Luka MT. 21
21
1AKAINUA macho yake akawaona watu wakitia sadaka zao katika sanduku ya hazina, watu matajiri. 2Akamwona na mjane mmoja maskini, akitia robo pesa mbili. 3Akasema, Amin, nawaambieni, Huyu mjane maskini ametia vingi kuliko wote: 4kwa maana hawa wote wametia katika sadaka za Mungu baadhi ya mali iliyowazidi, bali huyu katika mahitaji yake ametia vitu vyote alivyokuwa navyo.
5Hatta watu kadha wa kadha walipokuwa wakinena khabari za hekalu, ya kama lilipambwa kwa mawe mazuri, na sadaka za watu, akasema, 6Haya mnayoyatazama, siku zitakuja, halitasalia jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomolewa. 7Wakuimwuliza, wakisema, Mwalimu, haya yatakuwa lini, bassi? Na nini dalili ya kuwa haya yote ni karibu ya kutimia? 8Akasema, Jibadharini, msidanganyike; kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakinena, Mimi ndiye, na, Majira yamekaribia. Bassi, msiwafuate hawo. 9Nanyi mtakaposikia khabari za vita na fitina msitishwe: maana haya hayana buddi kutukia kwanza, lakini mwisho wenyewe hauji marra moja. 10Kiisha akawaambia, Taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme: 11kutakuwa na matetemeko makubwa ya inchi mahali mahali, na njaa, na tauni. Kutakuwa na mambo ya kutisha, na ishara kuu kutoka mbinguni. 12Lakini kabla ya haya yote watawakamateni na kuwaudhini, watawapelekeni mbele ya sunagogi na gerezani, mkichukuliwa mbele ya wafalme na maliwali kwa ajili ya jina langu. 13Lakini haya yatapata kuwa ushuhuda wenu. 14Azimuni bassi mioyoni mwenu, msitafakari mbele mtakavyojibu. 15Kwa maana mimi nitawapeni kinywa na hekima, ambayo watesi wenu hawataweza kuikana wala kushindana nayo. 16Nanyi mtasalitiwa na wazazi wenu, na ndugu zenu, na jamaa zenu, na rafiki zenu, nao watawafisha wengine wenu. 17Mtachukizwa na watu wote kwa ajili ya jina langu. 18Na unywele wa vichwa vyenu hautapotea kamwe. 19Kwa subira yenu mtazipata robo zenu.
20Lakini, mtakapoona Yerusalemi unazungukwa na majeshi, ndipo jueni ya kuwa uharibifu wake umekaribia. 21Ndipo walio katika Yahudi wakimbilie milimani, na walio katikati yake watoke waende zao, na walio shambani wasiuingie. 22Kwa sababu hizi ni siku ya mapatilizo, yote yaliyoandikwa yapate kutimizwa. 23Ole wao wenye mimba na wanyonyeshao siku zile! kwa maana itakuwa shidda kuu juu ya inchi, na ghadhabu juu ya watu hawa. 24Nao wataanguka kwa ukali wa upanga, watachukuliwa mateka mpaka mataifa yote: nao Yerusalemi utakanyagwa na mataifa, hatta majira ya mataifa yatakapotimia. 25Na kutakuwa ishara katika jua na mwezi na nyota: na katika inchi dhiiki ya mataifa, wakishangaa kwa uvumi wa bahari na msukosuko wake; 26watu wakizimia kwa khofu, na kwa kutazamia yanayoujia ulimwengu; kwa maana nguvu za mbingu zitatikisika. 27Ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija katika wingu kwa nguvu na utukufu mwingi. 28Bassi hayo yaanzapo kuwa, tazameni juu, mkainue vichwa vyenu kwa kuwa ukombozi wenu unakaribia. 29Akawaambia mfano; Utazameni mtini na miti yote; 30iishapo kuchupua, mwaona na kutambua nafsini mwenu ya kwamba mavuno yameisha kuwa karibu. 31Nanyi vivyo hivyo mwonapo hayo yanakuwa, tambueni ya kuwa ufalme wa Mungu u karibu. 32Amin, nawaanibieni, Kizazi hiki hakitapita kamwe hatta haya yote yatimizwe. 33Mbingu na inchi zitapita; bali maneno yangu hayatapita kamwe. 34Bassi, jiangalieni, mioyo yenu isije ikalemewa na ulafi na ulevi, na masumbufu ya maisha haya, 35siku ile ikawajieni kwa ghafula, kama mtego, maana hivyo ndivyo itakavyowajia watu wote wakaao juu ya uso wa dunia yote. 36Kwa hiyo kesheni killa wakati, mkiomba mpate kuhesabiwa kuwa mmestahili kuponea haya yote yatakayokuwa, na kusimama mahali penu mbele ya Mwana wa Adamu.
37Bassi killa siku alikuwa akifundisha hekaluni wakati wa mchana; na wakati wa usiku akitoka, na kulala katika mlima uitwao mlima wa mizeituni. 38Watu wote wakaamka mapema wakamwendea alfajiri mle hekaluni illi kumsikiliza.
Iliyochaguliwa sasa
Luka MT. 21: SWZZB1921
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Swahili New Testament © Bible Society of Tanzania, 1921.