Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 12

12
Kuwafundisha wanafunzi.
1Makundi yalipokuwa yamekusanyika maelfu ya watu wakakanyagana kwa kuwa wengi; ndipo, alipoanza kuwaambia kwanza wanafunzi wake; Jilindeni kwa ajili ya chachu ya Mafariseo iliyo ujanja!#Mat. 16:6; Mar. 8:15.
(2-9: Mat. 10:26-33.)
2Hakuna lililofunikwa lisilofunuliwa halafu, wala hakuna lililofichwa lisilotambulikana halafu.#Luk. 8:17; Mar. 4:22. 3Maneno yote, mnayoyasema gizani, yatasikiwa mwangani; nalo mnalolinong'oneza masikioni nyumbani, litatangazwa barazani. 4Lakini nawaambiani ninyi, wapenzi wangu: Msiwaogope wanaoweza kuiua miili tu, kisha hawana wanachoweza kuwafanyia tena! 5Lakini nitawaonyeshani ninyi wa kumwogopa: Mwogopeni yule anayeweza kuwaua, kisha yuko na nguvu ya kuwatupa shimoni mwa moto! Kweli nawaambiani: Huyo mwogopeni! 6Je? Videge vitano haviuzwi kwa senti mbili? Lakini hata mmoja wao hasahauliwi mbele ya Mungu. 7Lakini kwenu ninyi hata nywele za vichwani penu zimehesabiwa zote. Kwa hiyo msiogope, ninyi mnapita videge vingi!#Luk. 21:18. 8Lakini nawaambiani: Kila atakayeungama mbele ya watu, kwamba ni mtu wangu, naye Mwana wa mtu ataungama mbele ya malaika wa Mungu, kwamba ni mtu wangu. 9Lakini atakayenikana mbele ya watu atakanwa mbele ya malaika wa Mungu.#Luk. 9:26. 10Kila atakayesema neno la kumbisha Mwana wa mtu ataondolewa; lakini aliyembeza Roho Mtakatifu hataondolewa.#Mat. 12:32; Mar. 3:28-29. 11Lakini watakapowapeleka katika nyumba za kuombea na mabomani na pengine penye nguvu msihangaikie wala mizungu wala maneno ya kujikania wala ya kuwajibu!#Luk. 21:14-15; Mat. 10:19-20. 12Kwani Roho Mtakatifu atawafundisha saa ileile yapasayo kusema.
Mkulima akosaye werevu wa kweli.
13Kundini mwa watu alikuwamo aliyemwambia: Mfunzi, umwambie ndugu yangu, agawanye nami urithi, baba aliotuachia! 14Naye akamwambia: Mwenzangu, yuko nani aliyeniweka, niwaamue na kuwagawanyia mali zenu?
15*Akawaambia: Tazameni, mjilinde kwa ajili ya choyo cho chote! Kwani mali zikiwa nyingi sizo zinazomweka mtu, akizishika.#1 Tim. 6:9-10. 16Akawaambia mfano akisema: Kulikuwa na mtu mwenye mali, ambaye shamba lake lilikuwa limezaa sana. 17Ndipo, alipofikiri moyoni mwake akisema: Nifanyeje? Kwani sina pa kuyawekea mavuno yangu? 18Kisha akasema: Nitafanya hivyo: nitayavunja mawekeo yangu, nijenge makubwa kuyapita hayo ndimo niziweke ngano zangu na mali zangu zote. 19Ndipo, nitakapoiambia roho yangu: Roho yangu, unayo mema mengi yaliyowekwa ya miaka mingi. Basi, tulia, ule, unywe na kuchangamka! 20Lakini Mungu akamwambia: Mpumbavu wee! Usiku huu watakutoza roho yako; nayo, uliyoyalimbika, yatakuwa ya nani?#Ebr. 9:27. 21Ndivyo, vinavyoendelea vya mwenye kukusanya mali nyingi, asipoziweka kwa Mungu.*
Kujihangaisha.
(22-31: Mat. 6:25-33.)
22Akawaambia wanafunzi wake: Kwa hiyo nawaambiani: Msiyasumbukie maisha yenu mkisema: Tutakula nini? Wala msiisumbukie miili yenu mkisema: Tutavaa nini? 23Kwani maisha hupita vyakula, nao mwili hupita mavazi. 24Jifundisheni kwa makunguru! Hawapandi, wala hawavuni, wala hawana vichanja wala wekeo jingine. Naye Mungu anawalisha nao. Je? Ninyi hamwapiti ndege pakubwa?#Sh. 147:9. 25Tena kwenu yuko nani anayeweza kwa kusumbuka kwake kujiongezea miaka yake kipande kama cha mkono tu? 26Basi, msipokiweza hata kilicho kidogo sana, yale mengine mwayasumbukiaje?
27Jifundisheni kwa maua ya uwago, kama yanavyokua! Hayafanyi kazi wala hayafumi nguo. Lakini nawaambiani: Hata Salomo katika utukufu wake wote hakuvikwa kama moja lao. 28Basi, Mungu akiyavika hivyo majani ya porini yanayokaa leo tu, kesho yatupwe katika mabiwi, yateketee, je? Hatazidi kuwavika ninyi? Mbona mnamtegemea kidogo tu? 29Basi, ninyi msiulize: Tutakula nini? au: Tutakunywa nini? Wala msijikweze!#Sh. 39:7. 30Kwani wamizimu waliomo ulimwenguni ndio wanaoyatafuta hayo yote; lakini Baba yenu amewajua, ya kuwa mnapaswa nayo. 31Lakini utafuteni ufalme wake! Ndivyo mtakavyopewa hayo.#Luk. 22:29; Yes. 41:14. 32Msiogope, mlio kikundi kidogo! Kwani baba yenu imempendeza kuwapa ninyi huo ufalme.
(33-34: Mat. 6:20-21.)
33Uzeni vitu vyenu, mpate ya kuwagawia maskini! Jishoneeni mifuko isiyochakaa ya kuwekea mbinguni limbiko lisilopungua! Tena ndiko, kusikofika mwizi, wala kusikoharibiwa na mende.#Luk. 18:22. 34Kwani limbiko lenu liliko, ndiko, nayo mioyo yenu itakakokuwa.
Kukesha.
(35-46: Mat. 24:42-51.)
35*Mwe mmejifunga viuno vyenu, nazo taa zenu ziwe zinawaka!#2 Mose 12:11; Mat. 25:1-13; 1 Petr. 1:13. 36Nanyi mfanane na watu wanomngoja bwana wao, atakaporudi kutoka arusini, kusudi wamfungulie mlango papo hapo, atakaporudi na kupiga hodi.#Ufu. 3:20. 37Wenye shangwe ni watumwa wale, ambao bwana atakapokuja atawakuta, wakikesha. Kweli nawaambiani: Atajifunga na kuwaketisha chakulani, naye atakuja kuwatumikia. 38Wenye shangwe ndio, atakaowakuta hivyo, hata akija zamu ya pili au ya tatu ya kulinda usiku. 39Lakini litambueni neno hili: kama mwenye nyumba angaliijua saa, mwizi atakayojia, hangaliacha, nyumba yake ibomeolewe.#1 Tes. 5:2. 40Nanyi mwe tayari! Kwani Mwana wa mtu atajia saa, msiyomwazia.
Msimamizi mwelekevu.
41Petero akasema: Bwana, mfano huu unatuambia sisi tu au watu wote? 42Bwana akasema: Basi, yuko nani aliye mtunzaji mwelekevu na mwerevu, bwana wake atakayempa kuwatunza watumwa wake, awape posho, saa yao itakapofika? 43Mwenye shangwe ni mtumwa yule, bwana wake atakayemkuta, akifanya hivyo, atakapokuja.* 44Kweli nawaambiani: Atampa kuzitunza mali zake zote.#Mat. 25:21. 45Lakini yule mtumwa akisema moyoni mwake: Bwana wangu anakawia, akaanza kuwapiga watumwa na vijakazi, hata kula na kunywa na kulewa, 46bwana wake mtumwa yule atamjia siku, asiyomngojea, na saa, asiyoitambua, kisha atamchangua kuwa vipande viwili, nalo fungu lake atampa pamoja nao wasiomtegemea Mungu. 47Maana yule mtumwa aliyeyatambua, bwana wake ayatakayo, asijitengeneze, wala asiyafanye hayo, aliyoyataka, huyo atapigwa fimbo nyingi. 48Lakini yule asiyeyatambua alipofanya yapasayo kupigwa atapigwa fimbo chache. Kwani kila aliyepewa mengi, kwake yatatafutwa mengi, naye waliyemwagizia mengi watazidi kumwuliza mengi.
Kuleta magombano.
49Nalijia kutupa moto nchini, tena hakuna ninachokitaka, ila uwake. 50Lakini ninao ubatizo, ndio nibatizwe; nami ninasongeka sana, mpaka umalizike.#Mat. 20:22; 26:38; Mar. 10:39; Yoh. 12:27.
(51-53: Mat. 10:34-36.)
51Mwaniwazia, kwamba nimejia kuiletea nchi utengemano? Nawaambiani: Sivyo, ila naleta matengano. 52Kwani tokea sasa watu watano waliomo katika nyumba moja watatengana, watatu wagombanishe wawili, nao wawili wagombanishe watatu. 53Watagombana baba na mwana wake, tena mwana na baba yake, tena mama na mwana wake wa kike, tena mwana wa kike na mama yake, vilevile mkwe na mkwewe.#Mika 7:6.
Kupambanua vielekezo.
54Akayaambia makundi ya watu: Mnapoona wingu linalotoka machweoni, papo hapo mnasema: Mvua inakuja; nayo inakuja kweli.#Mat. 16:2-3. 55Tena mnaposikia upepo unaovuma kusini mnasema: Litakuwa jua kali; nalo linakuwapo. 56Enyi wajanja, mnayoyaona ya nchini na ya mbinguni mnajua kuyapambanua, mbona hamzipambanui siku hizi za sasa? 57Tena ninyi wenyewe, mbona hamfuati uamuzi wenye wongofu? 58Kwani mnapokwenda bomani, wewe na mshitaki wako, umkaze njiani, mpatane, maana asikukokote kwa mwenye hukumu, naye mwenye hukumu asikutie mkononi mwa mpiga fimbo, naye mpiga fimbo asikutie kifungoni.#Mat. 5:25-26. 59Nakuambia: Hutatoka humo kabisa, mpaka utakapomaliza kulipa, isisalie hata senti moja.

Iliyochaguliwa sasa

Luka 12: SRB37

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia