Matendo 9
9
Sauli Awa Mfuasi wa Yesu
1Huko Yerusalemu Sauli aliendelea kuwatisha wafuasi wa Bwana, na hata kuwaambia kuwa angewaua. Alikwenda kwa kuhani mkuu, 2na kumwomba aandike barua kwenda kwenye masinagogi yaliyokuwa katika mji wa Dameski. Sauli alitaka kuhani mkuu ampe mamlaka ya kuwatafuta watu katika mji wa Dameski waliokuwa wafuasi wa Njia ya Bwana.#9:2 Njia ya Bwana Ni maneno yaliyotumika ili kuainisha tabia na mafundisho ya Yesu. Ikiwa angewapata waamini huko, wanaume au wanawake, angewakamata na kuwaleta Yerusalemu.
3Hivyo Sauli alikwenda Dameski. Alipoukaribia mji, ghafla mwanga mkali kutoka mbinguni ukaangaza kumzunguka. 4Akadondoka chini na akasikia sauti ikimwambia, “Sauli, Sauli! Kwa nini unanitesa?”
5Sauli akasema, “Wewe ni nani, Bwana?”
Sauti ikajibu, “Mimi ni Yesu, unayemtesa. 6Simama sasa na uingie mjini. Mtu mmoja huko atakueleza unachopaswa kufanya.”
7Wanaume waliokuwa wanasafiri pamoja na Sauli walisimama pale kimya. Waliisikia sauti, lakini hawakumwona yeyote. 8Sauli alisimama kutoka chini na kufumbua macho yake, lakini hakuweza kuona. Hivyo wale aliokuwa nao wakamshika mkono na kumwongoza kuingia Dameski. 9Kwa siku tatu Sauli hakuweza kuona; hakula wala kunywa.
10Alikuwepo mfuasi wa Yesu katika mji wa Dameski aliyeitwa Anania. Katika maono Bwana alimwita, “Anania!”
Anania alijibu, “Niko hapa, Bwana.”
11Bwana akamwambia, “Amka na uende katika mtaa unaoitwa Mtaa Ulionyooka. Tafuta nyumba ya Yuda#9:11 Yuda Huyu si mmoja wa mitume aliyeitwa Yuda. na uliza kuhusu mtu anayeitwa Sauli anayetoka katika mji wa Tarso. Yuko katika nyumba hiyo sasa, anaomba. 12Ameoneshwa katika maono kuwa mtu anayeitwa Anania anamwendea na kuweka mikono juu yake ili aweze kuona tena.”
13Lakini Anania akajibu, “Bwana, watu wengi wameniambia kuhusu mtu huyu. Wameniambia kuhusu mambo mengi mabaya aliyowatendea watu wako watakatifu katika mji wa Yerusalemu. 14Na sasa amekuja hapa Dameski. Viongozi wa makuhani wamempa mamlaka ya kuwakamata watu wote wanaokuamini wewe.”#9:14 wanaokuamini wewe Kwa maana ya kawaida, “wanaoliitia jina lako”, ikimaanisha kumwamini Yesu kwa kumwabudu au kumwomba Yeye.
15Lakini Bwana Yesu akamwambia Anania, “Nenda, nimemchagua Sauli kwa kazi maalumu. Ninataka ayahubiri mataifa mengine, watawala na watu wa Israeli kuhusu mimi. 16Nitamwonyesha yote ambayo lazima atateseka kwa ajili yangu.”
17Hivyo Anania aliondoka na kwenda nyumbani kwa Yuda. Akaweka mikono yake juu ya Sauli na kusema, “Sauli, ndugu yangu, Bwana Yesu amenituma. Ndiye uliyemwona barabarani wakati ukija hapa. Amenituma ili uweze kuona tena, pia ujazwe Roho Mtakatifu.” 18Ghafla, vitu kama magamba ya samaki vikaanguka kutoka kwenye macho ya Sauli. Akaanza kuona tena! Kisha akasimama na kwenda kubatizwa. 19Baada ya kula chakula, akaanza kujisikia kuwa na nguvu tena.
Sauli Aanza Kuhubiri Juu ya Yesu Kristo
Sauli alikaa pamoja na wafuasi wa Yesu katika mji wa Dameski kwa siku chache. 20Baadaye alianza kwenda katika masinagogi na kuwahubiri watu kuhusu Yesu. Aliwaambia watu, “Yesu ni Mwana wa Mungu!”
21Watu wote waliomsikia Sauli walishangaa. Wakaulizana, “Je! huyu si yule aliyekuwa anajaribu kuwaangamiza watu wanaomwamini Yesu#9:21 wanaomwamini Yesu Kwa maana ya kawaida, “wanaoliitia jina lake”. katika mji wa Yerusalemu? Na hakuja hapa ili awakamate wafuasi wa Yesu na kuwarudisha kwa viongozi wa makuhani?”
22Lakini Sauli aliendelea kuwa nguvu katika kuthibitisha kwamba Yesu ndiye Masihi. Uthibitisho wake ulikuwa na nguvu kiasi kwamba Wayahudi walioishi Dameski hawakuweza kubishana naye.
Sauli Awatoroka Wayahudi
23Baada ya siku nyingi kupita, baadhi ya Wayahudi waliweka mpango wa kumwua Sauli. 24Waliyalinda malango ya mji usiku na mchana. Walitaka kumwua Sauli, lakini aliambiwa kuhusu mpango wao. 25Usiku mmoja baadhi ya wafuasi ambao Sauli aliwafundisha walimsaidia kuondoka mjini. Walimweka katika kikapu, wakamtoa kwa kumshusha kupitia kwenye tundu lililokuwa kwenye ukuta wa mji.
Sauli Katika Mji wa Yerusalemu
26Kisha Sauli alikwenda Yerusalemu. Akajaribu kujiunga na kundi la wafuasi, lakini wote walimwogopa. Hawakuamini kuwa naye amekuwa mfuasi wa Yesu. 27Lakini Barnaba alimkubali Sauli, akamchukua na kumpeleka kwa mitume. Akawaeleza namna ambavyo Sauli alimwona Bwana akiwa njiani na namna ambavyo Bwana aliongea naye. Kisha akawaambia namna ambavyo Sauli amehubiri kwa ujasiri kuhusu Yesu katika mji wa Dameski.
28Sauli alikaa na wafuasi na kwenda kila mahali katika mji wa Yerusalemu akihubiri kwa ujasiri kwa ajili ya Bwana. 29Kila mara alibishana na Wayahudi waliokuwa waliozungumza Kiyunani,#9:29 Kiyunani Au “Kigiriki”. ambao walianza kutengeneza mpango wa kumwua. 30Waamini walipoujua mpango huu, walimchukua Sauli mpaka Kaisaria, na kutoka huko walimsafirisha mpaka katika mji wa Tarso.
31Kanisa katika Uyahudi yote, Galilaya na Samaria likawa na wakati wa amani. Na kwa msaada wa Roho Mtakatifu, vikundi hivi vya waamini vikawa na nguvu katika imani na kuonesha utii kwa ajili ya Bwana kwa namna walivyoishi. Hivyo kanisa kila mahali liliongezeka kwa idadi.
Petro akiwa Lida na Yafa
32Petro alikuwa akisafiri katika sehemu zote za Uyahudi, Galilaya na Samaria, na akasimama kuwatembelea waamini#9:32 waamini Kwa maana ya kawaida, “watakatifu”, jina kwa ajili ya watu waliomwamini Yesu. Pia katika mstari wa 41. walioishi Lida. 33Huko alikutana na mtu aliyeitwa Ainea, ambaye alikuwa amepooza na hakuweza kutoka kitandani kwa miaka nane. 34Petro akamwambia, “Ainea, Yesu Kristo amekuponya. Simama na kiweke kitanda chako vizuri!” Ainea alisimama saa ile ile. 35Watu wote walioishi Lida na tambarare ya Sharoni walimwona, na wakaamua kumfuata Bwana.
36Katika mji wa Yafa kulikuwa na mfuasi wa Yesu aliyeitwa Tabitha, Jina lake kwa Kiyunani lilikuwa Dorkasi.#9:36 Dorkasi Maana yake ni mnyama aitwaye paa. Daima aliwatendea watu mambo mema na kuwapa pesa wale wenye mahitaji. 37Petro alipokuwa Lida, Tabitha aliugua na kufa. Waliusafisha mwili wake na kuuweka chumbani ghorofani. 38Wafuasi waliokuwa Yafa wakasikia kuwa Petro yuko Lida, mji ambao haukuwa mbali na Yafa. Hivyo waliwatuma watu wawili, waliomsihi Petro wakisema, “Tafadhali njoo kwetu haraka!”
39Petro alijiandaa na kwenda pamoja nao. Alipofika, walimchukua na kumpeleka kwenye chumba ghorofani. Wajane wote walisimama wakamzunguka huku wakilia na wakamwonesha mavazi ambayo Tabitha alitengeneza alipokuwa hai. 40Petro akawatoa watu wote chumbani. Akapiga magoti na kuomba. Kisha akaugeukia mwili wa Tabitha na kusema, “Tabitha! Simama.” Akafumbua macho yake. Alipomwona Petro akaketi. 41Petro akamshika mkono na akamsaidia kusimama. Ndipo akawaita waamini na wajane chumbani. Akawaonyesha Tabitha; akiwa hai!
42Watu kila mahali katika mji wa Yafa wakatambua kuhusu hili, na wengi wakamwamini Bwana. 43Petro alikaa Yafa siku nyingi nyumbani kwa mtu mmoja aitwaye Simoni, aliyekuwa mtengenezaji wa ngozi.
Iliyochaguliwa sasa
Matendo 9: TKU
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Toleo la Awali
© 2017 Bible League International