2 Samueli 1
1
Daudi anahabarishwa juu ya kifo cha Shauli
1Baada ya kifo cha Shauli, Daudi alirudi baada ya kuwashinda Waamaleki, akakaa Siklagi kwa muda wa siku mbili. 2Siku iliyofuata, mtu mmoja kutoka kambi ya Shauli, mavazi yake yakiwa yamechanwa kwa huzuni na akiwa na mavumbi kichwani alimwendea Daudi. Alipomfikia Daudi, alijitupa chini mbele yake akamsujudia. 3Daudi akamwambia, “Unatoka wapi?” Naye akamwambia, “Nimetoroka kutoka kambi ya Waisraeli.” 4Daudi akamwambia, “Niambie mambo yalivyokuwa huko.” Yule mtu akamjibu, “Watu wetu wameyakimbia mapigano na wengi wetu wameuawa. Zaidi ya hayo, Shauli na mwanawe Yonathani pia wameuawa.” 5Daudi akamwuliza yule kijana, “Unajuaje kuwa Shauli na Yonathani mwanawe wamekufa?”
6Yule kijana akamjibu, “Kwa bahati, nilikuwapo mlimani Gilboa. Nilimwona Shauli ameegemea mkuki wake na magari ya wapandafarasi ya adui zake yalikuwa yanamsonga sana. 7Shauli alipotazama nyuma, aliniona, akaniita. Nilipoitika, 8yeye aliniuliza mimi ni nani, nami nikamwambia kuwa mimi ni Mmaleki. 9Hapo, akaniambia, ‘Karibia uniue maana nimejeruhiwa vibaya na maumivu ni makali. Lakini bado ningali hai’. 10Hivyo, nilikwenda karibu naye na kumuua, kwa sababu nilikuwa na uhakika kuwa akianguka chini, hataweza kuishi zaidi. Lakini taji iliyokuwa kichwani pake na kikuku kilichokuwa mkononi mwake, vyote nimekuletea wewe, bwana wangu.”
11Daudi akayashika mavazi yake na kuyararua kwa huzuni. Hata watu waliokuwa pamoja na Daudi wakafanya vivyo hivyo. 12Wakaomboleza, wakalia na kufunga mpaka jioni kwa ajili ya Shauli, Yonathani mwanawe, na nchi ya Waisraeli, watu wa Mwenyezi-Mungu, kwa kuwa wengi wao waliuawa vitani. 13Daudi akamwuliza yule kijana aliyempasha habari, “Unatoka wapi?” Yeye akajibu, “Mimi ni Mmaleki, lakini ninaishi katika nchi yako kama mgeni.” 14Daudi akamwuliza, “Ilikuwaje wewe hukuogopa kuunyosha mkono wako na kumuua mtu aliyeteuliwa na Mwenyezi-Mungu kwa kupakwa mafuta?” 15Kisha, Daudi akamwita mmoja wa vijana wake akamwambia, “Muue mtu huyu!” Yule kijana alimpiga yule Mmaleki, naye akafa. 16Daudi akasema, “Uwajibike wewe mwenyewe kwa kifo chako, maana umejishuhudia wewe mwenyewe kwa mdomo wako ukisema, ‘Nimemuua mtu aliyeteuliwa na Mwenyezi-Mungu kwa kupakwa mafuta.’”
Daudi aomboleza kifo cha Shauli na Yonathani
17Daudi aliimba ombolezo lifuatalo kwa ajili ya Shauli na mwanawe Yonathani. 18Daudi alisema watu wa Yuda wafundishwe ombolezo#1:18 ombolezo: Kiebrania: Upinde. hilo, nalo limeandikwa katika kitabu cha Yashari.#1:18 Yashari: Au Mnyofu. Daudi aliimba,
19“Walio fahari yako, ee Israeli,
wameuawa milimani pako.
Jinsi gani mashujaa walivyoanguka!
20Jambo hilo msiuambie mji wa Gathi
wala katika mitaa ya Ashkeloni.
La sivyo, wanawake Wafilisti watashangilia,
binti za wasiotahiriwa, watafurahi.
21“Enyi milima ya Gilboa,
msiwe na umande au mvua juu yenu.
Wala mashamba yenu#1:21 mashamba yenu: Kiebrania: Mashamba ya dhabihu. daima yasitoe chochote.
Maana huko ngao za shujaa zilitiwa najisi,
ngao ya Shauli haikupakwa mafuta.
22“Upinde wa Yonathani kamwe haukurudi nyuma,
upanga wa Shauli kamwe haukurudi bure,
daima ziliua wengi.
Naam, ziliua mashujaa.
23“Shauli na Yonathani,
watu wa ajabu na wakupendeza.
Maishani na kifoni hawakutengana.
Walikuwa wepesi kuliko tai,
naam, wenye nguvu kuliko simba.
24“Wanawake wa Israeli, mlilieni Shauli!
Aliwavika mavazi mekundu ya fahari,
aliyatarizi mavazi yenu kwa dhahabu.
25“Jinsi gani mashujaa walivyoanguka!
Wamekufa wakiwa katika mapambano.
Yonathani analala,
akiwa ameuawa milimani.
26Nasikitika kwa ajili yako, ndugu yangu Yonathani.
Umekuwa kwangu daima mtu wa kupendeza,
pendo lako kwangu limekuwa la ajabu,
la ajabu kuliko la mwanamke.
27“Jinsi gani mashujaa wameanguka,
na silaha zao zimeachwa, hazina kazi.”
Iliyochaguliwa sasa
2 Samueli 1: BHN
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.