Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 16

16
Mtunza mali mpotovu.
1*Akawaambia wanafunzi wake: Kulikuwako mtu mwenye mali aliyekuwa na mtunza mali. Huyu aliposengenywa kwake, ya kuwa anatapanya mali zake, 2akamwita, akamwambia: Hayo nayasikiaje kwako? Toa hesabu ya utunzaji wako wa mali zangu! Kwani huwezi tena kuzitunza mali zangu. 3Mtunza mali akasema moyoni mwake: Nifanyeje? Kwani bwana wangu ananiondoa katika utunzaji wa mali. Kulima siwezi; nako kuomba, naona soni. 4Nimetambua, nitakavyofanya, kusudi wanipokee nyumbani mwao, nitakapoondolewa katika utunzaji wa mali. 5Akawaita wadeni wa bwana wake kila mmoja, akamwambia wa kwanza: Una deni gani kwa bwana wangu? 6Aliposema: Matanaki 100 ya mafuta, akamwambia: Kichukue cheti chako, ukae, uandike 50! 7Kisha akamwambia mwingine: Na wewe una deni gani? Naye aliposema: Makanda 100 ya mchele, akamwambia: Kichukue cheti chako, uandike 80! 8Naye bwana akamsifu yule mtunza mali mpotovu, ya kuwa alifanya werevu. Kwani wana wa dunia hii huwaendea wa kizazi chao wenye werevu kuliko wana wa mwanga.#Mat. 10:16; Ef. 5:9; 1 Tes. 5:5. 9Nami nawaambiani: Jipatieni rafiki na kutoa mali za nchini zilizo za upotovu, kusudi wawapokee kwenye makao ya kale na kale, mali zitakapokoseka!#Luk. 14:13-14; Mat. 6:20; 10:40; 19:21. 10Aliye mwelekevu wa vitu vilivyo vichache huwa mwelekevu hata wa vile vilivyo vingi. Naye aliye mpotovu wa vitu vilivyo vichache huwa mpotovu hata wa vile vilivyo vingi.#Luk. 19:17. 11Basi, msipokuwa waelekevu wa mali za nchini zilizo za upotovu, yuko nani atakayewapa yaliyo ya kweli?* 12Nanyi msipokuwa waelekevu wa mali zilizo za wengine, yuko nani atakayewapa zilizo zenu? 13Hakuna mtumishi anayeweza kutumikia mabwana wawili. Kwani itakuwa hivi: atamchukia wa kwanza na kumpenda wa pili, au atashikamana naye wa kwanza na kumbeza wa pili. Hamwezi kuwatumikia wote wawili, Mungu na Mali za Nchini (Mamona).#Mat. 6:24.
14Mafariseo waliopenda fedha walipoyasikia hayo yote, wakamfyoza.#Mat. 23:14. 15Akawaambia: Ninyi hujipa wongofu wenyewe mbele ya watu, lakini Mungu anaitambua mioyo yenu. Kwani yanayokwezwa na watu huwa chukizo mbele yake Mungu.#Luk. 18:9-14; Sh. 7:10; Fano. 6:16-17. 16Mambo ya Maonyo na ya Wafumbuaji yametangazwa mpaka kuja kwake Yohana; toka hapo hutangazwa Utume mwema wa ufalme wa Mungu, tena kila mtu huingizwa kwa nguvu.#Mat. 11:12-13. 17Kukoma kwao mbingu na nchi ni kwepesi kuliko kupotea kwa kichoro kimoja tu cha Maonyo.#Mat. 5:18. 18Kila mtu anayemwacha mkewe na kuoa mwingine anazini; naye anayeoa mke aliyeachwa na mumewe anazini.#Mat. 5:32; 19:9.
Mwenye mali na Lazaro.
19*Kulikuwa na mtu mwenye mali aliyevaa nguo za kifalme na za hariri, tena kila siku hula vya urembo vilivyo vizuri sana. 20Kulikuwako hata maskini, jina lake Lazaro, alikuwa amewekwa mlangoni pake kwa kuwa mwenye vidonda. 21Akataka sana kushibishwa na makombo yaliyoanguka mezani pake mwenye mali; mbwa nao huja kumlamba vidonda vyake. 22Ikawa, maskini alipokufa akachukuliwa na malaika, akapelekwa kifuani pa Aburahamu. Kisha mwenye mali akafa naye, akazikwa. 23Alipokuwa kuzimuni katika maumivu akayainua macho yake, akamwona Aburahamu, yuko mbali, naye Lazaro alikuwa amekaa kifuani pake. 24Akaita akisema: Baba Aburahamu, nihurumie! Umtume Lazaro, achovye ncha ya kidole chake majini, aje, aupoze ulimi wangu! kwani naumia humu motoni. 25Aburahamu akasema: Mwanangu, kumbuka, ya kuwa uliyapokea mema yako katika maisha yako! Lakini Lazaro huko alipata maovu tu. Lakini sasa yeye anatulizwa moyo hapa, nawe wewe unaumia. 26Tena si kwa ajili hii tu, ila kati yetu sisi nanyi pameatuka ufa mkubwa, kusudi wanaotaka kupita toka hapa, wafike kwenu, wasiweze, wala toka huko wasiweze kupapita, wafike kwetu. 27Ndipo, alipojibu: Nakuomba, baba, umtume, aende nyumbani kwa baba yangu. 28Kwani ninao ndugu watano; aje, awashuhudie mambo ya hapa, nao wasije hapa penye maumivu. 29Aburahamu aliposema: Wanao Mose na Wafumbuaji, na wawasikilize wao!#2 Tim. 3:14-17. 30akasema: Sivyo, baba Aburahamu, lakini mtu aliyetoka kwa wafu atakapowaendea, ndipo, watakapojuta. 31Lakini akamwambia: Wasipomsikia Mose na Wafumbuaji hawataonyeka, hata mtu akifufuka katika wafu.*#Yoh. 5:46-47.

Iliyochaguliwa sasa

Luka 16: SRB37

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia