Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Marko 3

3
Yesu Amponya Mtu Siku ya Sabato
(Mt 12:9-14; Lk 6:6-11)
1Kwa mara nyingine tena Yesu alikwenda kwenye sinagogi. Huko alikuwepo mtu aliyekuwa na mkono uliolemaa. 2Watu wengine walikuwa wakimwangalia Yesu kwa karibu sana. Walitaka kuona ikiwa angemponya mtu yule siku ya Sabato,#3:2 Walitaka … siku ya Sabato Haikuruhusiwa kwa Wayahudi kufanya kazi siku ya Sabato na wengi waliamini kumponya mtu ambaye hakuwa katika hatari ya kufa ilikuwa ni kazi. ili wapate sababu ya kumshitaki. 3Yesu akamwambia yule mtu aliyekuwa na mkono uliolemaa, “Simama mbele ili kila mtu akuone.”
4Ndipo Yesu akawaambia, “Je! ni halali kutenda mema ama kutenda mabaya siku ya Sabato? Je! ni halali kuyaokoa maisha ya mtu fulani ama kuyapoteza?” Lakini wao walikaa kimya.
5Yesu akawatazama wote waliomzunguka kwa hasira lakini alihuzunika kwa sababu waliifanya mioyo yao kuwa migumu. Akamwambia mtu yule “nyosha mkono wako”, naye akaunyosha, na mkono wake ukapona. 6Kisha Mafarisayo wakaondoka na papo hapo wakaanza kupanga njama pamoja na Maherode kinyume cha Yesu kutafuta jinsi gani wanaweza kumuua.
Wengi Wamfuata Yesu
7Yesu akaondoka pamoja na wanafunzi wake hadi Ziwa Galilaya, na kundi kubwa la watu kutoka Galilaya likawafuata, pamoja na watu kutoka Uyahudi, 8Yerusalemu, Idumea, na katika maeneo yote ng'ambo ya Mto Yordani na yale yanayozunguka Tiro na Sidoni. Lilikuwa kundi kubwa sana la watu. Wote walimjia Yesu kwa sababu walikuwa wamesikia mambo aliyokuwa anafanya.
9Kwa sababu ya kundi, aliwaambia wanafunzi wake, kumtayarishia mashua mdogo, ili kwamba wasiweze kumsonga na kumbana. 10Yesu alikuwa ameponya watu wengi. Hivyo wote wale waliokuwa na magonjwa waliendelea kujisogeza mbele kumwelekea ili wamguse. 11Kila mara pepo wachafu walipomwona Yesu, walianguka chini mbele yake, na kulia kwa sauti, “Wewe ni Mwana wa Mungu!” 12Lakini yeye aliwaamuru kila mara wasimwambie mtu yeyote yeye ni nani.
Yesu Achagua Wanafunzi Wake Kumi na Wawili
(Mt 10:1-4; Lk 6:12-16)
13Kisha Yesu akapanda juu kwenye vilima na akawaita baadhi ya wanafunzi wake, hasa wale aliowataka wajiunge naye pale. 14Akawachagua kumi na wawili, ambao aliwaita mitume. Aliwachagua ili waambatane pamoja naye, na kwamba aweze kuwatuma sehemu mbalimbali kuhubiri ujumbe wa neno la Mungu. 15Pia aliwapa mamlaka ya kufukuza mashetani toka kwa watu. 16Yafuatayo ni majina ya mitume kumi na wawili aliowateuwa Yesu:
Simoni ambaye Yesu alimwita Petro,
17Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohana ndugu yake (ambao wote Yesu aliwaita Boanergesi), yaani “wana wa ngurumo yenye radi”,
18Andrea,
Filipo,
Bartholomayo,
Mathayo,
Thomaso,
Yakobo mwana wa Alfayo,
Thadayo,
Simoni Mzelote
19na Yuda Iskariote,#3:19 Iskariote Yaweza kuwa “kutoka Kirioti”, mji kusini mwa Yuda. ambaye ndiye aliyemsaliti Yesu.
Nguvu ya Yesu Inatoka kwa Mungu
(Mt 12:22-32; Lk 11:14-23; 12:10)
20Kisha Yesu akaenda nyumbani. Kwa mara nyingine tena umati wa watu ukakusanyika, kiasi kwamba Yesu na wanafunzi wake hawakupata nafasi ya kula. 21Familia ya Yesu ilipoyasikia haya, walikwenda kumchukua kwa sababu watu walisema amerukwa na akili.
22Walimu wa Sheria waliokuwa wametoka Yerusalemu walikuwa wanasema, “Yeye ana Beelzebuli#3:22 Beelzebuli Kwa maana ya kawaida, “Shetani”. Jina hili limetumika badala ya lile la Shetani. ndani yake! Kwani anafukuza mashetani kwa nguvu ya mkuu wa mashetani!”
23Yesu akawaita na kuanza kuzungumza nao kwa kulinganisha: “Inawezekanaje Shetani ambaye ni roho mchafu kufukuza mashetani? 24Ikiwa basi ufalme utagawanyika katika sehemu mbili zinazopingana zenyewe kwa zenyewe, ufalme huo hautaendelea. 25Vivyo hivyo ufalme wa Shetani ukigawanyika naye akapigana dhidi ya pepo wake wabaya, basi huo utakuwa ndio mwisho wa ufalme wake. Pia ikiwa nyumba itapingana yenyewe kwa yenyewe, nyumba hiyo haitaweza kusalimika. 26Kwa hiyo ikiwa Shetani atajipinga mwenyewe na kugawanyika basi hataweza kuendelea na huo utakuwa mwisho wake.
27Hakika, hakuna anayeweza kuingia kwenye nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuzichukua mali zake bila kwanza kumfunga mtu huyo mwenye nguvu; hapo ndipo atakapoweza kuiba katika nyumba hiyo.
28Ninawaambia ukweli: Watu wanaweza kusamehewa dhambi zao zote na maneno yao yenye matusi kwa Mungu. 29Lakini yeyote atakayemtukana Roho Mtakatifu hatasamehewa kabisa. Kwa sababu mtu anayefanya hivyo atakuwa na hatia ya dhambi isiyosamehewa milele.”
30Yesu alisema haya kwa sababu walimu wa sheria walikuwa wanasema, “Yeye ana pepo mchafu ndani yake.”
Wafuasi wa Yesu ni Familia Yake Halisi
(Mt 12:46-50; Lk 8:19-21)
31Kisha mama yake Yesu na nduguze wakaja. Wao walisimama nje na wakamtuma mtu aende kumwita ndani. 32Humo lilikuwepo kundi lililoketi kumzunguka, lakini wao wakamwambia, “Tazama! Mama yako, kaka zako na dada zako wako#3:32 na dada zako wako Nakala zingine za Kiyunani hazina maneno haya. nje wanakusubiri.”
33Yesu akauliza, “Mama yangu ni nani na kaka zangu ni akina nani?” 34Yesu akawatazama wale walioketi kumzunguka na akasema “Hapa yupo mama yangu na wapo kaka zangu na dada zangu! 35Yeyote anayeyafanya mapenzi ya Mungu ndiye kaka yangu, dada yangu, na mama yangu.”

Iliyochaguliwa sasa

Marko 3: TKU

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia