Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wakorintho 12:12-27

1 Wakorintho 12:12-27 BHN

Kama vile mwili ulivyo mmoja wenye viungo vingi, na viungo hivyo vyote – ingawaje ni vingi – hufanya mwili mmoja, ndivyo ilivyo pia kwa Kristo. Maana sisi, tukiwa Wayahudi au watu wa mataifa mengine, watumwa au watu huru, sote tumebatizwa kwa Roho mmoja katika mwili huo mmoja; na sote tukanyweshwa Roho huyo mmoja. Mwili hauna kiungo kimoja tu, bali una viungo vingi. Kama mguu ungejisemea: “Kwa kuwa mimi si mkono, basi mimi si mali ya mwili,” je, ungekoma kuwa sehemu ya mwili? La hasha! Kama sikio lingejisemea: “Kwa vile mimi si jicho, basi mimi si mali ya mwili,” je, kwa hoja hiyo lingekoma kuwa sehemu ya mwili? La! Kama mwili wote ungekuwa jicho, sikio lingekuwa wapi? Na kama mwili wote ungekuwa sikio, mtu angewezaje kunusa? Lakini kama ilivyo, Mungu alizipanga sehemu hizo tofauti katika mwili kama alivyopenda. Kama sehemu zote zingekuwa kiungo kimoja, mwili ungekuwa wapi? Ukweli ni kwamba, sehemu za mwili ni nyingi, lakini mwili ni mmoja. Basi, jicho haliwezi kuuambia mkono: “Sikuhitaji wewe,” wala kichwa hakiwezi kuiambia miguu: “Siwahitaji nyinyi.” Zaidi ya hayo, inaonekana kwamba sehemu zile za mwili zinazoonekana kuwa ni dhaifu ndizo zilizo muhimu zaidi. Tena, viungo vile tunavyovifikiria kuwa havistahili heshima kubwa, ndivyo tunavyovitunza kwa uangalifu zaidi; viungo vya mwili ambavyo havionekani kuwa vizuri sana, huhifadhiwa zaidi, ambapo viungo vingine havihitaji kushughulikiwa. Mungu mwenyewe ameuweka mwili katika mpango, akakipa heshima zaidi kiungo kile kilichopungukiwa heshima, ili kusiweko na utengano katika mwili, bali viungo vyote vishughulikiane. Kama kiungo kimoja kinaumia viungo vyote huumia pamoja nacho. Kiungo kimoja kikisifiwa viungo vingine vyote hufurahi pamoja nacho. Basi, nyinyi nyote ni mwili wa Kristo; kila mmoja wenu ni kiungo cha mwili huo.