Marko 16
16
Yesu Amefufuka Kutoka Mauti
(Mt 28:1-8; Lk 24:1-12; Yh 20:1-10)
1Sabato ilipomalizika, Mariamu Magdalena, Maria mama yake Yakobo, na Salome wakanunua manukato yenye harufu nzuri ili kuyapaka kwenye mwili wa Yesu. 2Alfajiri na mapema Jumapili, mara tu baada ya jua kuchomoza, walienda kwenye kaburi la Yesu. 3Nao walikuwa wakiambiana wao kwa wao, ni nani atakayelivingirisha jiwe litoke katika mlango wa kaburi kwa ajili yetu?
4Kisha wakatazama juu na wakaona kuwa jiwe lile kubwa lilikuwa limevingirishwa tayari litoke mlangoni mwa kaburi la Yesu. 5Walipoingia kaburini, wakamwona kijana mmoja ameketi upande wa kulia naye alikuwa amevaa vazi jeupe, nao wakastaajabu.
6Naye akamwambia, “Usistaajabu. Unamtafuta Yesu wa Nazareti, aliyesulubiwa? Tazama amefufuka! Hayupo hapa. Angalieni mahali walipokuwa wameweka mwili wake. 7Hata hivyo nendeni na kuwaeleza wafuasi wake pamoja na Petro kwamba: ‘Ametangulia mbele yenu kuelekea Galilaya. Mtamkuta kule, kama alivyowaambia.’”
8Kwa hiyo wale wanawake walitoka na kukimbia kutoka kaburini, kwa sababu hofu na mshangao ulikuwa umewajia. Nao hawakusema chochote kwa mtu yeyote kwani waliogopa.#16:8 Kitabu kinaishia hapa katika nakala mbili za zamani za Kiyunani zilizopatikana. Nakala chache nyingine za baadaye zina mwisho huu mfupi: “Lakini mara wakampa maagizo yote Petro na wale waliokuwa pamoja naye. Kisha Yesu mwenyewe akawatuma watoke na kwenda mashariki na magharibi wakiwa na ujumbe mtakatifu ambao kamwe hautabadilika; kwamba watu wataokolewa milele.”
Yesu Awatokea Wafuasi Wake
(Mt 28:9-10,16-20; Lk 24:13-49; Yh 20:11-23; Mdo 1:6-8)
9Baada ya Yesu kufufuka alfajiri na mapema siku ya Jumapili, alimtokea kwanza Maria Magdalena, ambaye awali alifukuza mashetani saba kutoka kwake. 10Baada ya Mariamu kumwona Yesu, alienda na kuwaeleza wanafunzi wake. Walikuwa wamehuzunishwa sana na walikuwa wakilia. 11Lakini Mariamu aliwaambia kwamba Yesu yu hai. Aliwaambia ya kwamba yeye amemwona, lakini wao hawakumwamini.
12Baada ya hayo, Yesu kwa namna tofauti akawatokea wanafunzi wake wawili walipokuwa wakitembea kuelekea mashambani. 13Hawa kisha walirudi na wakawasimulia wengine wote, lakini nao hawakuwaamini.
14Baadaye, Yesu aliwatokea wale mitume kumi na mmoja walipokuwa wakila. Naye akawakaripia kwa kutokuwa na imani. Walikuwa wakaidi na walikataa kuwaamini wale waliomwona Yesu baada ya kufufuka kwake.
15Naye akawaambia, “Nendeni ulimwenguni pote, na mkahubiri Habari Njema kwa uumbaji wote. 16Yeyote atakayeamini na kubatizwa ataokolewa, lakini yeyote asiyeamini atahukumiwa. 17Na wale waaminio wataweza kufanya ishara hizi kama uthibitisho: watafukuza mashetani kwa jina langu; watasema kwa lugha mpya wasizojifunza bado; 18watakamata nyoka kwa mikono yao; na ikiwa watakunywa sumu yoyote, haitawadhuru; wataweka mikono yao kwa wagonjwa, nao watapona.”
Yesu Arudi Mbinguni
(Lk 24:50-53; Mdo 1:9-11)
19Hivyo baada ya Bwana Yesu kuzungumza nao, alichukuliwa mbinguni, kuketi katika mkono wa kuume wa Mungu. 20Na mitume wakatoka na kwenda kuhubiri kila mahali, na Bwana alifanya kazi pamoja nao akithibitisha kuwa ujumbe wao ni wa kweli kwa ishara zilizofuatana na mahubiri yao.
Iliyochaguliwa sasa
Marko 16: TKU
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Toleo la Awali
© 2017 Bible League International