Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 39

39
Yusufu Na Mke Wa Potifa
1 Wakati huu Yusufu alikuwa amechukuliwa mpaka Misri. Mmisri aliyeitwa Potifa aliyekuwa mmojawapo wa maafisa wa Farao, mkuu wa ulinzi, akamnunua Yusufu kutoka kwa Waishmaeli waliomleta Misri.
2 bwana alikuwa pamoja na Yusufu, naye akastawi, Yusufu akaishi nyumbani kwa bwana wake Mmisri. 3 Potifa alipoona kuwa bwana alikuwa pamoja na Yusufu na kwamba bwana alimfanikisha kwa kila kitu alichokifanya, 4 Yusufu alipata kibali machoni pa Potifa, akamfanya mhudumu wake. Potifa akamweka kuwa msimamizi wa nyumba yake, naye akamkabidhi kuwa mwangalizi wa kila kitu alichokuwa nacho. 5 Kuanzia wakati huo Potifa alipomweka Yusufu kuwa msimamizi wa nyumba na mali zake zote alizokuwa nazo, bwana aliibariki nyumba ya Mmisri huyo kwa sababu ya Yusufu. Baraka ya bwana ilikuwa juu ya kila kitu alichokuwa nacho Potifa, nyumbani na shambani. 6Kwa hiyo Potifa akamwachia Yusufu uangalizi wa kila kitu alichokuwa nacho, Yusufu alipokuwa katika uongozi, Potifa hakuwa na sababu ya kujishughulisha na kitu chochote isipokuwa chakula alichokula.
Yusufu alikuwa mwenye umbo zuri na sura ya kuvutia; 7baada ya kitambo mke wa Potifa akamtamani Yusufu, akamwambia, “Njoo, ukutane nami kimwili!”
8 Lakini Yusufu akakataa. Akamwambia yule mwanamke, “Mimi nikiwa katika uongozi, bwana wangu hahusiki na kitu chochote katika nyumba hii, kila kitu alicho nacho amenikabidhi. 9 Hapa nyumbani hakuna aliye mkuu kuliko mimi. Bwana wangu hakunizuilia kitu chochote isipokuwa wewe, kwa kuwa wewe ni mke wake. Nitawezaje basi kufanya uovu huu na kutenda dhambi dhidi ya Mungu?” 10Ingawa yule mwanamke aliendelea kumshawishi Yusufu siku baada ya siku, Yusufu alikataa kukutana naye kimwili wala kukaa karibu naye.
11 Siku moja Yusufu akaingia ndani ya nyumba kufanya kazi zake, wala hapakuwepo na mfanyakazi yeyote ndani ya nyumba. 12 Mke wa Potifa akashika vazi Yusufu alilokuwa amevaa, akamwambia, “Njoo tukutane kimwili!” Lakini Yusufu akaacha vazi lake mkononi mwa huyo mwanamke, akatoka nje ya nyumba akikimbia.
13Yule mwanamke alipoona kwamba Yusufu amemwachia vazi lake mkononi na kukimbilia nje ya nyumba, 14 akawaita watumishi wake wa nyumbani, akawaambia, “Tazameni! Huyu Mwebrania ameletwa hapa kutudhihaki! Aliingia hapa ndani ili akutane nami kimwili, lakini nikapiga kelele. 15Aliposikia kelele za kuomba msaada, akaacha vazi lake kando yangu akakimbilia nje.”
16Yule mwanamke akaliweka lile vazi karibu naye mpaka Potifa aliporudi nyumbani. 17 Ndipo akamweleza kisa hiki, akisema: “Yule mtumwa wa Kiebrania uliyetuletea alinijia ili kunidhihaki. 18Lakini mara nilipopiga kelele kuomba msaada, akaliacha vazi lake kando yangu akakimbia nje ya nyumba.”
19Potifa aliposikia kisa hiki mkewe alichomweleza, akisema, “Hivi ndivyo mtumwa wako alivyonitenda.” Hasira ya Potifa ikawaka. 20 Potifa akamchukua Yusufu na kumweka gerezani, mahali ambapo wahalifu wa mfalme walikuwa wamefungwa.
Lakini wakati Yusufu alipokuwa huko gerezani, 21 bwana alikuwa pamoja naye, akamhurumia na kumpa kibali mbele ya msimamizi wa gereza. 22Kwa hiyo msimamizi wa gereza akamweka Yusufu awe mkuu wa wafungwa pamoja na kusimamia yote ambayo yalitendeka mle gerezani. 23 Msimamizi wa gereza hakujishughulisha tena na kitu chochote kilichokuwa chini ya uangalizi wa Yusufu, kwa sababu bwana alikuwa pamoja na Yusufu akimfanikisha kwa kila alichofanya.

Iliyochaguliwa sasa

Mwanzo 39: NMM

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha