Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wakorintho UTANGULIZI:

UTANGULIZI:
Baada ya kutembelea Korintho kwa mara ya kwanza, wakati ambapo Paulo alianzisha kanisa hilo, aliwaandikia barua ambayo anaitaja katika 1Kor 5:9-13, ambayo haikuhifadhiwa wala kutufikia sisi. Baadaye Wakristo wa Korintho walimwandikia Paulo wakimweleza matatizo yao. Paulo aliandika ile barua inayojulikana sasa kama ya kwanza kwa Wakorintho ili kutatua matatizo hayo. Wakati alipoandika barua hiyo ya kwanza alikuwa amekusudia kuwatembelea tena Wakorintho mara ya pili (1Kor 16:3,5-6). Safari hiyo ya pili ilikuwa ya shida, na uhusiano kati yake na Wakorintho ukawa umezorota sana (2Kor 2:1). Hata hivyo inaonekana kwamba Paulo alitaka kuwatembelea tena (2Kor 1:15–2:1) lakini badala yake akawaandikia barua hii tunayojifunza sasa ambayo kwa kiasi inaonesha wasiwasi wake.
Mazingira ya karibu sana na ambayo yalisababisha barua hii iandikwe ni kwamba Paulo alikuwa anasafiri kwenda Troa kutoka Efeso (2Kor 2:12) na kwa kuwa hakumkuta Tito kule Troa aliendelea mpaka Makedonia ambako alimkuta amewasili kutoka Korintho. Tito alimpa Paulo habari nzuri kwamba Wakorintho walitaka tena kuwa na uhusiano mzuri naye (2Kor 7:5-13). Barua hii ya pili kwa Wakorintho iliandikwa katika mazingira hayo.
Muundo wa Barua hii na yaliyomo
Barua hii, kama kawaida ya barua nyingi za Paulo, inaanza na utangulizi au maneno ya kuanzia (1:1-11) na utangulizi huo unatuongoza katika sehemu kuu ya barua yenyewe ambayo imegawanyika katika visehemu vitatu: Sura 1:12–7:16; 8:1–9:15; 10:1–13:10 na kumalizia kwa maneno ya kuwaaga na kuwatakia walengwa baraka (13:11-14).
Katika sehemu ya kwanza, 1:12–7:16, Paulo anawaza juu ya uhusiano kati yake na Wakristo wa Korintho wahusika hapa na katika sura 12-13 anatoa sababu za kuacha kuwatembelea, anatetea kwa nguvu sana huduma yake ya kitume ambayo ni “huduma ya Roho Mtakatifu”, huduma “yenye kuleta upatanisho”.
Katika sehemu ya pili, 8:1–9:15, kwa jumla tuna habari juu ya kuwapa msaada waumini wa Yerusalemu ambao walikuwa katika hali ngumu ya mahitaji ya kawaida (Rom 15:26). Paulo anawataka Wakorintho wajihusishe kikamilifu katika kutoa mchango wao.
Na katika sehemu ya tatu, 10:1–13:10, Paulo anarudia tena kuzungumzia juu ya huduma yake ya kitume kwa kutaka achukuliwe na kuheshimiwa kama mtume halisi.

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia