Matendo 3
3
Petro Amponya Mlemavu Kwa Jina La Isa
1 Siku moja Petro na Yohana walikuwa wanapanda kwenda Hekaluni kusali yapata saa tisa alasiri. 2 Basi palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa kiwete tangu kuzaliwa. Alichukuliwa na kuwekwa kwenye lango la Hekalu liitwalo Zuri, kila siku ili aombe msaada kwa watu wanaoingia Hekaluni. 3Huyu mtu alipowaona Petro na Yohana wakikaribia kuingia Hekaluni, akawaomba wampe sadaka. 4 Wakamkazia macho, kisha Petro akamwambia, “Tutazame sisi.” 5Hivyo yule mtu akawatazama, akitazamia kupata kitu kutoka kwao.
6 Ndipo Petro akamwambia, “Sina fedha wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Isa Al-Masihi wa Nasiri, tembea!” 7Petro akamshika yule mtu kwa mkono wa kuume akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikapata nguvu. 8 Akaruka juu na kusimama, akaanza kutembea. Kisha akaingia Hekaluni pamoja na Petro na Yohana, huku akitembea na kurukaruka na kumsifu Mungu. 9 Watu wote walipomwona akitembea na kumsifu Mungu, 10 wakamtambua kuwa ni yule mtu aliyekuwa akiketi nje ya Hekalu penye lango liitwalo Zuri akiomba msaada, nao wakajawa na mshangao, wakastaajabu juu ya yale yaliyomtukia.
Petro Anashuhudia Kuwa Isa Anaponya
11 Aliyeponywa alipokuwa akiambatana na Petro na Yohana, watu wote walishangaa mno, wakaja wakiwakimbilia pale ukumbi wa Sulemani. 12Petro alipoona watu wamekusanyika akawaambia, “Enyi Waisraeli, kwa nini mnastaajabu kuhusu jambo hili? Mbona mnatukazia macho kwa mshangao kana kwamba ni kwa uwezo wetu au utakatifu wetu tumemfanya mtu huyu kutembea? 13 Mungu wa Ibrahimu na Isaka na Yakobo, Mungu wa baba zetu amemtukuza Mwanawe Isa, ambaye ninyi mlimtoa ahukumiwe kifo na mkamkana mbele ya Pilato, ingawa yeye alikuwa ameamua kumwachia aende zake. 14 Ninyi mlimkataa huyo Mtakatifu na Mwenye Haki mkaomba mpewe yule muuaji. 15 Hivyo mkamuua aliye chanzo cha uzima, lakini Mungu akamfufua kutoka kwa wafu. Sisi tu mashahidi wa mambo haya. 16 Kwa imani katika jina la Isa, huyu mtu mnayemwona na kumfahamu ametiwa nguvu. Ni kwa jina la Isa na imani itokayo kwake ambayo imemponya kabisa huyu mtu, kama ninyi wote mnavyoona.
17 “Sasa ndugu zangu, najua ya kuwa ninyi mlitenda bila kujua, kama walivyofanya viongozi wenu. 18 Lakini kwa njia hii Mungu alitimiza kile ambacho alikuwa ametabiri kwa vinywa vya manabii wake wote, kwamba Al-Masihi atateswa. 19 Tubuni basi mkamgeukie Mwenyezi Mungu, dhambi zenu zifutwe, ili zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwepo kwake Mwenyezi Mungu, 20 naye apate kumtuma Al-Masihi, ambaye ameteuliwa kwa ajili yenu, yaani Isa. 21 Ilimpasa mbingu zimpokee mpaka wakati wa kufanywa upya kila kitu, kama Mwenyezi Mungu alivyoahidi zamani kupitia kwa vinywa vya manabii wake watakatifu. 22 Kwa maana Musa alisema, ‘Bwana Mwenyezi Mungu wenu atawainulia nabii kama mimi kutoka miongoni mwa ndugu zenu. Itawapasa kumtii huyo kwa kila jambo atakalowaambia. 23 Mtu yeyote ambaye hatamsikiliza huyo nabii, atatupiliwa mbali kabisa na watu wake.’
24 “Naam, manabii wote tangu Samweli na waliokuja baada yake, wote walitabiri kuhusu siku hizi. 25 Ninyi ndio wana wa manabii na wa Agano ambalo Mungu alifanya na baba zenu, akimwambia Ibrahimu, ‘Kupitia kwa uzao wako, watu wote wa ulimwengu watabarikiwa.’ 26 Mungu alipomfufua Isa Mwanawe, alimtuma kwenu kwanza, ili awabariki kwa kumgeuza kila mmoja wenu kutoka njia yake mbaya.”
Iliyochaguliwa sasa
Matendo 3: NMM
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018 by Biblica, Inc.
Used with permission.
All rights reserved worldwide.