Matendo 2:22-41
Matendo 2:22-41 BHN
“Wananchi wa Israeli, sikilizeni maneno haya! Yesu wa Nazareti alikuwa mtu ambaye mamlaka yake ya kimungu yalithibitishwa kwenu kwa miujiza, maajabu na ishara Mungu alizofanya kati yenu kwa njia yake, kama mnavyojua. Kufuatana na mpango wake mwenyewe Mungu alikwisha amua kwamba Yesu angetiwa mikononi mwenu; nanyi mkamuua kwa kuwaachia watu wabaya wamsulubishe. Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, akamwokoa katika maumivu ya kifo kwa maana haingewezekana kabisa kifo kimfunge. Maana Daudi alisema juu yake hivi: ‘Nilimwona Bwana mbele yangu daima; yuko nami upande wangu wa kulia hata sitatikisika. Kwa hiyo, moyo wangu ulifurahi; tena nilipiga vigelegele vya furaha. Mwili wangu utakaa katika tumaini, maana hutaiacha roho yangu kuzimu, wala kumruhusu mtakatifu wako aoze. Umenionesha njia za uhai, umenijaza furaha kwa kuwako kwako!’ “Ndugu zangu, napenda kuwaambieni waziwazi juu ya mambo yaliyompata Daudi, babu yetu. Yeye alikufa, akazikwa, tena kaburi lake liko papa hapa petu mpaka leo. Lakini kwa vile Daudi alikuwa nabii, alijua kuwa Mungu alimwapia kiapo kwamba atamtawaza mmoja wa uzawa wake kuwa mfalme mahali pake. Daudi aliona kabla mambo yatakayofanywa na Mungu na hivyo akasema juu ya ufufuo wa Kristo wakati aliposema: ‘Hakuachwa kuzimu, mwili wake haukuoza.’ Basi, Mungu alimfufua huyo Yesu na sisi sote ni mashahidi wa tukio hilo. Yesu alipokwisha pandishwa na kuwekwa na Mungu upande wake wa kulia, akapokea kutoka kwake Baba yule Roho Mtakatifu ambaye alituahidi, ametumiminia huyo Roho. Hicho ndicho mnachoona sasa na kusikia. Maana Daudi mwenyewe, hakupanda mpaka mbinguni; ila yeye alisema: ‘Bwana alimwambia Bwana wangu: Keti upande wangu wa kulia, hadi niwafanye adui zako kiti cha miguu yako.’ “Watu wote wa Israeli wanapaswa kufahamu kwa hakika kwamba huyo Yesu mliyemsulubisha, ndiye huyo ambaye Mungu amemfanya kuwa Bwana na Kristo.” Basi, watu waliposikia hayo, walichomwa moyo, wakawauliza Petro na wale mitume wenzake: “Ndugu zetu, tufanye nini?” Petro akajibu, “Tubuni na kila mmoja wenu abatizwe kwa jina la Yesu Kristo ili mpate kuondolewa dhambi zenu na kupokea ile ahadi ya Roho Mtakatifu. Maana, ahadi ile ilikuwa kwa ajili yenu, kwa ajili ya watoto wenu, kwa ajili ya wote wanaokaa mbali na kwa ajili ya kila mtu ambaye Bwana Mungu wetu atamwita kwake.” Kwa maneno mengine mengi, Petro alisisitiza na kuwahimiza watu akisema, “Jiokoeni katika kizazi hiki kiovu.” Wengi waliyakubali maneno yake, wakabatizwa. Watu wapatao 3,000 wakaongezeka katika kile kikundi siku hiyo.