Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 1:22-37

1 Wafalme 1:22-37 BHN

Wakati Bathsheba alipokuwa akizungumza na mfalme, nabii Nathani aliingia ikulu. Nao watu wakamwambia mfalme, “Nabii Nathani yuko hapa.” Naye alipomfikia mfalme, alimwinamia mfalme mpaka uso ukafika chini udongoni. Ndipo Nathani aliposema, “Bwana wangu, je, ulisema, ‘Adoniya atatawala baada yangu na atakaa juu ya kiti changu cha enzi?’ Kwa maana leo ameteremka, akatoa sadaka ya ng'ombe, vinono na kondoo wengi na amewakaribisha wana wa mfalme, Yoabu jemadari wa jeshi, na kuhani Abiathari, na, tazama, wanakula na kunywa mbele yake, na kusema, ‘Uishi mfalme Adoniya!’ Lakini hakunialika mimi, mtumishi wako wala kuhani Sadoki, wala Benaya mwana wa Yehoyada na mtumishi wako Solomoni. Je, yote haya umeyafanya wewe bwana wangu, mfalme, bila kuwaambia watumishi wako mtu atakayekaa juu ya kiti chako cha enzi baada yako?” Naye mfalme Daudi akajibu, “Niitie Bathsheba.” Bathsheba alimwendea mfalme na kusimama mbele yake. Halafu mfalme aliapa akisema, “Kama Mwenyezi-Mungu aishivyo, aliyekomboa roho yangu katika taabu nyingi, kama nilivyokuapia mbele za Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nikisema, ‘Mwanao Solomoni atatawala baada yangu, na kwamba atakaa juu ya kiti changu cha enzi badala yangu,’ ndivyo nitakavyofanya leo.” Ndipo Bathsheba alipoinama mpaka chini, akamsujudia mfalme, na kusema “Bwana wangu, mfalme Daudi, aishi milele!” Kisha mfalme Daudi akasema, “Niitie kuhani Sadoki, nabii Nathani na Benaya mwana wa Yehoyada.” Nao wakamjia mfalme. Naye mfalme akawaambia, “Nenda na watumishi wangu mimi bwana wako, umpandishe mwanangu Solomoni juu ya nyumbu wangu, umpeleke Gihoni; halafu umruhusu kuhani Sadoki na nabii Nathani wampake mafuta kuwa mfalme wa Israeli; baadaye pigeni tarumbeta na kusema, ‘Mfalme Solomoni aishi!’ Nanyi mtamfuata, naye atakuja na kuketi juu ya kiti changu cha enzi badala yangu; nami nimemteua kuwa mtawala juu ya Israeli na juu ya Yuda.” Ndipo Benaya mwana wa Yehoyada alipomjibu mfalme, “Amina! Bwana Mungu wa bwana wangu mfalme, na anene vivyo hivyo. Kama Mwenyezi-Mungu alivyokuwa na bwana wangu mfalme, awe pia na Solomoni, na akikuze kiti chake cha enzi kuliko kiti cha enzi cha bwana wangu mfalme Daudi.”

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na 1 Wafalme 1:22-37