Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohana 17

17
Isa Ajiombea Mwenyewe
1 Baada ya Isa kusema haya, alitazama kuelekea mbinguni akawaombea na kusema:
“Baba,#17:1 Jina Baba linaonyesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. saa imewadia. Umtukuze Mwanao, ili Mwanao apate kukutukuza wewe. 2 Kwa kuwa umempa mamlaka juu ya wote wenye mwili ili awape uzima wa milele wale uliompa. 3 Nao uzima wa milele ndio huu, wakujue wewe uliye Mwenyezi Mungu wa pekee wa kweli, na Isa Al-Masihi uliyemtuma. 4 Nimekutukuza wewe duniani kwa kuitimiza ile kazi uliyonipa niifanye. 5 Hivyo sasa, Baba, unitukuze mbele zako kwa ule utukufu niliokuwa nao pamoja na wewe kabla ulimwengu haujakuwepo.
Isa Awaombea Wanafunzi Wake
6 “Nimelidhihirisha jina lako kwa wale ulionipa kutoka ulimwengu. Walikuwa wako, nawe ukanipa mimi, nao wamelitii neno lako. 7Sasa wamejua ya kuwa vyote ulivyonipa vimetoka kwako, 8 kwa kuwa maneno yale ulionipa nimewapa wao, nao wameyapokea na kujua kwamba kweli nimetoka kwako, nao wameamini kuwa wewe ulinituma. 9 Ninawaombea wao. Mimi siuombei ulimwengu, bali nawaombea wale ulionipa kwa sababu wao ni wako. 10 Wote walio wangu ni wako na walio wako ni wangu, nami nimetukuzwa ndani yao. 11 Mimi sasa simo tena ulimwenguni, lakini wao bado wamo ulimwenguni, nami naja kwako. Baba Mtakatifu, uwalinde kwa uweza wa jina lako ulilonipa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo wamoja. 12 Nilipokuwa pamoja nao, niliwalinda, wakawa salama kwa lile jina ulilonipa. Hakuna hata mmoja aliyepotea, isipokuwa yule aliyekusudiwa upotevu, ili Maandiko yapate kutimia.
13 “Lakini sasa naja kwako, nami ninasema mambo haya wakati bado nikiwa ulimwenguni, ili wawe na furaha yangu kamili ndani yao. 14 Nimewapa neno lako, nao ulimwengu umewachukia kwa kuwa wao si wa ulimwengu kama mimi nisivyo wa ulimwengu huu. 15 Siombi kwamba uwaondoe ulimwenguni, bali uwalinde dhidi ya yule mwovu. 16 Wao si wa ulimwengu huu, kama vile mimi nisivyo wa ulimwengu. 17 Uwatakase kwa ile kweli, neno lako ndilo kweli. 18 Kama vile ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami nawatuma vivyo hivyo. 19 Kwa ajili yao najiweka wakfu ili wao nao wapate kutakaswa katika ile kweli.
Isa Awaombea Wote Wamwaminio
20 “Siwaombei hawa peke yao, bali nawaombea na wale wote watakaoniamini kupitia neno lao 21 ili wawe na umoja kama vile wewe Baba ulivyo ndani yangu na mimi nilivyo ndani yako, wao nao wawe ndani yetu, ili ulimwengu upate kuamini ya kuwa wewe ndiwe uliyenituma mimi. 22 Utukufu ule ulionipa nimewapa wao, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo wamoja. 23 Mimi ndani yako na wewe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja na ulimwengu upate kujua ya kuwa umenituma, nami nimewapenda wao kama unavyonipenda mimi.
24 “Baba, shauku yangu ni kwamba, wale ulionipa wawe pamoja nami pale nilipo, ili waweze kuuona utukufu wangu, yaani, utukufu ule ulionipa kwa kuwa ulinipenda hata kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu.
25 “Baba Mwenye Haki, ingawa ulimwengu haukujui, mimi ninakujua, nao wanajua ya kuwa umenituma. 26Nimefanya jina lako lijulikane kwao nami nitaendelea kufanya lijulikane, ili kwamba upendo ule unaonipenda mimi uwe ndani yao na mimi mwenyewe nipate kuwa ndani yao.”

Iliyochaguliwa sasa

Yohana 17: NMM

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia