Luka 5
5
Yesu Achagua Baadhi ya Wafuasi
(Mt 4:18-22; Mk 1:16-20)
1Yesu aliposimama ukingoni mwa Ziwa Galilaya#5:1 Galilaya Kwa maana ya kawaida, “Genesareti”. kundi la watu lilimsogelea ili wasikie mafundisho kuhusu Mungu. 2Yesu aliona mashua mbili zikiwa kando ya ziwa. Wavuvi walikuwa wametoka katika mashua zao na walikuwa wanaosha nyavu zao. 3Yesu aliingia kwenye mashua ya Simoni. Akamwomba Simoni aisogeze mbali kidogo na ufukwe wa ziwa. Kisha akaketi ndani ya mashua na akawafundisha watu waliokuwa ufukweni mwa ziwa.
4Yesu alipomaliza kufundisha, alimwambia Simoni, “Ipeleke mashua mpaka kwenye kilindi cha maji kisha mshushe nyavu zenu majini na mtapata samaki.”
5Simoni akamjibu, “Bwana, tumejitahidi usiku kucha kuvua samaki na hatukupata chochote. Lakini kwa kuwa unasema nishushe nyavu majini, nitafanya hivyo.” 6Walipofanya hivi, nyavu zao zilijaa samaki wengi mpaka zikaanza kuchanika. 7Waliwaita rafiki zao waliokuwa katika mashua nyingine ili waje wawasaidie. Rafiki zao walikuja kuwasaidia, na mashua zote mbili zilijaa samaki kiasi cha kutaka kuzama.
8-9Wavuvi wote walistaajabu kwa sababu ya wingi wa samaki waliovua. Simoni Petro alipoona hili, akapiga magoti mbele ya Yesu na akasema, “Nenda mbali nami Bwana, mimi ni mwenye dhambi!” 10Yakobo na Yohana wana wa Zebedayo, walishangaa pia. (Yakobo na Yohana walikuwa wanavua pamoja na Simoni.)
Yesu akamwambia Simoni, “Usiogope. Kuanzia sasa kazi yako haitakuwa kuvua samaki bali kukusanya watu!”
11Wakaziendesha mashua zao mpaka pwani, kisha wakaacha kila kitu na kumfuata Yesu.
Yesu Amponya Mgonjwa
(Mt 8:1-4; Mk 1:40-45)
12Wakati mmoja Yesu alikuwa katika mji ambao mwanaume mmoja mgonjwa alikuwa anaishi. Mwanaume huyo alikuwa na ugonjwa hatari sana wa ngozi mwili wake wote. Alipomwona Yesu, alimsujudia na kumsihi akisema, “Bwana, ikiwa unataka una uwezo wa kuniponya.”
13Yesu akasema, “Hakika ninataka kukuponya, upone!” Kisha akamgusa, na ugonjwa ukatoweka papo hapo. 14Yesu akamwambia, “Usimwambie mtu yeyote kilichotokea. Lakini nenda kwa kuhani akakuchunguze.#5:14 kuhani akakuchunguze Sheria ya Musa ilisema ni lazima kuhani aamue ikiwa mtu aliyekuwa na ugonjwa hatari wa ngozi amepona. Na umtolee Mungu sadaka ambazo Musa aliamuru watu wanaoponywa watoe, ili iwe ushahidi kwa watu kwamba umepona.”
15Lakini habari kuhusu Yesu zilizidi kuenea zaidi. Watu wengi walikuja kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao. 16Mara nyingi Yesu alikwenda sehemu zingine zisizokuwa na watu na akaomba huko.
Yesu Amponya Aliyepooza
(Mt 9:1-8; Mk 2:1-12)
17Siku moja Yesu alikuwa anawafundisha watu. Mafarisayo na walimu wa sheria walikuwa wameketi hapo pia. Walitoka katika kila mji wa Galilaya, na Uyahudi, na Yerusalemu. BWANA alimpa Yesu uwezo wa kuponya watu. 18Alikuwepo mtu aliyepooza na baadhi ya watu walikuwa wamembeba kwenye machela. Walijaribu kumwingiza ndani ili wamweke mbele ya Yesu. 19Lakini walishindwa kufika alipokuwa Yesu kwa sababu kulikuwa na watu wengi sana. Hivyo walikwenda juu ya paa ya nyumba na kumshusha aliyepooza chini kupitia tundu kwenye dari. Waliishusha machela alimokuwa aliyepooza kwa usawa kiasi kwamba akawa amelala mbele ya Yesu. 20Yesu alipoona imani waliyokuwa nayo, akamwambia yule mgonjwa: “Rafiki yangu, dhambi zako zimesamehewa!”
21Walimu wa sheria na Mafarisayo wakaanza kuhojiana wao kwa wao wakisema: “Huyu mtu ni nani kiasi cha kuthubutu kusema hivi? Si anamtukana Mungu! Mungu peke yake ndiye anayesamehe dhambi.”
22Lakini Yesu alijua walichokuwa wanawaza, akawaambia: “Kwa nini mna maswali haya mioyoni mwenu? 23-24Wakati akiwa duniani Mwana wa Adamu anayo mamlaka ya kusamehe dhambi. Lakini nitawezaje kulithibitisha hili kwenu? Pengine mnafikiri ilikuwa rahisi kwangu kumwambia mtu huyu aliyepooza, ‘Dhambi zako zimesamehewa.’ Kwa sababu hilo haliwezi kuthibitishwa kwamba hakika limetokea. Lakini vipi nikimwambia, mtu huyu, beba machela yako na utembee? Hapo ndipo mtakapoweza kuona kama kweli ninayo mamlaka hayo ama sina.” Kwa hiyo Yesu akamwambia mtu yule aliyepooza, “Nitalithibitishaje hili kwako? Ninakwambia hivi, Inuka! Beba machela yako uende nyumbani!”
25Yule mtu akasimama saa ile ile mbele ya kila mtu. Akaubeba machela yake na kwenda nyumbani kwake, akimsifu Mungu. 26Kila mtu alishangaa na kuanza kumsifu Mungu. Wakajawa na hofu kuu baada ya kuiona nguvu ya Mungu. Wakasema, “Leo tumeona mambo ya kushangaza!”
Lawi (Mathayo) Amfuata Yesu
(Mt 9:9-13; Mk 2:13-17)
27Baada ya hayo Yesu alitoka nje akamwona mtoza ushuru amekaa sehemu yake ya kukusanyia ushuru. Jina lake aliitwa Lawi. Yesu akamwambia, “Nifuate!” 28Lawi akasimama, akaacha kila kitu na kumfuata Yesu.
29Lawi akaandaa chakula cha usiku nyumbani kwake kwa kumheshimu Yesu. Mezani walikuwepo watoza ushuru wengi na baadhi ya watu wengine. 30Lakini Mafarisayo na wale wanaofundisha sheria kwa ajili ya Mafarisayo wakaanza kulalamika kwa wafuasi wa Yesu wakisema, “Kwa nini mnakula na kunywa pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi wengine?”
31Yesu akawajibu, “Wagonjwa ndiyo wanaohitaji daktari, si wenye afya njema. 32Sikuja kuwaambia wenye haki wabadilike, bali wenye dhambi.”
Swali Kuhusu Kufunga
(Mt 9:14-17; Mk 2:18-22)
33Baadhi ya watu wakamwambia Yesu, “Wafuasi wa Yohana hufunga na kuomba mara kwa mara, vivyo hivyo wafuasi wa Mafarisayo. Lakini wafuasi wako hula na kunywa kila wakati.”
34Yesu akawaambia, “Kwenye harusi huwezi kuwaambia rafiki wa bwana harusi wafunge wakati bwana harusi bado yuko pamoja nao. 35Lakini muda ukifika na bwana harusi akaondolewa kwao. Watakuwa na huzuni, na watafunga.”
36Yesu akawaambia mfano huu: “Hakuna anayekata kiraka kwenye vazi jipya na kukishona kwenye vazi la zamani. Ataharibu vazi jipya, na kiraka kutoka vazi jipya hakitakuwa sawa na vazi la zamani. 37Pia hakuna mtu anayeweka divai mpya#5:37 divai mpya Maji ya zabibu ambayo ndiyo yanaanza kuchachuka na hutengeneza mgandamizo ndani ya chombo kilichofungwa. katika viriba vya zamani. Divai mpya itavipasua, divai itamwagika, na viriba vitaharibika. 38Daima mnaweka divai mpya kwenye viriba vipya. 39Hakuna mtu ambaye baada ya kunywa divai ya zamani hutaka divai mpya. Kwa sababu husema, ‘Divai ya zamani ni nzuri.’”
Iliyochaguliwa sasa
Luka 5: TKU
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Toleo la Awali
© 2017 Bible League International