Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 6:1-18

1 Wafalme 6:1-18 BHN

Solomoni alianza kujenga nyumba ya Mwenyezi-Mungu katika mwaka wa 480 baada ya Waisraeli kutoka Misri. Huo ulikuwa mwaka wa nne wa utawala wa Solomoni juu ya Israeli, katika mwezi wa Zifu, yaani mwezi wa pili. Nyumba hiyo ambayo mfalme Solomoni alimjengea Mwenyezi-Mungu ilikuwa na urefu wa mita 27, upana wa mita 9, na kimo cha mita 13.5. Ukumbi wa sebule ya nyumba ulikuwa na upana wa mita 4.5 toka upande mmoja wa nyumba mpaka upande mwingine. Na kina chake mbele ya hiyo nyumba kilikuwa mita 9. Aliiwekea nyumba hiyo madirisha mapana kwa ndani na membamba kwa nje. Pia alijenga nguzo kuzunguka, ili kutegemeza ukuta wa nje; akatengeneza na vyumba vya pembeni kila upande. Vyumba vya chini, katika hivyo vyumba vya nyongeza, vilikuwa na upana wa mita 2.25, na ghorofa iliyofuata ilikuwa na upana wa mita 2.75, na ghorofa ya juu kabisa ilikuwa na upana wa mita 3. Ghorofa hizo zilikuwa zimetofautiana kwa upana, kwa sababu Solomoni alikuwa amepunguza kiasi ukuta wa nje kuzunguka nyumba, ili boriti za kutegemeza jengo zisishikamane na kuta. Wakati nyumba ilipokuwa inajengwa, hapakusikika ndani ya nyumba mlio wa nyundo, wala wa chombo chochote cha chuma, maana ilijengwa kwa mawe yaliyokuwa yamechongwa na kutayarishwa kabisa huko yalikochukuliwa. Mlango wa kuingilia sehemu ya chini ya jengo lililoongezwa ubavuni mwa nyumba, ulikuwa upande wa kusini. Ndani, mlikuwa na ngazi ambayo watu waliweza kupanda ili kwenda ghorofa ya katikati na ya mwisho. Hivyo, Solomoni aliijenga nyumba, ikamalizika. Dari ya nyumba alikuwa ameitengeneza kwa boriti na mbao za mierezi. Kuuzunguka ukuta wa nje wa nyumba hiyo, alijenga vyumba vya ghorofa vyenye kimo cha mita 2.25; navyo vilikuwa vimeunganishwa na nyumba kwa boriti za mierezi. Wakati huo, ujumbe huu wa Mwenyezi-Mungu ukamjia Solomoni, “Kuhusu nyumba hii unayoijenga, kama ukifuata maongozi yangu, ukayatii maagizo yangu na amri zangu, nitakutimizia mambo yote niliyomwahidi baba yako Daudi. Mimi nitakaa miongoni mwa wazawa wa Israeli, na sitawaacha kamwe watu wangu, Israeli.” Hivyo, Solomoni akaijenga nyumba na kuimaliza. Upande wa ndani wa kuta za nyumba aliufunika kwa mbao za mierezi, kutoka sakafuni mpaka kwenye boriti za dari; na sakafu akaitandika mbao za miberoshi. Chumba cha ndani, kilichoitwa mahali patakatifu sana, kilijengwa katika sehemu ya nyuma ya nyumba. Kilikuwa kimejengwa kwa mbao za mierezi kutoka sakafuni hadi darini, na urefu wake ulikuwa mita 9. Nyumba ile iliyokuwa mbele ya mahali patakatifu sana, ilikuwa na urefu wa mita 18. Mbao za mierezi zilizotanda ukuta wa nyumba kwa ndani zilikuwa zimepambwa kwa michoro ya mibuyu na maua yaliyochanua. Kila sehemu ilikuwa imefunikwa kwa mbao za mierezi, wala hapana jiwe lililoonekana.