1 Wafalme 3:1-28
1 Wafalme 3:1-28 BHN
Solomoni alifanya ushirikiano na Farao mfalme wa Misri, kwa kumwoa binti yake. Akamleta binti Farao na kumweka katika mji wa Daudi, mpaka alipomaliza kujenga nyumba yake mwenyewe, nyumba ya Mwenyezi-Mungu, na ukuta wa kuuzunguka mji wa Yerusalemu. Kabla yake, watu walikuwa wakitoa tambiko vilimani, kwa kuwa nyumba ya Mungu ilikuwa bado haijajengwa. Solomoni alimpenda Mwenyezi-Mungu, akazingatia maongozi ya Daudi, baba yake; ila tu, naye ilimbidi kutoa tambiko na kufukiza ubani vilimani. Wakati mmoja, Solomoni alikwenda kutoa tambiko huko Gibeoni, maana palikuwa ndipo mahali maarufu pa ibada. Ilikuwa ni kawaida ya Solomoni kutoa maelfu ya sadaka za kuteketezwa katika madhabahu hiyo. Huko Gibeoni, Mwenyezi-Mungu alimtokea Solomoni katika ndoto usiku, akamwambia, “Omba chochote nami nitakupa.” Solomoni akamwambia, “Ulimwonesha mtumishi wako Daudi, baba yangu, fadhili nyingi, kwa sababu alikutumikia kwa uaminifu, uadilifu na kwa haki; na umedumisha fadhili zako kwa kumpa mwana anayeketi sasa kwenye kiti chake cha enzi. Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, umeniweka mimi mtumishi wako kuwa mfalme mahali pa baba yangu Daudi, ijapokuwa ningali mtoto mdogo na sijui namna ya kutekeleza wajibu huu. Na hapa umeniweka kati ya watu wako ambao umewachagua; nao ni wengi hata hawawezi kuhesabika kwa wingi wao. Kwa hiyo, nakuomba unipe mimi mtumishi wako moyo wa kusikia ili kuamua watu wako, niweze kutambua mema na mabaya; maana ni nani awezaye kuhukumu watu wako walio wengi hivi?” Ombi hili la Solomoni lilimfurahisha Mwenyezi-Mungu, naye akamwambia, “Kwa kuwa umetoa ombi hili, na hukujiombea maisha marefu au mali, na wala hukuomba adui zako waangamizwe, bali umejiombea utambuzi wa kutoa hukumu au kutenda haki basi, sasa nakutimizia kama ulivyoomba. Tazama, nakupa hekima na akili kiasi ambacho hapana mtu mwingine aliyepata kuwa nacho kabla yako, na wala hatatokea mwingine kama wewe baada yako. Pia, nitakupa yale ambayo hukuomba: Nitakupa utajiri na heshima zaidi ya mfalme mwingine yeyote wa nyakati zako. Tena kama ukifuata njia na maagizo yangu na kushika amri zangu kama alivyofanya baba yako Daudi, basi, nitakupa maisha marefu.” Solomoni alipoamka, alitambua kwamba ilikuwa ndoto. Ndipo akarudi Yerusalemu, akasimama mbele ya sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu, akamtolea tambiko za kuteketezwa na za amani. Halafu akawafanyia karamu watumishi wake wote. Siku moja, wanawake wawili makahaba, walikwenda kwa mfalme Solomoni. Mmoja wao akasema, “Ee bwana wangu, mimi na huyu mwenzangu tunakaa nyumba moja; mimi nilijifungua mtoto wakati huyu dada yumo nyumbani. Siku tatu baadaye, huyu naye alijifungua mtoto. Hapakuwa na mtu mwingine nyumbani ila sisi wawili tu. Halafu, usiku mmoja, mtoto wake alifariki kwa sababu alimlalia. Kisha akaamka usiku wa manane, akamchukua mwanangu kutoka kwangu wakati mimi nipo usingizini, akamlaza kifuani pake. Halafu akaichukua maiti ya mwanawe, akailaza kifuani pangu. Nilipoamka asubuhi na kutaka kumnyonyesha mwanangu, nikakuta mtoto amefariki. Nilipochunguza sana, nikagundua kuwa hakuwa mwanangu niliyemzaa.” Lakini yule mwanamke mwingine akasema, “Hapana! Wa kwangu ndiye aliye hai na wa kwako ndiye aliyekufa”. Naye mwanamke wa kwanza akasema, “La! Mtoto wako ndiye aliyekufa, wangu ni huyo aliye hai!” Basi, wakaendelea kubishana hivyo mbele ya mfalme. Ndipo mfalme Solomoni akasema, “Kila mmoja wenu anadai kwamba, mtoto wake ndiye aliye hai na kwamba aliyekufa si wake.” Basi, mfalme akaagiza: “Nileteeni upanga!” Wakamletea mfalme upanga. Mfalme akasema: “Mkate mtoto aliye hai vipande viwili, umpe mmoja nusu na mwingine nusu.” Yule mwanamke aliyekuwa mama yake huyo mtoto aliye hai alishikwa na huruma juu ya mwanawe, akamwambia mfalme, “Tafadhali mfalme, msimuue mtoto. Mpe mwenzangu huyo mtoto aliye hai, amchukue yeye.” Lakini yule mwanamke mwingine akasema, “La! Mtoto asiwe wangu wala wake. Mkate vipande viwili.” Mfalme Solomoni akasema, “Usimuue mtoto! Mpe mwanamke wa kwanza amchukue, kwani yeye ndiye mama yake.” Watu wote wa Israeli waliposikia juu ya hukumu ya mfalme, walimwogopa, wakatambua kwamba alikuwa na hekima ya Mungu iliyomwezesha kutoa hukumu.