Matendo 9
9
Kuokoka Kwa Sauli
(Matendo 22:6-16; 26:12-18)
1 Wakati ule ule, Sauli alikuwa bado anazidisha vitisho vya kuua wanafunzi wa Bwana Isa, akamwendea kuhani mkuu, 2 naye akamwomba kuhani mkuu ampe barua za kwenda kwenye masinagogi#9:2 Nyumba za ibada na mafunzo. huko Dameski, ili akimkuta mtu yeyote wa Njia Ile, akiwa mwanaume au mwanamke, aweze kuwafunga na kuwaleta Yerusalemu. 3 Basi akiwa katika safari yake, alipokaribia Dameski, ghafula nuru kutoka mbinguni ikamwangaza kotekote. 4 Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, “Sauli, Sauli, mbona unanitesa?”
5 Sauli akajibu, “U nani wewe, Bwana?”
Ile sauti ikajibu, “Mimi ni Isa unayemtesa.” 6 “Sasa inuka uingie mjini, nawe utaambiwa yakupasayo kutenda.”
7 Watu waliokuwa wakisafiri pamoja na Sauli wakasimama bila kuwa na la kusema, kwa sababu walisikia sauti lakini hawakumwona aliyekuwa akizungumza. 8 Sauli akainuka kutoka pale chini na alipojaribu kufungua macho yake hakuweza kuona kitu chochote. Basi wakamshika mkono wakamwongoza mpaka Dameski. 9Naye kwa muda wa siku tatu alikuwa kipofu naye hakula wala kunywa chochote.
10 Huko Dameski alikuwepo mwanafunzi mmoja jina lake Anania. Bwana Isa alimwita katika maono, “Anania!”
Akajibu, “Mimi hapa, Bwana.”
11 Bwana Isa akamwambia, “Ondoka uende katika barabara iitwayo Nyofu ukaulize katika nyumba ya Yuda mtu kutoka Tarso, jina lake Sauli, kwa maana wakati huu anaomba, 12 katika maono amemwona mtu aitwaye Anania akija na kuweka mikono juu yake ili apate kuona tena.”
13 Anania akajibu, “Bwana Isa, nimesikia kutoka kwa watu wengi habari nyingi kuhusu mtu huyu na madhara yote aliyowatendea watakatifu wako huko Yerusalemu. 14 Naye amekuja hapa Dameski akiwa na mamlaka kutoka kwa viongozi wa makuhani ili awakamate wote wanaotaja jina lako.”
15 Lakini Bwana Isa akamwambia Anania, “Nenda! Mtu huyu ni chombo changu kiteule nilichokichagua, apate kulichukua Jina langu kwa watu wa Mataifa na wafalme wao na mbele ya watu wa Israeli. 16 Nami nitamwonyesha jinsi impasavyo kuteseka kwa ajili ya Jina langu.”
17 Kisha Anania akaenda kwenye ile nyumba, akaingia ndani. Akaweka mikono yake juu ya Sauli akasema, “Ndugu Sauli, Bwana Isa aliyekutokea njiani amenituma kwako ili upate kuona tena na ujazwe Roho wa Mwenyezi Mungu.” 18 Ghafula vitu kama magamba vikaanguka chini, kutoka machoni mwa Sauli, akapata kuona tena. Akasimama, akabatizwa. 19 Baada ya kula chakula, akapata nguvu tena. Sauli akakaa siku kadhaa pamoja na wanafunzi huko Dameski.
Sauli Ahubiri Dameski
20 Papo hapo akaanza kuhubiri kwenye masinagogi kwamba “Isa Al-Masihi ni Mwana wa Mungu.#9:20 Yaani Mwana wa asili moja na Mwenyezi Mungu (Yn 1:1-2), wa kiroho, bali si wa kimwili.” 21 Watu wote waliomsikia Sauli walishangaa na kuuliza, “Huyu si yule mtu aliyesababisha maangamizi makuu huko Yerusalemu miongoni mwa watu waliolitaja jina hili? Naye si amekuja hapa kwa kusudi la kuwakamata na kuwapeleka wakiwa wafungwa mbele ya viongozi wa makuhani?” 22 Sauli akazidi kuwa hodari na kuwashangaza Wayahudi walioishi Dameski kwa kuthibitisha kuwa Isa ndiye Al-Masihi.
23 Baada ya siku nyingi kupita, Wayahudi wakafanya shauri kumuua Sauli. 24 Lakini shauri lao likajulikana kwa Sauli. Wayahudi wakawa wanalinda malango yote ya mji, usiku na mchana ili wapate kumuua. 25 Lakini wafuasi wake wakamchukua usiku wakamshusha akiwa ndani ya kapu kupitia mahali penye nafasi ukutani.
Sauli Huko Yerusalemu
26 Sauli alipofika Yerusalemu akajaribu kujiunga na wanafunzi lakini wote walimwogopa, kwa maana hawakuamini kwamba kweli naye alikuwa mwanafunzi. 27 Lakini Barnaba akamchukua, akampeleka kwa wale mitume. Akawaeleza jinsi Sauli akiwa njiani alivyomwona Bwana Isa, jinsi Bwana Isa alivyosema naye, na jinsi alivyohubiri kwa ujasiri kwa jina la Isa huko Dameski. 28 Kwa hiyo Sauli akakaa nao akitembea kwa uhuru kila mahali huko Yerusalemu, akihubiri kwa ujasiri katika jina la Bwana Isa. 29 Alinena na kuhojiana na Wayahudi wenye asili ya Kiyunani lakini wao walijaribu kumuua. 30 Wale ndugu walipopata habari wakampeleka hadi Kaisaria, wakamsafirisha kwenda Tarso.
31 Ndipo waumini katika Uyahudi wote, Galilaya na Samaria wakafurahia wakati wa amani. Wakatiwa nguvu, na kwa faraja ya Roho wa Mwenyezi Mungu, idadi yao ikazidi kuongezeka, na wakaendelea kudumu katika kumcha Bwana Isa.
Matendo Ya Petro
(9:32–12:25)
Kuponywa Kwa Ainea
32 Petro alipokuwa akisafiri sehemu mbalimbali, alikwenda kuwatembelea watakatifu walioishi huko Lida. 33Huko alimkuta mtu mmoja aitwaye Ainea, ambaye alikuwa amepooza na kwa muda wa miaka minane alikuwa hajaondoka kitandani. 34 Petro akamwambia, “Ainea, Isa Al-Masihi anakuponya, inuka utandike kitanda chako.” Mara Ainea akainuka. 35 Watu wote wa Lida na Sharoni walipomwona Ainea akitembea wakamgeukia Bwana Isa.
Petro Amfufua Dorkasi
36 Huko Yafa palikuwa na mwanafunzi jina lake Tabitha (ambalo kwa Kiyunani ni Dorkasi#9:36 Tabitha kwa Kiaramu na Dorkasi kwa Kiaramu yote yamaanisha Paa.). Huyu alikuwa mkarimu sana, akitenda mema na kuwasaidia maskini. 37 Wakati huo akaugua, akafa na wakiisha kuuosha mwili wake wakauweka katika chumba cha ghorofani. 38 Kwa kuwa Yafa hapakuwa mbali sana na Lida, wanafunzi waliposikia kwamba Petro yuko huko waliwatuma watu wawili kwake ili kumwomba, “Tafadhali njoo huku pasipo kukawia.”
39 Kwa hiyo Petro akainuka akaenda nao, naye alipowasili, wakampeleka hadi kwenye chumba cha ghorofani alipokuwa amelazwa. Wajane wengi walisimama karibu naye wakilia na kuonyesha majoho na nguo nyingine ambazo Dorkasi alikuwa amewashonea alipokuwa pamoja nao.
40 Petro akawatoa wote nje ya kile chumba, kisha akapiga magoti akaomba, akaugeukia ule mwili akasema, “Tabitha, inuka.” Akafumbua macho yake na alipomwona Petro, akaketi. 41 Petro akamshika mkono akamwinua, ndipo akawaita wale watakatifu na wajane akamkabidhi kwao akiwa hai. 42 Habari hizi zikajulikana sehemu zote za Yafa na watu wengi wakamwamini Bwana Isa. 43 Petro akakaa Yafa kwa siku nyingi akiishi na Simoni mtengenezaji ngozi.
Iliyochaguliwa sasa
Matendo 9: NMM
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018 by Biblica, Inc.
Used with permission.
All rights reserved worldwide.