Luka 2
2
Kuzaliwa kwa Yesu
(Mt 1:18-25)
1Ulikuwa wakati ambapo amri ilitolewa na Kaisari Augusto kwamba watu wote wanaoishi katika utawala wote wa Rumi#2:1 Rumi Au “dola ya ulimwengu ya Rumi”. wahesabiwe na kuorodheshwa#2:1 wahesabiwe na kuorodheshwa Yaani, “Sensa”, lengo hasa ilikuwa waorodheshwe katika kumbukumbu za serikali kwa ajili ya kulipa kodi. katika kumbukumbu za serikali. 2Orodha hii ilikuwa ya kwanza tangu Kirenio alipokuwa gavana wa Shamu. 3Kila mtu alikwenda katika mji aliozaliwa ili akahesabiwe na kuingizwa katika orodha hiyo.
4Hivyo Yusufu alitoka Nazareti, mji uliokuwa katika jimbo la Galilaya na kwenda katika mji wa Bethlehemu uliokuwa katika jimbo la Uyahudi. Pia, mji huu ulijulikana kama mji wa Daudi. Yusufu alikwenda Bethlehemu kwa sababu alikuwa mzaliwa wa ukoo wa Daudi. 5Yusufu alijiandikisha akiwa pamoja na Mariamu kwani alikuwa tayari amemchumbia ili amwoe. Na Mariamu alikuwa mjamzito. 6Yusufu na Mariamu walipokuwa Bethlehemu, wakati wa Mariamu kujifungua ulifika. 7Akamzaa mwanawe wa kwanza. Akamvingirishia nguo vizuri, kisha akamlaza katika hori la kulishia mifugo.#2:7 hori la kulishia mifugo Sehemu au chombo cha kulishia mifugo. Pia katika mstari wa 12 na 16. Walimweka humo kwa sababu chumba cha wageni kilikuwa kimejaa.
Wachungaji wa Mifugo Wajulishwa Kuhusu Yesu
8Usiku ule, baadhi ya wachungaji walikuwa mashambani nje ya mji wa Bethlehemu wakilinda kondoo zao. 9Malaika wa Bwana akawatokea ghafla, na utukufu wa Bwana ukaangaza kuwazunguka, wakaogopa sana. 10Malaika akawaambia, “Msiogope, kwa kuwa nimewaletea habari njema zitakazowafurahisha watu wa Mungu wote. 11Kwa sababu leo katika mji wa Daudi amezaliwa Mwokozi, ndiye Kristo,#2:11 Kristo Kwa maana ya kawaida “Kristo”, ni tafsiri ya Kiyunani ya neno la Kiebrania “Masihi” linalomaanisha “Mpakwa Mafuta”, ambapo katika Agano la Kale linawakilisha sherehe ya kupakwa mafuta (Kuwekwa Wakfu) mfalme mpya. Pia linamaanisha Mfalme Mteule. Tazama Kristo na Masihi katika Orodha ya Maneno. Pia katika mstari wa 26 na katika kitabu chote hiki. Bwana. 12Na hivi ndivyo mtakavyomtambua: Mtamkuta mtoto mchanga amevingirishiwa nguo na amelala katika hori la kulishia mifugo.”
13Kisha malaika pamoja na jeshi kubwa la mbinguni wakaanza kumsifu Mungu, wakisema:
14“Atukuzwe Mungu juu mbinguni,
na amani iwepo duniani
kwa watu wote wanaompendeza.”
15Malaika walipoondoka kurudi mbinguni, wale wachungaji wakaambiana wakisema, “Twendeni Bethlehemu, tukalione jambo hili lililotokea, ambalo Bwana ametujulisha.”
16Wakaenda haraka, wakamkuta Mariamu na Yusufu, na yule mtoto mchanga amelala katika hori la kulishia mifugo. 17Wachungaji walipomwona huyo mtoto, walisimulia kile walichoambiwa na malaika kuhusu mtoto. 18Kila aliyesikia maelezo ya wachungaji, alishangaa. 19Mariamu aliendelea kuyatafakari mambo haya, na kuyaweka moyoni. 20Wachungaji waliirudia mifugo yao, wakawa wanamsifu na kumshukuru Mungu kwa mambo yote waliyosikia na kuyaona. Ilikuwa kama walivyoambiwa na malaika.
21Ilipofika siku ya nane mtoto alitahiriwa, akaitwa Yesu. Hili ndilo jina alilopewa na malaika kabla mama yake hajaibeba mimba yake.
Yesu Atambulishwa Hekaluni
22Muda wa kutakaswa ulimalizika, kama ilivyotakiwa na Sheria ya Musa baada ya mtoto kuzaliwa.#2:22 baada ya mtoto kuzaliwa Sheria ya Musa iliagiza kuwa ifikapo siku 40 baada mwanamke wa Kiyahudi kuzaa mtoto, yule mtoto anapaswa kutakaswa kwa sherehe maalumu Hekaluni. Tazama Law 12:2-8. Baada ya hapo walimpeleka Yesu Yerusalemu na kumweka mbele za Bwana. 23Kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana: Mzaliwa wa kwanza akiwa mtoto wa kiume, atolewe wakfu kwa ajili ya Bwana.#2:23 wakfu kwa ajili ya Bwana Tazama Kut 13:2,12. 24Pia Mariamu na Yusufu walikwenda Yerusalemu kutoa dhabihu kama Sheria ya Bwana inavyosema kuwa, “Ni lazima utoe dhabihu ya jozi moja ya hua#2:24 hua Hua (au tetere) ni njiwa wa porini, ni wadogo kuliko wale wanaofugwa na huruka kwa mwendo kasi. Imenukuliwa kutoka Law 12:8. au makinda mawili wa njiwa.”
Simeoni Amwona Yesu
25Alikuwepo mtu mmoja aliyeishi katika mji wa Yerusalemu, mtu huyu aliitwa Simeoni. Alikuwa mtu mwema na mcha Mungu na Roho Mtakatifu alikuwa pamoja naye. Alikuwa akiusubiri wakati ambao Mungu angeisaidia Israeli. 26Roho Mtakatifu alimwambia kwamba asingekufa kabla ya kumwona Masihi kutoka kwa Bwana. 27Roho Mtakatifu alimwongoza mpaka Hekaluni. Hivyo, alikuwemo Hekaluni wakati Mariamu na Yusufu walipomleta mtoto Yesu ili wamfanyie kama ilivyotakiwa katika Sheria ya Kiyahudi. 28Simeoni alimbeba mtoto Yesu mikononi mwake, akamshukuru Mungu na kusema,
29“Sasa, Bwana, niruhusu mimi mtumishi wako nife kwa amani
kwa kuwa umeitimiza ahadi yako kwangu.
30Nimeona kwa macho yangu namna utakavyowaokoa watu wako.
31Sasa watu wote wanaweza kuuona mpango wako.
32Yeye ni mwanga wa kuionesha njia yako kwa mataifa mengine,
na atawaletea heshima watu wako Israeli.”
33Mariamu na Yusufu walishangazwa sana na maneno aliyosema Simeoni kuhusu Yesu. 34Kisha Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu; “Wayahudi wengi wataanguka na wengi watainuka kwa sababu ya mtoto huyu. Atakuwa ishara kutoka kwa Mungu, lakini baadhi ya watu watamkataa. 35Mawazo ya siri ya watu wengi yatajulikana. Na mambo yatakayotokea yatakuumiza, kama upanga unaokuchoma moyoni.”
Ana Amwona Yesu
36Alikuwapo nabii aliyeitwa Ana binti Fanueli, kutoka katika kabila la Asheri. Alikuwa mwanamke mzee sana. Aliishi na mume wake kwa miaka saba, 37kabla ya mume wake kufa na kumwacha peke yake. Na sasa alikuwa na umri wa miaka themanini na nne. Ana alikuwa Hekaluni daima, hakutoka. Alimwabudu Mungu kwa kufunga na kuomba usiku na mchana.
38Simeoni alipokuwa anazungumza na Yusufu na Mariamu, Ana alikwenda walipokuwa na akaanza kumsifu Mungu na kuwaambia kuhusu Yesu watu wote waliokuwa wanasubiri Mungu kuikomboa Yerusalemu.
Yusufu, Mariamu na Yesu Warudi Nyumbani
39Yusufu na Mariamu walipotimiza mambo yote yanayotakiwa katika sheria ya Bwana, walirudi Galilaya, katika mji wao wa Nazareti. 40Mtoto Yesu aliendelea kukua na kuwa kijana mwenye nguvu na aliyejaa hekima nyingi. Na Mungu alikuwa anambariki.
Yesu Akiwa Mvulana
41Kila mwaka wazazi wa Yesu walikwenda Yerusalemu kwa ajili ya sikukuu ya Pasaka. 42Yesu alipokuwa na umri wa miaka kumi na miwili, walikwenda kwenye sikukuu kama ilivyokuwa desturi ya Kiyahudi. 43Sikukuu ilipokwisha, walirudi nyumbani, lakini Yesu alibaki Yerusalemu bila wazazi wake kutambua. 44Walianza kumtafuta kwa jamaa na rafiki zao baada ya kusafiri kutwa nzima, wakidhani kuwa alikuwa pamoja nao katika msafara. 45Walipomkosa, walirudi Yerusalemu kumtafuta.
46Ikawa baada ya siku tatu wakamkuta Hekaluni, amekaa katikati ya walimu wa dini, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. 47Na wote waliomsikiliza walishangazwa sana kwa ufahamu wake na majibu yake ya busara. 48Wazazi wake walipomwona walishangaa pia, ndipo mama yake akamwambia, “Mwanangu, kwa nini umefanya hivi? Mimi na baba yako tulikuwa na wasiwasi sana, na tumekuwa tukikutafuta.”
49Yesu akawaambia, “Kwa nini mlikuwa mnanitafuta? Mnapaswa kujua kuwa inanilazimu kuwemo nyumbani mwa Baba yangu?” 50Lakini wao hawakuelewa alichowaambia.
51Yesu alirudi pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii. Mama yake aliendelea kuyaweka mambo haya yote moyoni mwake. 52Naye Yesu akakua katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu.
Iliyochaguliwa sasa
Luka 2: TKU
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Toleo la Awali
© 2017 Bible League International