili na akalikubali.
3Petro akasema, “Anania, kwa nini umemruhusu Shetani aitawale akili yako kwa wazo la namna hii? Umebakiza sehemu ya pesa kwa ajili yako mwenyewe na kumdanganya Roho Mtakatifu! 4Je! kabla ya kuuza shamba, halikuwa lako? Na hata baada ya kuliuza, ungeweza kutumia pesa kwa namna yoyote unayotaka. Imekuwaje hata ufikirie kufanya jambo hili? Hukutudanganya sisi bali Mungu!”
5-6Anania aliposikia hili, alianguka chini na kufa. Baadhi ya vijana wakaja na kuufunga mwili wake. Wakautoa nje na kuuzika. Kila mtu aliyelisikia hili aliingiwa hofu.
7Baada ya kama saa tatu baadaye, mkewe naye alifika. Safira hakujua kilichompata mumewe. 8Petro akamwambia, “Niambie mlipata pesa kiasi gani baada ya kuuza shamba lenu. Kilikuwa kiasi hiki?”
Safira akajibu, “Ndiyo, hicho ndicho tulichopata baada ya kuuza shamba.”
9Petro akamwambia, “Kwa nini wewe na mume wako mlikubaliana kumjaribu Roho wa Bwana? Sikiliza! Unasikia vishindo hivyo vya miguu? Watu waliomzika mume wako, wako mlangoni. Watakuchukua nje kwa njia hiyo hiyo.” 10Safira akaanguka miguuni kwa Petro na kufa papo hapo. Vijana wakaingia, walipomwona amekwisha kufa, walimchukua na kumzika kando ya mume wake. 11Kanisa lote na watu wote waliosikia kuhusu hili waliingiwa hofu.
Uthibitisho kutoka kwa Mungu
12Mitume walipewa nguvu ya kufanya ishara nyingi za miujiza na maajabu katikati ya watu. Walikuwa wanakutanika pamoja mara kwa mara katika eneo la Hekalu lililoitwa Ukumbi wa Sulemani. 13Hakuna mtu yeyote ambaye hakuwa mwamini alikaa na kushirikiana nao, lakini kila mtu alisema mambo mazuri juu yao. 14Watu wengi zaidi na zaidi walimwamini Bwana; na watu wengi, wanaume kwa wanawake waliongezwa katika kundi la waamini. 15Hivyo watu waliwatoa wagonjwa majumbani na kuwaweka mitaani katika vitanda vidogo na mikeka. Walitumaini kuwa ikiwa Petro atapita karibu yao na kivuli chake kikawaangukia watapona. 16Watu walikuja kutoka katika miji kuzunguka Yerusalemu. Waliwaleta wagonjwa au waliosumbuliwa na pepo wachafu. Wote waliponywa.
Mitume Wakamatwa
17Kuhani mkuu na wafuasi wake wote wa karibu, kundi liitwalo Masadukayo wakaingiwa wivu sana. 18Waliwakamata mitume na kuwafunga katika gereza la mji. 19Lakini wakati wa usiku, malaika wa Bwana alifungua milango ya gereza. Malaika akawaongoza mitume nje ya gereza na kusema, 20“Nendeni mkasimame katika eneo la Hekalu. Waelezeni watu kila kitu kuhusu maisha haya mapya.” 21Mitume waliposikia hili, walifanya kama walivyoambiwa. Walikwenda katika eneo la Hekalu asubuhi na mapema jua lilipokuwa linachomoza na kuanza kuwafundisha watu.
Kuhani mkuu na wafuasi wake wakakusanyika na kuitisha mkutano wa Baraza kuu na wazee wa Kiyahudi. Wakawatuma baadhi ya watu gerezani ili wawalete mitume kwao. 22Watu wale walipokwenda gerezani, hawakuwaona mitume. Hivyo walirudi na kuwaambia viongozi wa Kiyahudi kuhusu hili. 23Walisema, “Gereza lilikuwa limefungwa na milango ilikuwa imefungwa. Walinzi walikuwa wamesimama milangoni. Lakini tulipofungua milango, gereza lilikuwa tupu!” 24Mkuu wa walinzi wa Hekalu na viongozi wa makuhani walipolisikia hili, walichanganyikiwa na kujiuliza maana yake ni nini.
25Ndipo mtu mwingine akaja na kuwaambia, “Sikilizeni! Watu mliowafunga gerezani wamesimama katika eneo la Hekalu wanawafundisha watu!” 26Mkuu wa walinzi na askari walinzi wa Hekalu walikwenda na kuwarudisha mitume. Lakini askari hawakutumia nguvu, kwa sababu waliwaogopa watu. Waliogopa watu wangewapiga kwa mawe mpaka wafe.
27Askari waliwaleta mitume na kuwasimamisha mbele ya baraza. Kuhani mkuu akawauliza. 28Akisema, “Tuliwaambia msifundishe tena kwa kutumia jina lile. Lakini tazameni mlichofanya! Mmeujaza mji wa Yerusalemu kwa mafundisho yenu. Na mnajaribu kutulaumu sisi kwa sababu ya kifo chake.”
29Petro na mitume wengine wakajibu, “Ni lazima tumtii Mungu, siyo wanadamu! 30Mlimwua Yesu kwa kumpigilia msalabani. Lakini Mungu, Mungu yule yule wa Baba zetu, alimfufua Yesu kutoka kwa wafu. 31Yesu ndiye ambaye Mungu amemtukuza kwa kumpa nafasi upande wake wa kuume. Amemfanya kuwa Kiongozi na Mwokozi wetu. Mungu alifanya hivi ili kuwapa watu wote wa Israeli fursa ya kubadilika na kumgeukia Mungu ili dhambi zao zisamehewe. 32Tuliona mambo haya yote yakitokea, na tunathibitisha kuwa ni ya kweli. Pia, Roho Mtakatifu anaonesha kuwa mambo haya ni ya kweli. Mungu amemtoa Roho huyu kwa ajili ya wote wanaomtii Yeye.”
33Wajumbe wa Baraza waliposikia haya, walikasirika sana. Walianza kupanga namna ya kuwaua mitume. 34Lakini mjumbe mmoja wa Baraza, Farisayo aliyeitwa Gamalieli, akasimama, alikuwa mwalimu wa sheria na watu wote walimheshimu. Aliwaambia wajumbe wawatoe nje mitume kwa dakika chache. 35Kisha akawaambia, “Wanaume wa Israeli, iweni waangalifu kwa kile mnachopanga kuwatendea watu hawa. 36Mnakumbuka Theuda alipotokea? Alijidai kuwa alikuwa mtu mkuu, na wanaume kama mia nne waliungana naye. Lakini aliuawa na wote waliomfuata walitawanyika. 37Baadaye, wakati wa sensa, mtu mmoja aitwaye Yuda alikuja kutoka Galilaya. Watu wengi walijiunga kwenye kundi lake, lakini yeye pia aliuawa na wafuasi wake wote walitawanyika. 38Na sasa ninawaambia, kaeni mbali na watu hawa. Waacheni. Ikiwa mpango wao ni kitu walichopanga wao wenyewe, utashindwa. 39Lakini ikiwa ni mpango wa Mungu, hamtaweza kuwazuia. Mnaweza kuwa mnapigana kinyume na Mungu mwenyewe!”
Viongozi wa Kiyahudi wakakubaliana na kile alichosema Gamalieli. 40Wakawaita mitume ndani tena. Wakawachapa viboko na kuwakanya waache kusema na watu kwa kutumia jina la Yesu. Kisha wakawaachia huru. 41Mitume waliondoka kwenye mkutano wa Baraza, wakifurahi kwamba wamepewa heshima ya kudharauliwa kwa ajili ya Yesu. 42Mitume hawakuacha kuwafundisha watu. Waliendelea kuzisema Habari Njema, kwamba Yesu ni Masihi. Walifanya hivi kila siku katika eneo la Hekalu na katika nyumba za watu.
Iliyochaguliwa sasa
Matendo 5: TKU
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Toleo la Awali
© 2017 Bible League International