Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 21

21
Kuzaliwa kwa Isaka
1Mwenyezi-Mungu alimkumbuka Sara, akamtendea kama alivyoahidi. 2Basi, Abrahamu akiwa mzee, Sara akapata mimba, akamzalia mtoto wa kiume, wakati uleule Mungu alioutaja. 3Abrahamu akampa huyo mwanawe ambaye Sara alimzalia jina Isaka. 4Isaka alipotimiza umri wa siku nane, Abrahamu akamtahiri kama alivyoamriwa na Mungu. 5Abrahamu alikuwa na umri wa miaka 100 wakati mwanawe Isaka alipozaliwa. 6Naye Sara akasema, “Mungu amenipatia kicheko#21:6 kicheko: Jina Isaka Kiebrania maana yake ni “Hucheka” (taz pia 17:17-19).; yeyote atakayesikia habari hizi, atacheka pamoja nami.” 7Kisha akaongeza, “Ni nani angeweza kumwambia Abrahamu kwamba mimi Sara nitanyonyesha watoto? Tena nimemzalia mtoto wa kiume katika uzee wake!”
8Isaka akaendelea kukua, na siku alipoachishwa kunyonya, Abrahamu akafanya sherehe kubwa.
Hagari anafukuzwa
9Baadaye Sara alimwona Ishmaeli, mtoto wa Abrahamu aliyezaliwa na Hagari, Mmisri, akicheza na Isaka mwanawe. 10Basi, Sara akamwambia Abrahamu, “Mfukuzie mbali mjakazi huyu na mwanawe. Haiwezekani kabisa mtoto wa mjakazi kurithi pamoja na mwanangu Isaka.” 11Jambo hili lilimhuzunisha sana Abrahamu kwa kuwa Ishmaeli pia alikuwa mtoto wake. 12Lakini Mungu akamwambia Abrahamu, “Usihuzunike kwa sababu ya mtoto huyu, wala huyo mtumwa wako wa kike. Lolote akuambialo Sara lifanye; kwa kweli wazawa wako watatokana na Isaka. 13Na kuhusu huyo mwana wa mjakazi wako, nitamfanya awe baba wa taifa kubwa kwa kuwa yeye pia ni mtoto wako.”
14Hivyo, asubuhi na mapema, Abrahamu akachukua chakula na kiriba cha maji, akampa Hagari na kumtwika begani; akamfukuza pamoja na mwanawe. Hagari akaondoka, akawa anatangatanga nyikani Beer-sheba.
15Ikawa maji yalipomwishia katika kile kiriba, Hagari akamlaza mwanawe chini ya mti. 16Naye akaenda kando, akaketi umbali wa kama mita 100 hivi, akisema moyoni mwake, “Heri nisimwone mwanangu akifa.” Na alipokuwa ameketi hapo, mtoto#21:16 mtoto: Tafsiri moja ya awali ina Hagari. akalia kwa sauti.
17Mungu akamsikia mtoto huyo akilia, na malaika wa Mungu akamwita Hagari kutoka mbinguni, akamwambia, “Una shida gani Hagari? Usiogope; Mungu amesikia sauti ya mtoto huko alipo. 18Simama umwinue mtoto na kumshika vizuri mikononi mwako, kwani nitamfanya awe baba wa taifa kubwa.” 19Mungu akamfumbua Hagari macho, naye akaona kisima cha maji. Akaenda akajaza kiriba maji, akamnywesha mtoto wake.
20Mungu akawa pamoja na huyo mtoto, naye akaendelea kukua. Alikaa nyikani na akawa mpiga upinde hodari sana. 21Alikuwa akikaa katika nyika za Parani, na mama yake akamwoza mke kutoka nchi ya Misri.
Agano kati ya Abrahamu na Abimeleki
22Wakati huo, Abimeleki pamoja na Fikoli, mkuu wa jeshi lake, alimwendea Abrahamu, akamwambia, “Mungu yuko pamoja nawe katika kila kitu unachofanya. 23Kwa hiyo niapie kwa jina la Mungu kwamba hutanifanyia hila mimi au watoto wangu au wazawa wangu. Kadiri mimi nilivyokuwa mwaminifu kwako, vivyo hivyo nawe uwe mwaminifu kwangu na kwa nchi hii unamokaa.” 24Abrahamu akasema, “Naapa.”
25Wakati huo Abrahamu alikuwa amemlalamikia Abimeleki juu ya kisima cha maji ambacho watumishi wa Abimeleki walikuwa wamemnyanganya. 26Abimeleki akamwambia, “Mimi sijui nani aliyefanya hivyo; mpaka leo hii wewe hukuniambia; wala mimi sijapata kusikia habari hizi hadi leo.” 27Basi, Abrahamu akachukua kondoo na ng'ombe akampa Abimeleki nao wawili wakafanya agano baina yao. 28Abrahamu akatenga wanakondoo wa kike saba. 29Abimeleki akamwuliza Abrahamu, “Kwa nini unawatenga hao wanakondoo wa kike saba?” 30Abrahamu akamjibu, “Hawa wanakondoo wa kike saba ninakupa kwa mkono wangu mwenyewe kama shahidi wangu kwamba mimi ndimi niliyechimba kisima hiki.” 31Kwa hiyo kisima hicho kikaitwa Beer-sheba,#21:31 Beer-sheba: Kiebrania maana yake ni “Kisima cha Kiapo” au “Kisima cha Wale Saba” (taz pia 26:33). maana wote wawili walikula kiapo mahali hapo. 32Hivyo, wakafanya agano huko Beer-sheba. Abimeleki na Fikoli, mkuu wa jeshi lake, akaondoka na kurudi katika nchi ya Wafilisti. 33Abrahamu akapanda mkwaju huko Beer-sheba, akaomba kwa jina la Mwenyezi-Mungu, akamwabudu Mungu, Mungu wa milele. 34Abrahamu alikaa katika nchi ya Wafilisti muda mrefu.

Iliyochaguliwa sasa

Mwanzo 21: SCLDC10

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia