1 Wakorintho 1:18-25
1 Wakorintho 1:18-25 BHN
Maana ujumbe kuhusu kifo cha Kristo msalabani ni jambo la kipumbavu kwa wale walio katika mkumbo wa kupotea, lakini kwetu sisi tulio katika njia ya wokovu, ujumbe huo ni nguvu ya Mungu. Maana Maandiko Matakatifu yasema: “Nitaiharibu hekima yao wenye hekima, na elimu ya wataalamu nitaitupilia mbali.” Yu wapi basi, mwenye hekima? Yu wapi basi, mwalimu wa sheria? Naye bingwa wa mabishano wa nyakati hizi yuko wapi? Mungu ameifanya hekima ya ulimwengu kuwa upumbavu. Maana, kadiri ya hekima ya Mungu, watu hawawezi kumjua Mungu kwa njia ya hekima yao wenyewe. Badala yake, Mungu amependa kuwaokoa wale wanaoamini kwa njia ya kile ambacho wenye hekima wanakiona kuwa ni upumbavu, yaani ujumbe tunaohubiri. Wayahudi wanataka ishara, na Wagiriki wanatafuta hekima; lakini sisi tunamhubiri Kristo aliyesulubiwa. Kwa Wayahudi jambo hili ni kikwazo, na kwa watu wa mataifa ni upumbavu; lakini kwa wale walioitwa, Wayahudi kwa Wagiriki, Kristo ni nguvu ya Mungu na hekima ya Mungu. Maana kinachoonekana kuwa ni upumbavu wa Mungu, kina busara kuliko hekima ya binadamu; na kinachoonekana kuwa ni udhaifu wa Mungu, kina nguvu kuliko nguvu za binadamu.