Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 30

30
1Raheli alipoona hamzalii Yakobo watoto, akamwonea dada yake wivu. Hivyo akamwambia Yakobo, “Nipe watoto, la sivyo nitakufa!”
2Yakobo akamkasirikia, akamwambia, “Je, mimi ni badala ya Mungu, ambaye amekuzuia kuzaa watoto?”
3Ndipo Raheli akamwambia, “Hapa yupo Bilha, mjakazi wangu. Kutana naye kimwili ili aweze kunizalia watoto, na kupitia kwake mimi pia niweze kuwa na uzao.”
4Hivyo Raheli akampa Yakobo Bilha awe mke wake. Yakobo akakutana naye kimwili, 5naye Bilha akapata mimba, akamzalia Yakobo mwana. 6Ndipo Raheli akasema, “Mungu amenipa haki yangu; amesikiliza maombi yangu na kunipa mwana.” Kwa hiyo akamwita jina Dani#30:6 maana yake Anahukumu.
7Bilha mjakazi wa Raheli akapata mimba tena, akamzalia Yakobo mwana wa pili. 8Ndipo Raheli akasema, “Nilikuwa na mashindano makubwa na dada yangu, nami nimeshinda.” Kwa hiyo akamwita jina Naftali#30:8 maana yake Nimeshindana.
9Lea alipoona kuwa amekoma kuzaa watoto, alimchukua mjakazi wake Zilpa, naye akampa Yakobo awe mke wake. 10Zilpa mjakazi wa Lea akamzalia Yakobo mwana. 11Ndipo Lea akasema, “Hii ni bahati nzuri aje!” Kwa hiyo akamwita jina Gadi#30:11 maana yake Jeshi laja.
12Mjakazi wa Lea akamzalia Yakobo mwana wa pili. 13Ndipo Lea akasema, “Nina furaha kiasi gani! Wanawake wataniita furaha.” Kwa hiyo akamwita jina Asheri#30:13 maana yake Nimefurahi.
14Msimu wa kuvuna ngano, Reubeni akaenda shambani akachuma tunguja ambazo alizileta kwa Lea mama yake. Raheli akamwambia Lea, “Tafadhali nakuomba unipe baadhi ya tunguja za mwanao.”
15Lakini Lea akamwambia, “Haikukutosha kuninyang’anya mume wangu? Je, utachukua na tunguja za mwanangu pia?”
Raheli akasema, “Vema sana! Yakobo atakutana nawe kimwili leo usiku, kwa malipo ya tunguja za mwanao.”
16Kwa hiyo Yakobo alipokuja kutoka shambani jioni ile, Lea akaenda kumlaki, akamwambia, “Lazima ukutane nami kimwili. Nimekukodisha kwa tunguja za mwanangu.” Kwa hiyo akakutana naye kimwili usiku ule.
17Mungu akamsikiliza Lea, naye akapata mimba, akamzalia Yakobo mwana wa tano. 18Ndipo Lea akasema, “Mungu amenizawadia kwa kumpa mume wangu mjakazi wangu.” Kwa hiyo akamwita jina Isakari#30:18 maana yake Zawadi.
19Lea akapata mimba tena, akamzalia Yakobo mwana wa sita. 20Ndipo Lea aliposema, “Mungu amenizawadia kwa zawadi ya thamani sana. Sasa mume wangu ataniheshimu kwa sababu nimemzalia wana sita.” Kwa hiyo akamwita jina Zabuloni#30:20 maana yake Heshima.
21Baadaye akamzaa mtoto wa kike, akamwita jina Dina#30:21 maana yake Tetea haki.
22Ndipo Mungu akamkumbuka Raheli, akasikia maombi yake na akafungua tumbo lake. 23Akapata mimba na akamzaa mwana; akasema, “Mungu ameniondolea aibu yangu.”
24Akamwita jina Yusufu#30:24 maana yake Yeye na aongeze, akasema, “Mwenyezi Mungu na anipe mwana mwingine.”
Makundi ya Yakobo yaongezeka
25Baada ya Raheli kumzaa Yusufu, Yakobo akamwambia Labani, “Nipe ruhusa nirudi katika nchi yangu. 26Nipe wake zangu na watoto, ambao nimetumika kuwapata, nami niende zangu. Unajua kazi niliyokufanyia.”
27Lakini Labani akamwambia, “Ikiwa nimepata kibali machoni pako, tafadhali ukae. Nimegundua kwa uaguzi kwamba Mwenyezi Mungu amenibariki kwa sababu yako.” 28Akaongeza kumwambia, “Taja ujira wako nami nitakulipa.”
29Yakobo akamwambia, “Unajua jinsi nimekutumikia na jinsi wanyama wako walivyolishwa vizuri chini ya uangalizi wangu. 30Kidogo ulichokuwa nacho kabla sijaja kimeongezeka sana, naye Mwenyezi Mungu amekubariki popote nilipokuwa. Lakini sasa, ni lini nitashughulikia mambo ya nyumba yangu mwenyewe?”
31Labani akamuuliza, “Nikupe nini?”
Yakobo akamjibu, “Usinipe chochote, lakini kama utanifanyia jambo hili moja, nitaendelea kuchunga na kuyaangalia makundi yako. 32Niruhusu nipite katika makundi yako yote leo niondoe humo kila kondoo mwenye mabaka mabaka au madoadoa, kila mwana-kondoo mweusi, na kila mbuzi mwenye madoadoa au mabaka mabaka. Hawa watakuwa ujira wangu. 33Uadilifu wangu utanishuhudia siku zijazo, kila utakapochunguza ujira ambao umenilipa mimi. Mbuzi yeyote wangu ambaye hana mabaka mabaka wala madoadoa, au mwana-kondoo ambaye si mweusi, atahesabika ameibwa.”
34Labani akasema, “Ninakubali; na iwe kama ulivyosema.” 35Siku ile ile Yakobo akawaondoa beberu wote waliokuwa na mistari au madoadoa, na mbuzi jike wote waliokuwa na mistari au madoadoa (wote waliokuwa na alama nyeupe juu yao), na wana-kondoo weusi wote, akawaweka chini ya uangalizi wa wanawe. 36Kisha Labani akamwacha Yakobo kwa mwendo wa safari ya siku tatu, naye Yakobo akaendelea kuchunga lile kundi la Labani lililobaki.
37Lakini Yakobo akachukua fito mbichi zilizokatwa wakati huo huo za miti ya mlubna, mlozi na mwaramoni, akazibambua ili mistari myeupe ionekane katika fito hizo. 38Kisha akaweka fito hizo katika mabirika yote ya kunyweshea mifugo, ili ziwe mbele ya makundi walipokuja kunywa maji. Wanyama walipokuja kunywa maji, hali wakiwa wanahitaji mbegu, 39wakapandwa hizo fito zikiwa mbele yao. Wanyama waliopata mimba mbele ya hizo fito walizaa wanyama wenye mistari, madoadoa na mabaka mabaka. 40Yakobo akawatenga wadogo wa kundi peke yao, lakini akazielekeza nyuso za hao waliobaki kwenye wale wenye mistari na weusi waliokuwa mali ya Labani. Hivyo akatenga makundi yake mwenyewe, wala hakuwachanganya na wanyama wa Labani. 41Kila mara wanyama wenye nguvu walipohitaji mbegu, Yakobo aliweka zile fito kwenye mabirika mbele ya hao wanyama, ili wapandwe karibu na hizo fito, 42lakini ikiwa wanyama walikuwa wadhaifu hakuziweka hizo fito. Hivyo wanyama wadhaifu wakawa wa Labani, na wanyama wenye nguvu wakawa wa Yakobo. 43Hivyo Yakobo akastawi sana, tena akawa na makundi makubwa, mjakazi na watumishi, na ngamia na punda.

Iliyochaguliwa sasa

Mwanzo 30: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia