Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohana 21

21
Isa Awatokea Wanafunzi Saba
1 Baada ya haya Isa akawatokea tena wanafunzi wake kando ya Bahari ya Tiberia.#21:1 Yaani Bahari ya Galilaya. Yeye alijionyesha kwao hivi: 2 Simoni Petro, Tomaso aitwaye Didimasi, yaani Pacha, Nathanaeli wa Kana ya Galilaya, wana wa Zebedayo na wanafunzi wengine wawili walikuwa pamoja. 3 Simoni Petro akawaambia wenzake, “Mimi naenda kuvua samaki.” Nao wakamwambia, “Tutakwenda pamoja nawe.” Wakatoka, wakaingia ndani ya mashua, lakini usiku ule hawakupata chochote.
4 Mara baada ya kupambazuka, Isa akasimama ufuoni, lakini wanafunzi hawakumtambua kwamba alikuwa Isa.
5 Isa akawaambia, “Wanangu, je, mna samaki wowote?”
Wakamjibu, “La.”
6 Akawaambia, “Shusheni nyavu upande wa kuume wa mashua yenu nanyi mtapata samaki.” Wakashusha nyavu na tazama wakapata samaki wengi mno hata wakashindwa kuvutia zile nyavu zilizojaa samaki ndani ya mashua.
7 Yule mwanafunzi aliyependwa na Isa akamwambia Petro, “Huyu ni Bwana Isa!” Simoni Petro aliposikia kwamba ni Bwana Isa, akajifunga nguo yake (kwa kuwa alikuwa ameitoa), naye akajitosa baharini. 8Wale wanafunzi wengine wakaja kwa ile mashua huku wakikokota ule wavu uliyojaa samaki, maana hawakuwa mbali na nchi kavu, ilikuwa yapata dhiraa 200#21:8 Dhiraa 200 ni kama mita 90. 9 Walipofika ufuoni, wakaona moto wa makaa na samaki wakiokwa juu yake na mikate.
10Isa akawaambia, “Leteni baadhi ya hao samaki mliovua sasa hivi.”
11Simoni Petro akapanda kwenye mashua na kuukokota ule wavu pwani. Ulikuwa umejaa samaki wakubwa 153. Ingawa samaki walikuwa wengi kiasi hicho, ule wavu haukuchanika. 12 Isa akawaambia, “Njooni mpate kifungua kinywa.” Hakuna hata mmoja wa wanafunzi aliyethubutu kumuuliza, “Wewe ni nani?” Kwa sababu walijua ya kuwa ni Bwana Isa. 13 Basi Isa akaja, akachukua ule mkate, akawapa na vivyo hivyo akawagawia pia wale samaki. 14 Hii ilikuwa mara ya tatu Isa kuwatokea wanafunzi wake baada yake kufufuliwa kutoka kwa wafu.
Isa Amuuliza Petro Kama Anampenda
15 Walipokwisha kula, Isa akamuuliza Simoni Petro, “Je, Simoni mwana wa Yohana, unanipenda kweli kuliko hawa?”
Yeye akamjibu, “Ndiyo Bwana, wewe unajua ya kuwa ninakupenda.”
Isa akamwambia, “Lisha wana-kondoo wangu.”
16 Isa akamwambia tena, “Simoni, mwana wa Yohana, wanipenda?”
Petro akamjibu, “Ndiyo Bwana, wewe unajua ya kuwa ninakupenda.”
Isa akamwambia, “Chunga kondoo zangu.”
17 Kwa mara ya tatu Isa akamuuliza Petro, “Simoni mwana wa Yohana, unanipenda?”
Petro akahuzunika sana kwa kuwa Isa alimuuliza mara ya tatu, “Unanipenda?” Akamjibu, “Bwana, wewe unajua yote, unajua ya kuwa ninakupenda.”
Isa akamwambia, “Lisha kondoo wangu. 18Amin, amin nakuambia, ulipokuwa kijana ulivaa na kwenda unakotaka, lakini utakapokuwa mzee utanyoosha mikono yako na mtu mwingine atakuvika na kukupeleka usipotaka kwenda.” 19 Isa alisema haya ili kuashiria ni kifo cha aina gani Petro atakachomtukuza nacho Mungu. Kisha Isa akamwambia Petro, “Nifuate!”
20 Petro akageuka, akamwona yule mwanafunzi aliyependwa na Isa akiwafuata. (Huyu ndiye yule mwanafunzi aliyeegama kifuani mwa Isa walipokula naye chakula cha mwisho na kuuliza, “Bwana, ni nani atakayekusaliti?”) 21Petro alipomwona huyo mwanafunzi, akamuuliza Isa, “Bwana, na huyu je?”
22 Isa akamjibu, “Ikiwa nataka aishi mpaka nitakaporudi, inakuhusu nini? Wewe inakupasa unifuate!” 23 Kwa sababu ya maneno haya ya Isa, uvumi ukaenea miongoni mwa ndugu kwamba huyu mwanafunzi hangekufa. Lakini Isa hakusema kuwa hangekufa. Yeye alisema tu kwamba, “Ikiwa nataka aishi mpaka nitakaporudi, inakuhusu nini?”
24 Huyu ndiye yule mwanafunzi anayeshuhudia mambo haya na ndiye ambaye ameandika habari hizi. Nasi tunajua ya kuwa ushuhuda wake ni kweli.
25 Lakini kuna mambo mengine mengi ambayo Isa alifanya. Kama yote yangeliandikwa, nadhani hata ulimwengu wote usingekuwa na nafasi ya kutosha kuweka vitabu vyote ambavyo vingeandikwa. Amen.

Iliyochaguliwa sasa

Yohana 21: NMM

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia