Matendo 7
7
1KUHANI mkuu akasema, Je! Mambo hayo ndivyo yalivyo?
2Nae akasema, Ndugu zangu na baba zangu, sikilizeni: Mungu wa utukufu alimtokea baba yetu Ibrahimu, alipokuwa katika Mesopotamia, kabla hajakaa Kharran, akamwambia, 3Toka katika inchi yako na katika jamaa zako, ukaende hatta inchi nitakayokuonyesha. 4Ndipo alitoka katika inchi ya Wakaldayo, akakaa Kharran, akatoka huko baada ya kufa baba yake, Mungu akamhamisha hatta inchi hii mnayokaa ninyi sasa. 5Wala hakumpa urithi humu hatta kiasi cha kuweka mguu: akaahidi kwamba atampa, iwe milki yake, na ya, uzao wake baadae, alipokuwa hana mtoto. 6Mungu akanena hivi, ya kama wazao wake watakuwa wageni katika inchi ya watu wengine, nao watawafanya kuwa watumwa wao, na kuwatenda mabaya kwa muda wa miaka aroba mia. 7Na lile taifa watakaowafanya watumwa nitawahukumu mimi, alisema Mungu; na baada ya hayo watatoka, nao wataniabudu mahali hapa. 8Akampa agano la Tohara; bassi Ibrahimu akazaa Isaak, akamtahiri siku ya nane. Isaak akamzaa Yakobo, Yakobo akawazaa wale thenashara, wazee wetu. 9Wale wazee wetu wakamwonea wivu Yusuf, wakamwuza aende Misri. Mungu akawa pamoja nae, 10akamtoa katika misiba yake yote, akampa kibali na hekima mbele ya Farao, mfalme wa Misri: nae akamfanya msimamizi wa Misri na nyumba yake yote. 11Bassi kukawa njaa juu ya inchi yote ya Misri na Kanaan, na dhiki nyingi, wala baba zetu hawakupata chakula cha kuwatosha. 12Hatta Yakobo aliposikla ya kwamba huko Misri kuna nafaka, akawatuma baba zetu marra ya kwanza. 13Hatta safari ya pili Yusuf akajitambulisha kwa ndugu zake, jamaa ya Yusuf ikawa dhahiri kwa Farao. 14Yusuf akatuma watu akamwita Yakobo baba yake na jamaa zake wote pia, watu sabaini na watano. 15Yakobo akashuka hatta Misri, akafariki yeye na baba zetu; 16wakachukuliwa hatta Sukem wakazikwa katika kaburi lile, ambalo Ibrahimu alilinunua kwa kimo cha fedha kwa wana wa Emmor, huko Sukem. 17Bassi wakati wa ile ahadi ambayo Mungu alimpa Ibrahimu ulipokuwa unakaribia, wale watu wakazidi na kuongezeka sana huko Misri, 18mpaka mfalme mwingine akaondoka, asiyemfahamu Yusuf. 19Huyo akawafanyia hila baba zetu, na kuwatenda mabaya baba zetu, akiwaamuru watupe watoto wao wachanga, illi wasiishi. 20Wakati huo akazaliwa Musa, nae alikuwa mzuri sana, akalelewa muda wa miezi mitatu katika nyumba ya baba yake. 21Hatta alipotupwa, binti Farao akamtwaa, akamlea awe kama mwana wake. 22Musa akafundishwa hekima yote ya Misri, akawa hodari wa maneno na matendo. 23Umri wake ulipopata kama miaka arubaini akaazimu moyoni kwenda kuwatazama ndugu zake wana wa Israeli. 24Akamwona mmoja akidhulumiwa, akamhami, akamlipia kisasi yule aliyekuwa akionewa, akampiga Mmisri. 25Alidhani kwamba ndugu zake watafahamu ya kuwa Mungu anawapa wokofu kwa mkono wake, lakini hawakufahamu. 26Siku ya pili yake akawatokea walipokuwa wakishindana, akataka kuwapatanisha, akisema, Enyi bwana zangu, ninyi m ndugu: Mbona mnadhulumiana? 27Lakini yeye aliyemdhulumu mwenziwe akamsukumia mbali, akisema, Ni nani aliyekuweka kuwa mkuu wetu, na mwamuzi wetu? 28Je! wataka kuniua mimi kama ulivyomwua yule Mmisri jana? 29Musa akakimbia kwa neno hilo, akakaa hali ya mgeni katika inchi ya Madiani, akazaa wana wawili huko. 30Hatta miaka arubaini ilipotimia, malaika wa Bwana akamtokea katika jangwa la mlima Sinai katika mwali wa moto, kijitini. 31Musa alipouona, akastaajabia maono yale, na alipokaribia illi atazame, sauti ya Bwana ikamjia, 32Mimi ni Mungu wa baba zako, Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaak, na Mungu wa Yakobo. 33Musa akatetemeka, asithubutu kutazama. Bwana akamwambia, Vua viatu vyako, kwa maana mahali hapa unaposimama ni inchi takatifu. 34Yakini nimeona mateso ya watu wangu waliomo Misri, nimesikia kuugua kwao, nimeshuka niwatoe. Bassi sasa, nitakutuma hatta Misri. 35Musa huyo waliyemkataa, wakisema, Ni nani aliyekuweka kuwa mkuu na mwamuzi? ndiye aliyetumwa na Mungu kuwa mkuu na mkombozi, kwa mkono wa yule malaika aliyemtokea katika kile kijiti. 36Huyo ndiye aliyewatoa, akifanya ajabu na ishara katika inchi ya Misri, na katika bahari ya Sham, na katika jangwa muda wa miaka arubaini. 37Musa huyo ndiye aliyewaambia wana wa Israeli, Bwana Mungu wenu atawainulieni nabii katika ndugu zenu, kama mimi: mtamsikia huyo. 38Yeye ndiye aliyekuwa katika kanisa jangwani pamoja na yule malaika aliyesema nae katika mlima Sinai, tena pamoja na baba zetu: ndiye aliyepokea maneno ya uzima atupe sisi. 39Mtu huyo baba zetu hawakutaka kumtii, bali wakamsukumia mbali, na kwa mioyo yao wakarudi Misri, 40wakamwambia Haruni, Tufanyie miungu, watakaotutangulia: maana huyo Musa, aliyetutoa katika inchi ya Misri, hatujui lililompata. 41Wakafanya ndama siku zile, wakaleta dhabihu kwa sanamu ile, wakafurahia kazi ya mikono yao. 42Bassi Mungu akaghairi, akawaacha, wakaliabudu jeshi la mbinguni, kama ilivyoandikwa katika kitabu cha manabii,
Je! mlinitolea dhabihu na sadaka
Miaka arubaini katika jangwa, enyi nyumba ya Israeli?
43Nanyi mlichukua khema ya Molok,
Na nyota za mungu wenu Refan,
Sanamu mlizozifanya illi kuziabudu:
Nami nitawabamisha mwende mbali hatta Babel.
44Ile khema ya shahada ilikuwa pamoja na baba zetu jangwani, kama alivyoagiza yeye aliyesema na Musa, ya kwamba aifanye sawa sawa na mfano ule aliouona; 45ambayo baba zetu waliipokea; wakaiingiza pamoja na Yoshua katika milki ya mataifa wale, ambao Mungu aliwafukuza mbele ya baba zetu, mpaka siku za Daud: 46aliyepata kibali mbele ya Mungu, nae aliomba ampatie Mungu wa Yakobo maskani. 47Lakini Sulemani alimjengea nyumba. 48Illakini yeye aliye juu hakai katika nyumba zilizofanyika kwa mikono, kama vile asemavyo nabii:
49Mbingu ni kiti changu cha enzi,
Na inchi ni mahali pa kutia miguu yangu:
Ni nyumba gani mtakayonijengea? asema Bwana:
Au ni mahali gani nitakapostarebe?
50Sio mkono wangu uliofanya haya yote?
51Enyi wenye shingo gumu, msiotahiriwa mioyo wala masikio, siku zote mnampinga Roho Mtakatifu; kama baba zenu walivyofanya na ninyi vivyo hivyo. 52Ni yupi katika manabii ambae baba zenu hawakumwudhi? nao waliwaua wale waliotabiri khabari za kuja kwake yule mwenye haki; ambae ninyi sasa mmemsaliti mkamwua; 53ninyi mlioipokea torati kwa khuduma ya malaika wala hamkuishika.
54Bassi waliposikia maneno haya, wakachomwa mioyo, wakamsagia meno. 55Nae akijaa Roho Mtakatifu, akakaza macho yake, akitazama mbinguni, akauona utukufu wa Mungu, na Yesu akisimama mkono wa kuume wa Mungu. 56Akasema, Tazama! naona mbingu zimefunuliwa, na Mwana wa Adamu amesimama mkono wa Mungu. 57Wakapiga kelele kwa sauti kuu, wakaziba masikio yao, wakamrukia kwa nia moja, 58wakamtoa nje ya mji, wakampiga mawe. Nao mashahidi wakaweka nguo zao miguuni pa kijana mmoja aliyekwitwa Saul. 59Wakampiga mawe Stefano, nae akiomba, akisema, Bwana Yesu, pokea roho yangu. 60Akapiga magoti, akalia kwa sauti kuu, Bwana, usiwahesabie dhambi hii. Akiisha kusema haya akalala.
Iliyochaguliwa sasa
Matendo 7: SWZZB1921
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Swahili New Testament © Bible Society of Tanzania, 1921.