Mathayo 24
24
Yesu Aonya Kuhusu Wakati Ujao
(Mk 13:1-31; Lk 21:5-33)
1Yesu alipokuwa anaondoka eneo la Hekalu, wanafunzi wake walimwendea na kumwonyesha majengo ya Hekalu. 2Akawauliza, “Mnayaona majengo haya? Ukweli ni kuwa, yataharibiwa. Kila jiwe litadondoshwa chini, hakuna jiwe litakaloachwa juu ya jiwe jingine.”
3Baadaye, Yesu alipokuwa ameketi mahali fulani katika Mlima wa Mizeituni, Wafuasi wake walimwendea faraghani. Wakasema, “Twambie mambo haya yatatokea lini. Na nini kitatokea ili kutuandaa kwa ajili ya ujio wako na mwisho wa nyakati?”
4Yesu akajibu, “Mjihadhari! Msimruhusu mtu yeyote awadanganye. 5Watu wengi watakuja na watatumia jina langu. Watasema, ‘Mimi ndiye Masihi.’ Na watawadanganya watu wengi. 6Mtasikia kuhusu vita vinanavyopiganwa na pia matetesi ya kuwapo vita vingine. Lakini msiogope. Mambo haya lazima yatokee na mwisho wenyewe hautafuata palepale. 7Mataifa yatapigana na mataifa mengine. Falme zitapigana na falme zingine. Utakuwepo wakati wa njaa ambapo watu watakosa chakula. Na kutakuwa matetemeko ya ardhi sehemu mbalimbali. 8Mambo haya ni mwanzo wa matatizo, kama uchungu wa kwanza mwanamke anapozaa.
9Kisha mtakamatwa na kupelekwa kwa wenye mamlaka ili mhukumiwe na kuuawa. Watu wote katika ulimwengu watawachukia kwa sababu mnaniamini mimi. 10Nyakati hizo watu wengi wataacha kuwa wafuasi wangu. Watasalitiana na kuchukiana. 11Manabii wengi watatokea na kusababisha watu wengi kuamini mambo yasiyo ya kweli. 12Kutakuwepo na uovu mwingi sana duniani kiasi kwamba upendo wa waaminio wengi utapoa. 13Lakini yeyote yule atakayekuwa mwaminifu mpaka mwisho ataokolewa. 14Na Habari Njema niliyoihubiri kuhusu Ufalme wa Mungu itahubiriwa ulimwenguni kote. Itatawanywa katika kila taifa. Kisha mwisho utakuja.
15Nabii Danieli alizungumza kuhusu ‘jambo la kutisha litakalosababisha uharibifu.’#24:15 jambo … uharibifu Tazama Dan 9:27; 12:11 (pia Dan 11:31). Mtakapoliona jambo hili la kutisha limesimama patakatifu.” (Asomaye hili anapaswa kuelewa jambo hili linamaanisha nini.) 16“Watu walio Uyahudi wakimbilie milimani. 17Wakimbie pasipo kupoteza muda ili kuchukua kitu chochote. Wakiwa darini wasiteremke ili kuchukua kitu na kukitoa nje ya nyumba. 18Wakiwa shambani wasirudi nyumbani kuchukua koti.
19Itakuwa hali ngumu kwa wanawake wenye mimba na wenye watoto wachanga! 20Ombeni isiwe majira ya baridi au isiwe siku ya Sabato mambo haya yatakapotokea na mkalazimika kukimbia, 21kwa sababu utakuwa wakati wa dhiki kuu. Kutakuwepo na usumbufu mwingi sana kuliko ule uliowahi kutokea tangu mwanzo wa ulimwengu. Na hakuna jambo baya kama hilo litakalotokea tena.
22Lakini Mungu amekwisha amua kuufupisha wakati huo. Ikiwa usingefupishwa, hakuna ambaye angeendelea kuishi. Lakini Mungu ataufupisha ili kuwasaidia watu aliowachagua.
23Wakati huo watu wataweza kuwaambia, ‘Tazama, Masihi yuko kule!’ Au wakasema, ‘Ni yule!’ Msiwaamini. 24Manabii wa uongo na masihi wa uongo watatokea na kufanya miujiza na maajabu#24:24 miujiza na maajabu Hapa ina maana ya kazi za ajabu zinazofanywa kwa kutumia nguvu za Shetani. makuu, ili ikiwezekana wawadanganye wateule. 25Na sasa nimewatahadharisha kuhusu hili kabla halijatokea.
26Inawezekana mtaambiwa, ‘Masihi yuko jangwani!’ Msiende jangwani kumtafuta. Mtu mwingine anaweza akasema, ‘Masihi yuko katika chumba kile!’ Msiamini. 27Mwana wa Adamu atakapokuja, kila mtu atamwona. Itakuwa kama radi inavyowaka angani na kuonekana kila mahali. 28Ni kama kutafuta mzoga: Mzoga hupatikana mahali ambapo tai wengi wamekusanyika.
Yesu Atakaporudi Tena
(Mk 13:24-27; Lk 21:25-28)
29Mara baada ya mateso ya siku hizo, mambo haya yatatokea:
‘Jua litakuwa jeusi,
na mwezi hautatoa mwanga.
Nyota zitaanguka kutoka angani,
na kila kitu kilicho angani
kitatikiswa kutoka mahali pake.’#24:29 Tazama Isa 13:10; 34:4.
30Kisha kutatokea ishara angani kuwa Mwana wa Adamu anakuja. Watu wote wa ulimwengu watajipiga kifuani wakiomboleza. Kila mtu atamwona Mwana wa Adamu akija katika mawingu ya angani akiwa na nguvu na utukufu mkuu. 31Naye atatumia parapanda kuu kuwatuma malaika zake kila mahali duniani. Nao watawakusanya wateule wake kutoka mwisho mmoja wa mbingu hadi mwingine.
32Jifunze kwa mtini: Matawi yake yanapokuwa ya kijani na laini na kuanza kutoa majani mapya, ndipo mnatambua kuwa majira ya joto yamekaribia. 33Katika namna hiyo hiyo, mtakapoona mambo haya yote yakitokea, mtajua kuwa wakati#24:33 wakati Wakati ambao Yesu aliuzungumzia ni ule ambapo kitu muhimu kitatokea. Tazama Lk 21:31, pale ambapo Yesu anasema huu ni wakati wa Ufalme wa Mungu kutufikia. umekaribia wa kile kitakachotokea. 34Ninawahakikishia kuwa mambo haya yote yatatokea wakati ambao baadhi ya watu wa nyakati hizi wakiwa bado hai. 35Ulimwengu wote, dunia na anga vitaangamizwa, lakini maneno yangu yatadumu milele.
Mungu Peke Yake Ndiye Ajuaye Siku ya Kurudi kwa Mwana wa Adamu
(Mk 13:32,35; Lk 17:26-30,34-36)
36Hakuna anayeijua siku wala wakati. Malaika wa mbinguni hawaijui hata Mwana hajui itakuwa lini. Baba peke yake ndiye anayejua.
37Mwana wa Adamu atakapokuja, itakuwa kama ilivyokuwa nyakati za Nuhu. 38Siku zile kabla ya gharika, watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuwatoa binti zao kuolewa mpaka siku ambayo Nuhu aliingia kwenye safina. 39Hawakujua juu ya kilichokuwa kinaendelea mpaka mafuriko yalipowajia na kuwaangamiza wote.
Ndiyo itakavyokuwa Mwana wa Adamu atakapokuja. 40Wanaume wawili watakuwa wakifanya kazi shambani, mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa. 41Wanawake wawili watakuwa wanasaga nafaka pamoja, mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.
42Hivyo iweni tayari daima. Hamjui siku ambayo Bwana wenu atarudi. 43Mwenye nyumba angefanya nini ikiwa angejua wakati ambao mwizi atakuja? Mnajua angelikesha ili mwizi asivunje na kuingia. 44Hivyo, ninyi nanyi iweni tayari. Mwana wa Adamu atakuja katika wakati msiomtarajia.
Watumishi Wema na Wabaya
(Mk 13:33-37; Lk 12:41-48)
45Fikiria mtumishi aliyewekwa na bwana wake kuwapa chakula watumishi wake wengine katika muda uliopangwa. Ni kwa namna gani mtumishi huyo atajionyesha kuwa ni mwangalifu na mwaminifu? 46Bwana wake atakaporudi na kumkuta anafanya kazi aliyompa, siku hiyo itakuwa siku ya furaha kwa mtumishi huyo. 47Ninawaambia bila mashaka yoyote kuwa, bwana wake atamchagua mtumishi huyo awe msimamizi wa kila kitu anachomiliki yule Bwana.
48Lakini nini kitatokea ikiwa mtumishi huyo ni mbaya na akadhani kuwa bwana wake hatarudi karibuni? 49Ataanza kuwapiga watumishi wengine na kuanza kunywa na kula na walevi. 50Ndipo bwana wake atakuja wakati asioutarajia, ambapo mtumishi hakujiandaa. 51Bwana atamwadhibu mtumishi huyo na kumpeleka anakostahili kuwapo pamoja na watumishi wengine waliojifanya kuwa wema. Huko watalia na kusaga meno kwa maumivu.
Iliyochaguliwa sasa
Mathayo 24: TKU
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Toleo la Awali
© 2017 Bible League International