Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 5

5
Anania na Safira
1Lakini mtu mmoja jina lake Anania pamoja na mkewe Safira waliuza kiwanja. 2Huku mkewe akijua kikamilifu, Anania alificha sehemu ya fedha alizopata, akaleta kiasi kilichobaki na kukiweka miguuni pa mitume.
3Petro akamuuliza, “Anania, mbona Shetani ameujaza moyo wako ili kumwambia uongo Roho wa Mungu, ukaficha sehemu ya fedha ulizopata kutokana na kiwanja? 4Je, kabla hujauza hicho kiwanja, si kilikuwa mali yako? Hata baada ya kukiuza, je, fedha ulizozipata, si zilikuwa kwenye uwezo wako? Kwa nini basi umewaza hila hii moyoni mwako kufanya jambo kama hili? Wewe hukumwambia uongo mwanadamu, bali Mungu.”
5Anania aliposikia maneno haya akaanguka chini na kufa. Hofu kuu ikawapata wote waliosikia jambo lililokuwa limetukia. 6Vijana wakaja, wakaufunga mwili wake sanda, wakampeleka nje kumzika.
7Muda wa saa tatu baadaye, mkewe Anania akaingia, naye hana habari ya mambo yaliyotukia. 8Petro akamuuliza, “Niambie, je, mliuza kiwanja kwa thamani hii?” Akajibu, “Ndiyo, tuliuza kwa thamani hiyo.”
9Ndipo Petro akamwambia, “Imekuwaje mkakubaliana kumjaribu Roho wa Bwana Mungu Mwenyezi? Tazama! Nyayo za vijana waliomzika mumeo ziko mlangoni, wewe nawe watakupeleka nje.”
10Wakati ule ule, akaanguka chini miguuni mwake na kufa. Nao wale vijana wakaingia, wakamkuta amekufa, wakamchukua wakamzika kando ya mumewe. 11Hofu kuu ikalipata kundi la waumini wa Isa lote, pamoja na watu wote waliosikia kuhusu matukio haya.
Mitume waponya watu wengi
12Mitume walifanya ishara nyingi na miujiza miongoni mwa watu. Waumini wote walikuwa wakikusanyika katika Ukumbi wa Sulemani. 13Hakuna mtu mwingine aliyethubutu kuambatana nao, ijapokuwa waliheshimiwa sana na watu. 14Hata hivyo, waliomwamini Bwana Isa wakazidi kuongezeka, wanaume na wanawake. 15Hata wakawa wanawaleta wagonjwa na kuwalaza kwenye magodoro na kwenye vitanda barabarani ili yamkini Petro akipita kivuli chake kiwaguse baadhi yao. 16Pia watu wakakusanyika kutoka miji iliyokuwa karibu na Yerusalemu, wakileta wagonjwa na watu walioteswa na pepo wachafu. Hao wote wakaponywa.
Mitume washtakiwa
17Kisha kuhani mkuu na wenzake wote waliokuwa pamoja naye, waliokuwa wa kundi la Masadukayo#5:17 Kundi la kidini la Wayahudi; waliamini kwamba hakuna ufufuo, wala hakuna malaika au roho., wakajawa na wivu. 18Wakawakamata mitume na kuwafunga gerezani. 19Lakini wakati wa usiku, malaika wa Mwenyezi Mungu akaja, akafungua milango ya gereza na akawatoa nje. Akawaambia, 20“Nendeni, mkasimame Hekaluni, mkawaambie watu maneno yote ya maisha haya mapya.”
21Waliposikia haya wakaenda Hekaluni alfajiri wakaendelea kufundisha watu.
Kuhani mkuu na wale waliokuwa pamoja nao walipowasili, alikusanya Baraza la Wayahudi, yaani wazee wote wa Israeli. Wakatumana wale mitume waletwe kutoka gerezani. 22Lakini wale walinzi wa Hekalu walipoenda gerezani hawakuwakuta mitume mle. Kwa hiyo wakarudi na kutoa habari. 23Wakasema, “Tumekuta milango ya gereza imefungwa sawasawa na askari wa gereza wamesimama nje ya mlango, lakini tulipofungua milango hakuwepo mtu yeyote.” 24Basi mkuu wa walinzi wa Hekalu na viongozi wa makuhani waliposikia haya, wakafadhaika na kushangaa sana kwa ajili yao kwamba jambo hili litakuwaje.
25Ndipo mtu mmoja akaja akawaambia, “Tazameni watu mliowafunga gerezani wako Hekaluni wakiwafundisha watu.” 26Ndipo yule mkuu wa walinzi wa Hekalu wakaenda pamoja na askari wakawaleta wale mitume, lakini bila ghasia kwa sababu waliogopa kupigwa mawe na watu.
27Waliwaleta mitume, wakawasimamisha mbele ya Baraza la Wayahudi ili kuhani mkuu awahoji. 28“Tuliwaonya kwa nguvu msifundishe kwa jina hili, lakini ninyi mmeijaza Yerusalemu yote mafundisho yenu na tena mmekusudia kuleta damu ya mtu huyu juu yetu.”
29Petro na wale mitume wengine wakajibu, “Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu. 30Mungu wa baba zetu alimfufua Isa kutoka kwa wafu, ambaye ninyi mlimuua kwa kumtundika kwenye msalaba. 31Mungu alimtukuza, akamweka mkono wake wa kuume kuwa Kiongozi na Mwokozi ili awape Israeli toba na msamaha wa dhambi. 32Nasi tu mashahidi wa mambo haya, vivyo hivyo na Roho Mtakatifu wa Mungu ambaye Mungu amewapa wale wanaomtii.”
33Wale wajumbe wa Baraza la Wazee waliposikia haya, walijawa na ghadhabu, wakataka kuwaua mitume. 34Lakini Farisayo#5:34 Kundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli. mmoja, jina lake Gamalieli, aliyekuwa mwalimu wa Torati, aliyeheshimiwa na watu wote, akasimama mbele ya Baraza la Wayahudi, akaamuru mitume watolewe nje kwa muda. 35Ndipo alipowaambia wazee wa Baraza, “Enyi wanaume wa Israeli, fikirini kwa uangalifu mnayotaka kuwatendea watu hawa. 36Kwa maana wakati uliopita, aliinuka mtu mmoja jina lake Theuda, alijidai kuwa yeye ni mtu maarufu, akapata wafuasi wapatao mia nne walioambatana naye. Lakini aliuawa, na wafuasi wake wote wakatawanyika, wakawa si kitu. 37Baada yake, alitokea Yuda Mgalilaya wakati wa kuorodhesha watu, naye akaongoza kundi la watu kuasi. Yeye pia aliuawa, nao wafuasi wake wakatawanyika. 38Kwa hiyo, kwa habari ya jambo hili nawashauri, jiepusheni na watu hawa. Waachieni waende zao! Kwa maana kama kusudi lao na shughuli yao imetokana na mwanadamu, haitafanikiwa. 39Lakini ikiwa imetoka kwa Mungu, hamtaweza kuwazuia watu hawa. Badala yake mtajikuta mnapigana na Mungu.”
40Wakapokea ushauri wa Gamalieli. Wakawaita mitume ndani, wakaamuru wachapwe mijeledi, kisha wakawaagiza wasinene tena kwa jina la Isa, wakawaachia waende zao.
41Nao mitume wakatoka nje ya Baraza la Wayahudi, wakiwa wamejaa furaha kwa sababu wamehesabiwa kustahili kupata aibu kwa ajili ya jina la Isa. 42Kila siku, Hekaluni na nyumba kwa nyumba, hawakuacha kufundisha na kuhubiri Habari Njema kwamba Isa ndiye Al-Masihi#5:42 Al-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta..

Iliyochaguliwa sasa

Matendo 5: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia