Mwanzo 46
46
Yakobo Aenda Misri
1Hivyo Israeli akaondoka na vyote vilivyokuwa mali yake, naye alipofika Beer-Sheba, akamtolea dhabihu Mungu wa Isaka baba yake.
2 Mungu akanena na Israeli katika maono usiku na kusema, “Yakobo! Yakobo!”
Akajibu, “Mimi hapa.”
3 Mungu akamwambia, “Mimi ndimi Mungu wa baba yako, usiogope kushuka Misri, kwa maana huko nitakufanya taifa kubwa. 4 Nitashuka Misri pamoja nawe, nami hakika nitakurudisha tena Kanaani. Mikono ya Yusufu mwenyewe ndiyo itakayofunga macho yako.”
5 Ndipo Yakobo akaondoka Beer-Sheba nao wana wa Israeli wakamchukua baba yao Yakobo na watoto wao na wake zao katika magari ya kukokotwa yale Farao aliyokuwa amempelekea kumsafirisha. 6 Wakachukua pia mifugo yao na mali walizokuwa wamezipata Kanaani, Yakobo na uzao wake wote wakashuka Misri. 7Akawachukua wanawe na binti zake, wajukuu wake wa kiume na wa kike, yaani uzao wake wote mpaka Misri.
8Haya ndiyo majina ya wana wa Israeli (Yakobo na wazao wake), waliokwenda Misri:
Reubeni mzaliwa wa kwanza wa Yakobo.
9Wana wa Reubeni ni:
Hanoki, Palu, Hesroni na Karmi.
10 Wana wa Simeoni ni:
Yemueli, Yamini, Ohadi, Yakini, Sohari na Shauli mwana wa mwanamke Mkanaani.
11Wana wa Lawi ni:
Gershoni, Kohathi na Merari.
12 Wana wa Yuda ni:
Eri, Onani, Shela, Peresi na Zera (lakini Eri na Onani walifariki katika nchi ya Kanaani).
Wana wa Peresi ni:
Hesroni na Hamuli.
13Wana wa Isakari ni:
Tola, Puva, Yashubu na Shimroni.
14 Wana wa Zabuloni ni:
Seredi, Eloni na Yaleeli.
15 Hawa ndio wana wa Lea aliomzalia Yakobo huko Padan-Aramu pamoja na binti yake Dina. Jumla ya wanawe na binti zake walikuwa thelathini na watatu.
16 Wana wa Gadi ni:
Sefoni, Hagi, Shuni, Esboni, Eri, Arodi na Areli.
17 Wana wa Asheri ni:
Imna, Ishva, Ishvi na Beria.
Dada yao alikuwa Sera.
Wana wa Beria ni:
Heberi na Malkieli.
18Hawa ndio watoto Zilpa aliomzalia Yakobo, ambao Labani alimpa binti yake Lea; jumla yao walikuwa kumi na sita.
19Wana wa Raheli mke wa Yakobo ni:
Yusufu na Benyamini.
20 Huko Misri, Asenathi binti wa Potifera, aliyekuwa kuhani wa mji wa Oni,#46:20 Yaani Heliopoli (Mji wa Jua). alimzalia Yusufu wana wawili, Manase na Efraimu.
21 Wana wa Benyamini ni:
Bela, Bekeri, Ashbeli, Gera, Naamani, Ehi, Roshi, Mupimu, Hupimu na Ardi.
22Hawa ndio wana wa Raheli aliomzalia Yakobo; jumla yao ni kumi na wanne.
23Mwana wa Dani ni:
Hushimu.
24 Wana wa Naftali ni:
Yaseeli, Guni, Yeseri na Shilemu.
25 Hawa walikuwa wana wa Bilha aliomzalia Yakobo, ambaye Labani alikuwa amempa Raheli binti yake; jumla yao walikuwa saba.
26 Wote waliokwenda Misri pamoja na Yakobo, waliokuwa wazao wake hasa pasipo kuhesabu wakwe zake, walikuwa watu sitini na sita. 27 Pamoja na wana wawili waliozaliwa na Yusufu huko Misri, jumla yote ya jamaa ya Yakobo, waliokwenda Misri, walikuwa sabini.
28 Basi Yakobo akamtanguliza Yuda aende kwa Yusufu ili amwelekeze njia ya Gosheni. Walipofika nchi ya Gosheni, 29 gari kubwa zuri la Yusufu liliandaliwa, naye akaenda Gosheni kumlaki baba yake Israeli. Mara Yusufu alipofika mbele yake, alimkumbatia baba yake, akalia kwa muda mrefu.
30 Israeli akamwambia Yusufu, “Sasa niko tayari kufa, kwa kuwa nimejionea mwenyewe kwamba bado uko hai.”
31 Ndipo Yusufu akawaambia ndugu zake na watu wa nyumbani mwa baba yake, “Nitapanda kwa Farao na kumwambia, ‘Ndugu zangu na watu wa nyumbani mwa baba yangu, waliokuwa wakiishi katika nchi ya Kanaani, wamekuja kwangu. 32 Watu hao ni wachunga mifugo, huchunga mifugo, wamekuja na makundi ya kondoo, mbuzi na ng’ombe pamoja na kila kitu walicho nacho.’ 33 Farao atakapowaita na kuwaulizeni, ‘Kazi yenu ni nini?’ 34 Mjibuni, ‘Watumwa wako wamekuwa wachunga mifugo tangu ujana wetu mpaka sasa, kama baba zetu walivyofanya.’ Ndipo mtakaporuhusiwa kukaa katika nchi ya Gosheni, kwa kuwa wachunga mifugo wote ni chukizo kwa Wamisri.”
Iliyochaguliwa sasa
Mwanzo 46: NMM
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018 by Biblica, Inc.
Used with permission.
All rights reserved worldwide.