Marko 5
5
Yesu Amweka Huru Mtu Kutoka Pepo Wachafu
(Mt 8:28-34; Lk 8:26-39)
1Wakafika ng'ambo ya ziwa, katika nchi walimoishi Wagerasi.#5:1 Wagerasi Nakala zingine za Kiyunani zina “Wagadarini” na zingine zimewaita “Wagergesini”. 2Yesu alipotoka katika mashua ile ghafla, mtu mmoja aliyekuwa na roho chafu alitoka makaburini kuja kumlaki. 3Mtu huyu aliishi makaburini, na hakuna mtu yeyote aliyeweza kumfunga hata kwa mnyororo, 4Watu walijaribu kila mara kumfunga kwa minyororo na vyuma kwenye miguu na mikono. Hata hivyo, aliweza kuivunja minyororo ile na pingu zile za vyuma wala hakuna aliyekuwa na nguvu za kutosha kumdhibiti. 5Kila mara usiku na mchana akiwa makaburini na kwenye milima alipiga kelele na kujikata kwa mawe.
6Alipomwona Yesu kutoka mbali, alimkimbilia, na kusujudu mbele yake. 7Kisha akalia kwa sauti kubwa na kusema, “Unataka nini kwangu, Yesu Mwana wa Mungu Aliye Mkuu zaidi? Nakuomba uape mbele za Mungu kwamba hutanitesa.” 8Yule pepo alisema haya kwa sababu Yesu alikuwa anamwambia, “Mtoke huyo mtu, ewe pepo mchafu!”
9Ndipo Yesu akamwuliza yule mtu, “Jina lako nani?”
Naye akamjibu, “Jina langu ni Jeshi,#5:9 Jeshi Jina hili lina maana nyingi sana. Jina hili lina maana “wengi zaidi” Ni neno lililotumika kwa kundi la wanajeshi 6,000 wa Jeshi la Kirumi. kwa sababu tuko wengi.” 10Yule pepo akamwomba Yesu tena na tena asiwaamuru kutoka katika eneo lile.
11Kulikuwepo kundi kubwa la nguruwe likila katika kilima. 12Wale pepo wakamwomba Yesu awatume waende katika lile kundi la nguruwe na kuliingia, 13Naye akawaruhusu. Kwa hiyo pepo wachafu walimtoka mtu yule na kuwaingia nguruwe.#5:13 nguruwe Watu kijijini walikuwa wakiwatunza nguruwe katika kundi moja kubwa. Kundi hilo lilikuwa chanzo muhimu cha mapato kwa kijiji. Kundi lile lilikuwa na idadi karibu ya elfu mbili, lilikimbia kuelekea kwenye kingo zenye mtelemko mkali na kutumbukia ziwani, ambamo walizama.
14Wale waliowachunga walikimbia. Wakatoa taarifa mjini na katika maeneo jirani ya mashambani. Watu wakaja kuona ni kitu gani kilichotokea. 15Watu hao wakamwendea Yesu. Nao wakamwona yule aliyekuwa na mashetani ameketi mahali pale, amevaa nguo na akiwa mwenye akili zake nzuri; huyu ni yule aliyekuwa amepagawa na jeshi la mashetani. Wakaogopa. 16Wale waliokuwa wameona hili waliwasimulia kile kilichomtokea mtu yule aliyekuwa amepagawa na mashetani na kuhusu nguruwe wale. 17Nao wakamwomba Yesu aondoke katika eneo lile.
18Wakati Yesu akipanda katika mtumbwi, mtu yule aliyekuwa amepagawa na mashetani alimwomba Yesu afuatane naye. 19Lakini Yesu hakumruhusu aende naye, isipokuwa alimwambia, “Nenda kwa watu wa kwenu, na uwaambie yote ambayo Bwana amekufanyia, na uwaambie jinsi alivyokuwa na huruma kwako.”
20Hivyo mtu yule aliondoka, na akaanza kuwaeleza watu katika Dekapoli#5:20 Dekapoli Eneo wanaloishi wasio Wayahudi mashariki mwa Galilaya inaloitwa pia Eneo la Miji Kumi. mambo mengi ambayo Yesu amemtendea, na watu wote walistaajabu.
Yesu Anampa Uhai Msichana Aliyekufa na Kumponya Mwanamke Mgonjwa
(Mt 9:18-26; Lk 8:40-56)
21Kisha, Yesu alivuka kurudi upande wa magharibi wa ziwa. Pale kundi kubwa la watu lilikusanyika kwake. Yeye alikuwa kando ya ziwa, na 22mmoja wa viongozi wa sinagogi, aliyeitwa Yairo, alifika pale. Naye alipomwona Yesu, alipiga magoti miguuni pake. 23Kisha akamwomba kwa msisitizo, akisema, “Binti yangu mdogo yu karibu kufa. Ninakuomba ufike na kumwekea mikono, ili kwamba apone na kuishi.”
24Hivyo Yesu alienda pamoja naye. Na kundi kubwa la watu lilimfuata; nao walikuwa wakimsonga pande zote kumzunguka.
25Alikuwepo mwanamke mmoja aliyekuwa akitoka damu (kama ilivyo desturi ya wanawake kila mwezi) kila siku kwa miaka kumi na miwili. 26Huyu alikuwa ameteseka sana akiwa chini ya uangalizi wa madaktari wengi. Yeye alikuwa ametumia vyote alivyokuwa navyo. Hata hivyo hali yake iliendelea kuwa mbaya zaidi.
27Wakati aliposikia juu ya Yesu, alimwendea kwa nyuma akiwa katika kundi lile na kuligusa joho lake. 28Kwani alikuwa akijisemea mwenyewe, “Ikiwa nitagusa tu vazi lake, nitapona.” 29Mara moja chanzo cha kutoka kwake damu kikakauka, na akajisikia mwilini mwake kwamba amepona matatizo yake. 30Naye Yesu akatambua mara moja kwamba nguvu zilimtoka. Aligeuka nyuma na kuuliza “Nani aliyegusa mavazi yangu?”
31Wanafunzi wake wakamwambia, “Uliliona kundi likisukumana kukuzunguka, nawe unauliza, Nani aliyenigusa?”
32Lakini Yesu aliendelea kuangalia kumzunguka kuona ni nani aliyeyafanya haya. 33Yule Mwanamke akiwa anatetemeka kwa hofu akijua nini kilichotokea kwake, alikuja na kuanguka mbele yake, akamweleza ukweli wote. 34Kisha Yesu akamwambia, “Binti yangu imani yako imekuponya. Nenda kwa amani, na uendelee kupona matatizo yako.”
35Wakati alipokuwa akizungumza haya watumishi walikuja kutoka nyumbani kwa afisa wa sinagogi. Nao wakamwambia yule afisa, “Binti yako amefariki kwa nini uendelee kumsumbua huyo mwalimu?”
36Lakini Yesu aliyasikia yale waliyokuwa wakisema, na akamwaambia yule afisa wa sinagogi, “Usiogope. Amini tu.”
37Naye hakumruhusu mtu yeyote kumfuata isipokuwa Petro, Yakobo na Yohana ndugu yake Yakobo, 38nao wakaenda katika nyumba ya yule afisa wa sinagogi, na Yesu akaona vurugu na watu wakilia kwa sauti. 39Yesu aliingia ndani na kuwaambia, “Za nini vurugu zote hizi na vilio hivi? Mtoto hajafa; amelala tu.” 40Nao wakamcheka.
Yeye aliwatoa nje watu wote, akamchukua baba na mama wa mtoto na wale waliokuwa pamoja naye, akaenda hadi pale alipokuwepo mtoto, 41akaushika mkono wa mtoto yule na kumwambia “Talitha koum!” (maana yake, “Msichana mdogo, ninakuambia amka usimame!”) 42Yule msichana aliinuka mara moja na kuanza kutembea mahali pale. Naye alikuwa na miaka kumi na miwili. Nao mara moja wakaelemewa na mshangao mkubwa. 43Yeye akawapa amri kuwa mtu yeyote asijue juu ya jambo hili. Kisha akawaambia wampatie msichana yule chakula ale.
Iliyochaguliwa sasa
Marko 5: TKU
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Toleo la Awali
© 2017 Bible League International