Luka 8
8
Mfano wa mpanzi
(Mathayo 13:1-9; Marko 4:1-9)
1Baada ya haya Isa alienda, akawa anazunguka katika miji na vijiji akihubiri Injili ya ufalme wa Mungu. Wale wanafunzi wake kumi na wawili walikuwa pamoja naye, 2pia baadhi ya wanawake waliokuwa wametolewa pepo wachafu na kuponywa magonjwa. Miongoni mwao alikuwa Mariamu Magdalene, aliyetolewa pepo wachafu saba; 3Yoana mkewe Kuza, msimamizi wa nyumba ya watu wa nyumbani mwa Herode; Susana; na wengine wengi waliokuwa wakimhudumia kwa mali yao.
4Umati mkubwa wa watu walipokuwa wakikusanyika, nao watu walikuwa wakimjia Isa kutoka kila mji, akawaambia mfano huu: 5“Mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu zake. Alipokuwa akitawanya mbegu, nyingine zilianguka kando ya njia; zikakanyagwa, nao ndege wa angani wakazila. 6Mbegu nyingine zilianguka penye miamba, nazo zilipoota, hiyo mimea ikakauka kwa kukosa unyevu. 7Nazo mbegu nyingine zilianguka kwenye miiba, nayo ile miiba ikakua pamoja nazo, na kuisonga hiyo mimea. 8Mbegu nyingine zilianguka kwenye udongo mzuri. Zikaota na kuzaa mara mia moja zaidi ya mbegu alizopanda.”
Baada ya kusema haya, Isa akapaza sauti, akasema, “Mwenye masikio ya kusikia, na asikie.”
Sababu ya kufundisha kwa mifano
(Mathayo 13:9-17; Marko 4:10-12)
9Wanafunzi wake wakamuuliza maana ya mfano huo. 10Naye akasema, “Ninyi mmepewa ujuzi wa siri za ufalme wa Mungu, lakini kwa wengine nazungumza kwa mifano, ili,
“ ‘ingawa wanatazama, wasione;
ingawa wanasikiliza, wasielewe.’#8:10 Isaya 6:9
Maelezo ya mfano wa mbegu
(Mathayo 13:18-23; Marko 4:13-20)
11“Maana ya mfano huu ni hii: Mbegu ni neno la Mungu. 12Zile zilizoanguka kando ya njia ni wale ambao husikia neno, naye ibilisi anakuja na kuliondoa neno kutoka mioyoni mwao, ili wasije wakaamini na kuokoka. 13Zile mbegu zilizoanguka kwenye mwamba ni wale ambao hulipokea neno kwa furaha wanapolisikia, lakini hawana mizizi. Wanaamini kwa muda mfupi, lakini wakati wa kujaribiwa huiacha imani. 14Zile mbegu zilizoanguka kwenye miiba ni mfano wa wale wanaosikia, lakini wanapoendelea husongwa na masumbufu ya maisha haya, utajiri na anasa, nao hawakui. 15Lakini zile mbegu zilizoanguka kwenye udongo mzuri ni mfano wa wale ambao hulisikia neno la Mungu na kulishika kwa moyo mnyofu wa utiifu, nao kwa kuvumilia kwingi huzaa matunda.
Mfano wa taa
(Marko 4:21-25)
16“Hakuna mtu awashaye taa na kuificha ndani ya gudulia au kuiweka mvunguni mwa kitanda. Badala yake, huiweka juu ya kinara, ili wale wanaoingia ndani waone mwanga. 17Kwa maana hakuna jambo lolote lililofichika ambalo halitafichuliwa, wala lolote lililositirika ambalo halitajulikana na kuwekwa wazi. 18Kwa hiyo, kuweni waangalifu mnavyosikia. Kwa maana yeyote aliye na kitu atapewa zaidi. Lakini yule asiye na kitu, hata kile anachodhani anacho atanyang’anywa.”
Mama yake na ndugu zake Isa
(Mathayo 12:46-50; Marko 3:31-35)
19Wakati mmoja mama yake Isa na ndugu zake walikuja kumwona, lakini hawakuweza kumfikia kwa sababu ya msongamano wa watu. 20Mtu mmoja akamwambia, “Mama yako na ndugu zako wako nje wanataka kukuona.”
21Isa akamjibu, “Mama yangu na ndugu zangu ni wale wote wanaolisikia neno la Mungu na kulifanya.”
Isa atuliza dhoruba
(Mathayo 8:23-27; Marko 4:35-41)
22Siku moja Isa alipanda ndani ya mashua pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, “Tuvukeni hadi ng’ambo ya ziwa.” Nao wakaondoka. 23Hivyo walipokuwa wakienda, akalala usingizi. Dhoruba kali ikatokea mle ziwani, hata mashua ikawa inajaa maji, nao walikuwa katika hatari kubwa.
24Wanafunzi wake wakamwendea na kumwamsha, wakisema, “Bwana#8:24 Wale ambao hawakumfahamu Isa kuwa Masihi walimwita “Bwana” kwa heshima ya kawaida., Bwana, tunaangamia!”
Yeye akaamka, akaukemea ule upepo na yale mawimbi; dhoruba ikakoma, nako kukawa shwari. 25Akawauliza wanafunzi wake, “Imani yenu iko wapi?”
Kwa woga na mshangao wakaulizana, “Huyu ni nani, ambaye anaamuru hata upepo na maji, navyo vikamtii?”
Isa amponya mtu mwenye pepo mchafu
(Mathayo 8:28-34; Marko 5:1-20)
26Basi wakafika katika nchi ya Wagerasi, iliyo upande wa pili wa ziwa kutoka Galilaya. 27Isa aliposhuka kutoka mashua na kukanyaga ufuoni, alikutana na mtu mmoja wa mji ule aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, naye kwa muda mrefu alikuwa havai nguo wala kuishi nyumbani, bali aliishi makaburini. 28Alipomwona Isa, alipaza sauti, akajitupa chini mbele yake na kusema kwa sauti kuu, “Una nini nami, Isa, Mwana wa Mungu#8:28 Yaani Mwana wa asili moja na Mwenyezi Mungu (Yohana 1:1-2), wa kiroho, bali si wa kimwili. Aliye Juu Sana? Nakuomba, usinitese!” 29Wakati huo Isa alikuwa amemwamuru yule pepo mchafu amtoke huyo mtu. Mara nyingi huyo pepo mchafu alimpagaa, na hata alipofungwa kwa minyororo mikono na miguu na kuwekwa chini ya ulinzi, alikata hiyo minyororo na kupelekwa na huyo pepo mchafu kwenda nyikani.
30Isa akamuuliza, “Jina lako ni nani?”
Akamjibu, “Legioni#8:30 maana yake Jeshi,” kwa kuwa alikuwa ameingiwa na pepo wachafu wengi mno. 31Wale pepo wachafu wakamsihi sana asiwaamuru kwenda katika Shimo#8:31 Shimo hapa ina maana Abyss (yaani shimo lisilo na mwisho), yaani Kuzimu..
32Palikuwa na kundi kubwa la nguruwe hapo likilisha kando ya kilima. Wale pepo wachafu wakamsihi Isa awaruhusu wawaingie hao nguruwe, naye akawaruhusu. 33Wale pepo wachafu walipomtoka yule mtu, wakawaingia wale nguruwe, nalo kundi lote likateremkia gengeni kwa kasi, likatumbukia ziwani na kuzama.
34Wale watu waliokuwa wakichunga lile kundi la nguruwe walipoona yaliyotukia, wakakimbia, wakaeneza habari hizi mjini na mashambani. 35Nao watu wakatoka kwenda kujionea wenyewe yaliyotukia. Walipofika hapo alipokuwa Isa, wakamkuta yule mtu aliyetokwa na pepo wachafu amekaa karibu na Isa, akiwa amevaa nguo na mwenye akili timamu! Wakaogopa. 36Wale walioyaona mambo hayo wakawaeleza watu wengine jinsi yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo wachafu alivyoponywa. 37Ndipo watu wote wa nchi ile ya Wagerasi wakamwomba Isa aondoke kwao, kwa sababu walikuwa wamejawa na hofu. Basi akaingia katika mashua, akaondoka zake.
38Yule mtu aliyetokwa na pepo wachafu akamsihi Isa afuatane naye, lakini Isa akamuaga, akamwambia: 39“Rudi nyumbani ukawaeleze mambo makuu Mungu aliyokutendea.” Kwa hiyo yule mtu akaenda, akatangaza katika mji wote mambo makuu ambayo Isa alimtendea.
Isa amponya mwanamke na kumfufua msichana
(Mathayo 9:18-26; Marko 5:21-43)
40Basi Isa aliporudi, umati mkubwa wa watu wakampokea kwa furaha, kwani walikuwa wakimngojea. 41Kisha mtu mmoja, jina lake Yairo, aliyekuwa kiongozi wa sinagogi#8:41 Nyumba ya ibada na mafunzo., akaja na kuanguka miguuni mwa Isa, akimwomba afike nyumbani mwake, 42kwa kuwa binti yake wa pekee, mwenye umri wa miaka kumi na mbili, alikuwa anakufa.
Isa alipokuwa akienda, umati wa watu wakamsonga sana. 43Palikuwa na mwanamke mmoja aliyekuwa na tatizo la kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na mbili, [na alikuwa amegharimia mali yake yote kwa matibabu]#8:43 Maandiko mengine ya kale hayana maneno haya. lakini hakuna yeyote aliyeweza kumponya. 44Huyo mwanamke akaja kwa nyuma ya Isa na kugusa upindo wa vazi lake. Mara kutokwa damu kwake kukakoma.
45Isa akauliza, “Ni nani aliyenigusa?”
Watu wote walipokana, Petro akasema, “Bwana, umati huu wa watu wanakusonga na kukusukuma kila upande.”
46Lakini Isa akasema, “Kuna mtu aliyenigusa, kwa maana nimetambua kuwa nguvu zimenitoka.”
47Yule mwanamke alipofahamu ya kuwa hawezi kuendelea kujificha, alikuja akitetemeka, akaanguka miguuni mwa Isa. Akaeleza mbele ya watu wote kwa nini alimgusa na jinsi alivyoponywa mara moja. 48Basi Isa akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani.”
49Isa alipokuwa bado anasema, akaja mtumishi kutoka nyumbani mwa Yairo, yule kiongozi wa sinagogi, kumwambia, “Binti yako amekwisha kufa. Usiendelee kumsumbua Mwalimu.”
50Isa aliposikia jambo hili, akamwambia Yairo, “Usiogope. Amini tu, naye binti yako atapona.”
51Walipofika nyumbani mwa Yairo, hakumruhusu mtu yeyote aingie ndani naye isipokuwa Petro, Yohana na Yakobo, pamoja na baba na mama wa yule binti. 52Wakati ule ule watu wote walikuwa wakilia na kuomboleza kwa ajili ya huyo binti. Isa akawaambia, “Acheni kulia. Huyu binti hajafa, ila amelala.”
53Wao wakamcheka kwa dharau, wakijua kuwa amekwisha kufa. 54Isa akamshika yule binti mkono na kuita, “Binti, amka!” 55Roho yake ikamrudia, naye akainuka mara moja. Akaamuru apewe kitu cha kula. 56Wazazi wake wakastaajabu sana, lakini Isa akawakataza wasimwambie mtu yeyote kuhusu yale yaliyotukia.
Iliyochaguliwa sasa
Luka 8: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.