18
Isa Akamatwa
(Mathayo 26:47-56; Marko 14:43-50; Luka 22:47-53)
1 Isa alipomaliza kuomba, akaondoka na wanafunzi wake wakavuka Bonde la Kidroni. Upande wa pili palikuwa na bustani, yeye na wanafunzi wake wakaingia humo.
2 Basi Yuda, yule aliyemsaliti alipafahamu mahali hapo kwani Isa alikuwa akikutana humo na wanafunzi wake mara kwa mara. 3 Hivyo Yuda akaja bustanini. Aliongoza kikosi cha askari wa Kirumi, na baadhi ya maafisa kutoka kwa viongozi wa makuhani na Mafarisayo.#18:3 Kundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli. Nao walikuwa wamechukua taa, mienge na silaha.
4 Isa akijua yale yote yatakayompata, akajitokeza mbele yao akawauliza, “Mnamtafuta nani?”
5 Wao wakamjibu, “Isa Al-Nasiri.”
Isa akawajibu, “Mimi ndiye.” Yuda, yule aliyemsaliti alikuwa amesimama pamoja nao. 6Isa alipowaambia, “Mimi ndiye,” walirudi nyuma na kuanguka chini!
7 Akawauliza tena, “Mnamtafuta nani?”
Nao wakamjibu, “Isa Al-Nasiri.”
8Isa akawaambia, “Nimekwisha kuwaambia kuwa, mimi ndiye; kwa hiyo kama mnanitafuta mimi, waacheni hawa watu waende zao.” 9 Hii ilikuwa ili litimie lile neno alilosema, “Sikumpoteza hata mmoja miongoni mwa wale ulionipa.”
10 Simoni Petro, aliyekuwa na upanga, akaufuta na kumkata sikio la kuume mtumishi wa kuhani mkuu. Jina la mtumishi huyo aliitwa Malko.
11 Isa akamwambia Petro, “Rudisha upanga wako kwenye ala yake. Je, hainipasi kukinywea kikombe alichonipa Baba?#18:11 Jina Baba linaonyesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu.”
Isa Mbele Ya Kuhani Mkuu
12 Hivyo wale askari, wakiwa pamoja na majemadari wao na maafisa wa Wayahudi, wakamkamata Isa na kumfunga. 13 Kwanza wakampeleka kwa Anasi, mkwewe Kayafa, aliyekuwa kuhani mkuu mwaka ule. 14 Kayafa ndiye alikuwa amewashauri Wayahudi kwamba imempasa mtu mmoja kufa kwa ajili ya watu.
Petro Anamkana Isa
(Mathayo 26:69-70; Marko 14:55-64; Luka 22:66-71)
15 Simoni Petro pamoja na mwanafunzi mwingine walikuwa wakimfuata Isa. Huyu mwanafunzi mwingine alikuwa anafahamika kwa kuhani mkuu, hivyo aliingia ndani ya ukumbi pamoja na Isa. 16 Lakini Petro alisimama nje karibu na lango, ndipo yule mwanafunzi mwingine, aliyejulikana na kuhani mkuu, akazungumza na msichana aliyekuwa analinda lango, akamruhusu Petro aingie ndani.
17 Yule msichana akamuuliza Petro, “Je, wewe pia si mmoja wa wanafunzi wa mtu huyu?”
Petro akajibu, “Sio mimi.”
18 Wale watumishi na askari walikuwa wamesimama wakiota moto wa makaa kwa sababu palikuwa na baridi, Petro naye alikuwa amesimama pamoja nao akiota moto.
Kuhani Mkuu Amhoji Isa
19Wakati huo kuhani mkuu akawa anamuuliza Isa kuhusu wanafunzi wake na mafundisho yake.
20 Isa akamjibu, “Nimekuwa nikizungumza waziwazi mbele ya watu wote. Siku zote nimefundisha katika masinagogi#18:20 Nyumba za ibada na mafunzo. na Hekaluni, mahali ambapo Wayahudi wote hukusanyika. Sikusema jambo lolote kwa siri. 21Mbona unaniuliza mimi maswali? Waulize wale walionisikia yale niliyowaambia. Wao wanajua niliyosema.”
22 Alipomaliza kusema hayo, mmoja wa askari aliyekuwa amesimama karibu naye, akampiga Isa kofi usoni, kisha akasema, “Je, hivyo ndivyo unavyomjibu kuhani mkuu?”
23 Isa akamjibu akasema, “Kama nimesema jambo baya, shuhudia huo ubaya niliousema. Lakini kama nimesema yaliyo kweli, mbona umenipiga?” 24 Ndipo Anasi akampeleka Isa kwa kuhani mkuu Kayafa, akiwa bado amefungwa.
Petro Amkana Isa Tena
(Mathayo 26:71-75; Marko 14:69-72; Luka 22:58-62)
25 Wakati huo Simoni Petro alikuwa amesimama akiota moto. Baadhi ya wale waliokuwepo wakamuuliza, “Je, wewe si mmoja wa wanafunzi wake?”
Petro akakana, akasema, “Sio mimi.”
26 Mmoja wa watumishi wa kuhani mkuu, ndugu yake yule mtu ambaye Petro alikuwa amemkata sikio, akamuuliza, “Je, mimi sikukuona kule bustanini ukiwa na Isa?” 27 Kwa mara nyingine tena Petro akakana, naye jogoo akawika wakati huo huo.
Isa Apelekwa Kwa Pilato
(Mathayo 27:1-2, 11-14; Marko 15:1-5; Luka 23:1-5)
28 Ndipo Wayahudi wakamchukua Isa kutoka kwa Kayafa na kumpeleka kwenye jumba la kifalme la mtawala wa Kirumi.#18:28 Jumba la mfalme la mtawala wa Kirumi lilikuwa linaitwa Praitorio. Wakati huo ilikuwa ni alfajiri, ili kuepuka kuwa najisi kwa taratibu za ibada, Wayahudi hawakuingia ndani kwa sababu ya sheria za Kiyahudi. Wangehesabiwa kuwa najisi kama wangeingia nyumbani mwa mtu asiye Myahudi na wasingeruhusiwa kushiriki katika Sikukuu ya Pasaka. 29Hivyo Pilato akatoka nje walikokuwa akawauliza, “Mmeleta mashtaka gani kumhusu mtu huyu?”
30Wao wakamjibu, “Kama huyu mtu hakuwa mhalifu tusingemleta kwako.”
31Pilato akawaambia, “Basi mchukueni ninyi mkamhukumu kwa kufuata sheria zenu.”
Wayahudi wakamjibu, “Sisi haturuhusiwi kutoa hukumu ya kifo kwa mtu yeyote.” 32 Walisema hivyo ili yale maneno aliyosema Isa kuhusu kifo atakachokufa yapate kutimia.
33 Kwa hiyo Pilato akaingia ndani ya jumba la kifalme, akamwita Isa, akamuuliza, “Wewe ndiye mfalme wa Wayahudi?”
34 Isa akamjibu, “Je, unauliza swali hili kutokana na mawazo yako mwenyewe, au uliambiwa na watu kunihusu mimi?”
35 Pilato akamjibu, “Mimi si Myahudi, ama sivyo? Taifa lako mwenyewe na viongozi wa makuhani wamekukabidhi kwangu. Umefanya kosa gani?”
36 Isa akajibu, “Ufalme wangu si wa ulimwengu huu. Ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, wafuasi wangu wangenipigania ili nisitiwe mikononi mwa Wayahudi. Lakini kama ilivyo, ufalme wangu hautoki hapa ulimwenguni.”
37 Pilato akamuuliza, “Kwa hiyo wewe ni mfalme?” Isa akajibu, “Wewe wasema kwamba mimi ni mfalme. Kwa kusudi hili nilizaliwa, na kwa ajili ya hili nilikuja ulimwenguni, ili niishuhudie kweli. Mtu yeyote aliye wa kweli husikia sauti yangu.”
38 Pilato akamuuliza Isa, “Kweli ni nini?” Baada ya kusema haya Pilato akaenda nje tena akawaambia wale viongozi wa Wayahudi waliomshtaki Isa, “Sioni kosa lolote alilotenda mtu huyu. 39 Lakini ninyi mna desturi yenu kwamba wakati wa Pasaka nimwachie huru mfungwa mmoja mnayemtaka. Je, mnataka niwafungulie huyu ‘Mfalme wa Wayahudi’?”
40 Wao wakapiga kelele wakisema, “Si huyu mtu, bali tufungulie Baraba!” Yule Baraba alikuwa mnyang’anyi.