Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 8

8
Yesu Akiwa Galilaya
1Siku iliyofuata, Yesu alisafiri kupitia katika baadhi ya miji na vijiji. Yesu aliwahubiri watu Habari Njema kuhusu ufalme wa Mungu. Mitume kumi na wawili walikuwa pamoja naye. 2Walikuwepo pia baadhi ya wanawake ambao Yesu aliwaponya magonjwa na pepo wabaya. Mmoja wao alikuwa Mariamu aitwaye Magdalena ambaye alitokwa na pepo saba; 3Pia pamoja na wanawake hawa alikuwepo Yoana mke wa Kuza (msimamizi wa mali za Herode), Susana, na wanawake wengine wengi. Wanawake hawa walitumia fedha zao kuwahudumia Yesu na mitume wake.
Simulizi Kuhusu Mkulima Aliyepanda Mbegu
(Mt 13:1-17; Mk 4:1-12)
4Kundi kubwa la watu lilikusanyika. Watu walimjia Yesu kutoka katika kila mji, naye Yesu akawaambia fumbo hili:
5“Mkulima alikwenda kupanda mbegu. Alipokuwa akizitawanya, baadhi zilianguka kandokando ya njia. Watu wakazikanyaga, na ndege wa angani wakazila. 6Zingine zikaanguka kwenye udongo wenye mawe. Zilipoanza kukua zikafa kwa sababu ya kukosa maji. 7Mbegu zingine ziliangukia kwenye miiba. Miiba ikakua pamoja nazo, miiba ikazisongasonga na hazikukua. 8Zilizosalia ziliangukia kwenye udongo mzuri wenye rutuba. Mbegu hizi zikaota na kuzaa kila moja mia.”
Yesu akamalizia fumbo. Kisha akapaza sauti, akasema, “Ninyi watu mnaonisikia, sikilizeni!”
9Wafuasi wake wakamwuliza, “Fumbo hili linamaanisha nini?”
10Akasema, “Mmechaguliwa kujua kweli za siri kuhusu ufalme wa Mungu. Lakini ninatumia mafumbo kuzungungumza na watu wengine. Ninafanya hivi ili,
‘Watazame,
lakini wasiweze kuona.
Wasikia,
lakini wasielewe.’#Isa 6:9
Yesu Afafanua Simulizi Kuhusu Mbegu
(Mt 13:18-23; Mk 4:13-20)
11Hii ndiyo maana ya fumbo hili: Mbegu ni Neno la Mungu. 12Watu wengine ni kama mbegu zilizoanguka njiani. Husikia mafundisho ya Mungu, lakini Shetani huja na kuwafanya waache kuyatafakari. Hii huwafanya kutoamini na kuokoka. 13Wengine wanafanana na mbegu zilizoanguka kwenye udongo wenye mawe. Ni watu ambao huyasikia mafundisho ya Mungu na kuyapokea kwa furaha, lakini kwa kuwa hawana mizizi yenye kina, huamini kwa muda mfupi. Majaribu yanapokuja, humwacha Mungu.
14Zilizoanguka katika miiba, zinafanana na watu wanaoyasikia Mafundisho ya Mungu, lakini wanaruhusu wasiwasi, mali na anasa za maisha haya kuwasimamisha na hawaendelei kukua. Hivyo mafundisho hayazalishi matokeo mazuri katika maisha yao.#8:14 hayazalishi matokeo mazuri … yao Hayazalishi matokeo mazuri katika maisha yao ina maana ya, “kukua kiroho”, ama watu hawa hawafanyi mambo mazuri ambayo Mungu anataka wayafanye. 15Na zile zilizoangukia katika udongo mzuri, ni wale ambao huyasikia mafundisho ya Mungu kwa moyo safi na mnyoofu. Huyatii na kwa uvumilivu wao huzaa mazao mazuri.
Zingatieni Nuru
(Mk 4:21-25)
16Hakuna mtu anayewasha taa na kuifunika kwa bakuli au kuificha uvunguni mwa kitanda. Badala yake huiweka kwenye kinara cha taa mahali palipo wazi, ili wanaoingia ndani wapate nuru ya kuwawezesha kuona. 17Kila jambo lililofichwa litawekwa wazi na kila siri itajulikana na kila mtu ataiona. 18Hivyo yatafakarini kwa umakini yale mnayosikia. Watu wenye uelewa kiasi watapokea zaidi. Lakini wale wasio na uelewa watapoteza hata ule wanaodhani kuwa wanao.”
Wafuasi wa Yesu ni Familia Yake Halisi
(Mt 12:46-50; Mk 3:31-35)
19Mama yake Yesu na wadogo zake wakaenda kumwona, lakini walishindwa kumfikia kwa sababu walikuwepo watu wengi sana. 20Mtu mmoja akamwambia Yesu, “Mama yako na wadogo zako wamesimama nje. Wanataka kukuona.”
21Yesu akawajibu “Mama yangu na wadogo zangu ni wale wanaolisikia na kulitii Neno la Mungu.”
Yesu Atuliza Dhoruba
(Mt 8:23-27; Mk 4:35-41)
22Siku moja Yesu na wafuasi wake walipanda mashua. Akawaambia, “Tuvuke mpaka upande mwingine wa ziwa.” Wakaanza safari kuvuka ziwa. 23Walipokuwa wanasafiri, Yesu alisinzia. Tufani kubwa ikalikumba ziwa na mashua ikaanza kujaa maji, wakawa katika hatari. 24Wafuasi wakamwendea, wakamwamsha, wakasema, “Mkuu, mkuu, tutazama!”
Yesu akasimama, akaukemea upepo na mawimbi ya maji. Upepo ukakoma na ziwa likatulia. 25Ndipo Yesu akawaambia wafuasi wake, “Imani yenu iko wapi?”
Lakini wao waliogopa na kustaajabu, wakanong'onezana, “Huyu ni mtu wa namna gani? Anaamuru upepo na maji, na vinamtii?”
Yesu Amweka Huru Mtu Kutoka Pepo Wachafu
(Mt 8:28-34; Mk 5:1-20)
26Yesu na wafuasi wake wakasafiri mpaka katika nchi walimoishi Wagerasi#8:26 Wagerasi Nakala zingine za Kiyunani zina “Wagadarini” na zingine zimewaita “Wagergesini”. iliyokuwa ng'ambo ya ziwa Galilaya. 27Yesu alipotoka katika mashua, mwanaume mmoja kutoka katika mji ule alimwendea. Mtu huyu alikuwa na mapepo ndani yake. Kwa muda mrefu hakuwahi kuvaa nguo na aliishi makaburini.
28-29Pepo aliyekuwa ndani yake alikuwa akimpagaa mara nyingi na alikuwa akifungwa gerezani, mikono na miguu yake ikiwa imefungwa kwa minyororo. Lakini kila mara aliivunja. Pepo ndani yake alikuwa anamlazimisha kwenda nje ya mji mahali pasipoishi watu. Yesu alimwamuru kumtoka mtu yule. Alipomwona Yesu, alianguka mbele yake huku akipiga kelele kwa sauti, “Unataka nini kwangu, Yesu, Mwana wa Mungu Mkuu Aliye Juu? Tafadhali usiniadhibu!”
30Yesu akamwuliza, “Jina lako nani?”
Mtu yule akajibu, “Jeshi.”#8:30 Jeshi Jina hili lina maana nyingi sana. Jina hili lina maana “wengi zaidi” Ni neno lililotumika kwa kundi la wanajeshi 6,000 wa Jeshi la Kirumi. (Alisema jina lake ni “Jeshi” kwa sababu pepo wengi walikuwa wamemwingia.) 31Pepo wale wakamsihi Yesu asiwaamuru kwenda shimoni.#8:31 shimoni Hii ina maana kuwa ni shimo lisilo na mwisho. Ni kama shimo refu ambalo mapepo hukaa (kuzimu). 32Katika kilima kile, kulikuwa kundi kubwa la nguruwe wakichungwa. Pepo wakamsihi Yesu awaruhusu wawaingie wale nguruwe. Hivyo Yesu akawaruhusu. 33Pepo wakamtoka yule mtu, na kuwaingia nguruwe. Kundi lote la wale nguruwe likakimbia kutelemkia ziwani kwa kasi, nguruwe wakazama na kufia humo.
34Wachungaji wa nguruwe walipoona lililotokea, walikimbia, wakaenda kutoa taarifa mjini na mashambani. 35Watu wakaenda kuona lililotokea. Walipofika alipokuwa Yesu wakamwona mtu yule aliyetokwa na pepo ameketi karibu na Yesu, amevaa nguo, akiwa na akili zake timamu; pepo walikuwa wamemtoka. Jambo hili likawaogopesha watu. 36Wale walioona mambo haya yalivyotokea waliwaambia wengine namna Yesu alivyomponya yule mtu. 37Watu wote waliokuwa wakiishi eneo lote la Gerasi wakamtaka Yesu aondoke kwa sababu waliogopa.
Hivyo Yesu akapanda mashua na kurudi Galilaya. 38Mtu aliyeponywa alimsihi amfuate Yesu. Lakini Yesu akamtuma, akamwambia, 39“Rudi nyumbani, ukawaeleze watu mambo ambayo Mungu amekutendea.”
Hivyo mtu yule alikwenda sehemu zote za mji akieleza mambo ambayo Yesu amemtendea.
Yesu Anampa Uhai Msichana Aliyekufa na Kumponya Mwanamke Mgonjwa
(Mt 9:18-26; Mk 5:21-43)
40Yesu aliporudi Galilaya, watu walimkaribisha. Kila mtu alikuwa anamsubiri. 41-42Mtu mmoja jina lake Yairo, aliyekuwa mkuu wa sinagogi alimwendea. Alikuwa na binti mmoja tu mwenye umri wa miaka kumi na mbili na alikuwa mgonjwa sana katika hali ya kufa. Hivyo Yairo alisujudu miguuni pa Yesu na akamsihi aende nyumbani kwake.
Yesu alipokuwa akienda nyumbani kwa Yairo, watu walimzonga kila upande. 43Mwanamke aliyekuwa akitokwa damu kwa miaka kumi na mbili alikuwepo katika umati huo. Alikuwa ametumia mali zake zote kwa madaktari,#8:43 Alikuwa ametumia … madaktari Nakala zingine za Kiyunani hazina maneno haya. lakini hakuna daktari aliyeweza kumponya. 44Alikwenda nyuma ya Yesu na kugusa pembe ya vazi lake. Wakati huo huo damu ikaacha kumtoka. 45Ndipo Yesu akasema, “Nani amenigusa?”
Kila mtu alikataa kuwa hajamgusa, Petro akasema, “Mkuu, watu wamekuzunguka na wanakuzongazonga kila upande.”
46Lakini Yesu akasema, “Kuna mtu amenigusa. Nimesikia nguvu ikinitoka.” 47Yule mwanamke alipoona ya kwamba hataweza kujificha akajitokeza akitetemeka. Akasujudu mbele ya Yesu. Huku kila mmoja akisikia, akaeleza sababu iliyomfanya amguse, na kwamba alipona wakati ule ule alipomgusa. 48Yesu alimwambia, “Binti yangu umeponywa kwa sababu uliamini. Nenda kwa amani.”
49Yesu alipokuwa bado anaongea, mtu mmoja kutoka nyumbani kwa yule mkuu wa sinagogi alikuja na akasema, “Binti yako amekwisha kufa! Hakuna haja ya kuendelea kumsumbua Mwalimu.”
50Yesu aliposikia maneno hayo, alimwambia Yairo, “Usiogope! Amini tu na binti yako ataponywa.”
51Yesu akaenda nyumbani, alipofika akaruhusu Petro, Yohana, Yakobo pamoja na baba na mama wa yule mtoto tu kuingia ndani pamoja naye. 52Kila mtu alikuwa akilia na kusikia huzuni kwa sababu msichana alikuwa amekufa. Lakini Yesu akasema, “Msilie. Hajafa. Amelala usingizi tu.”
53Watu wakamcheka, kwa sababu walijua kuwa amekwisha kufa. 54Lakini Yesu akamshika mkono na kumwambia, “Mtoto inuka!” 55Roho yake ikamrudia, akasimama hapo hapo. Yesu akasema, “Mpeni chakula.” 56Wazazi wa yule binti wakashangaa. Yesu akawakataza wasimwambie mtu yeyote lililotokea.

Iliyochaguliwa sasa

Luka 8: TKU

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia